ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton, ameelezea masikitiko yake alipojitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu ashindwe kwenye Uchaguzi wa Marekani na mgombea kutoka Chama cha Republican, Donald Trump.
Hillary, akihutubia mjini Washington DC, amesema alikuwa hataki kutoka tena nyumbani.
Ameliambia Shirika la Kulinda Watoto (CDF) kwamba uchaguzi huo umewafanya Wamarekani wengi kutafakari.
Hillary aliongoza kwa wingi wa kura za kawaida, lakini akashindwa kinyang’anyiro cha urais kupitia kura za uwakilishi, ambazo ndizo huamua mshindi wa urais.
“Sasa, nikiri kuwa ujio wangu hapa halikuwa jambo rahisi,” alisema baada ya kutunukiwa tuzo ya heshima na shirika hilo.
“Kuna nyakati kadhaa wiki moja iliyopita ambapo nilitaka kujikunyata tu nikiwa na kitabu kizuri na nisitoke nje ya nyumba tena.”
Aliendelea: “Ninajua wengi wenu mmevunjika moyo na matokeo ya uchaguzi huu. Hata mimi pia, zaidi kushinda ninavyoweza kueleza.”
“Ninajua si jambo rahisi. Najua wiki moja iliyopita, watu wengi wamekuwa wakijiuliza iwapo Marekani ni nchi ambayo tumekuwa tukiiamini hivyo.
“Migawanyiko iliyowekwa wazi na uchaguzi huu imekolea, lakini tafadhali nisikuze mambo ninaposema hili. Marekani ni ya thamani. Watoto wetu ni wa thamani. Kuweni na imani katika nchi yetu, mpiganie maadili yetu na daima, msikate tama.”
Alipokuwa anatoa hotuba ya kukubali kushindwa wiki iliyopita, Hillary alisema kuwa Trump anafaa kupewa fursa ya kuongoza.
Tangu wakati huo, amekuwa haonekani, ingawa siku moja alionekana akifanya matembezi porini.
Aidha kwenye mawasiliano ya simu ambayo yalifichuliwa kwa wanahabari wa Marekani, alisikika akimlaumu Mkurugenzi Mkuu wa FBI, James Comey, aliyetangaza kuanzishwa kwa uchunguzi mpya kuhusu kashfa yake ya barua pepe, zikiwa zimesalia siku 11 kabla ya uchaguzi kufanyika.
Lakini uchaguzi ulipokaribia, Comey alisema hakukupatikana ushahidi mpya ambao ungebadilisha uamuzi wa awali wa FBI wa kutokuwapo ushahidi wa kumfungulia mashtaka.