22.7 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Hatuwezi kushinda hivihivi

DSC_3936NA WAANDISHI WETU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kampeni za urais Zanzibar huku mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, akisema hawawezi kushinda bila kujipanga vyema.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo katika Uwanja wa Demokrasia wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.

“Hatuwezi kushinda hivi hivi, ni lazima tujipange vizuri, uchaguzi wa mwaka huu ni man to man (mtu na mtu)

“Lazima umjue mtu wako vizuri, umkabe ipasavyo, uombe kura na uipate. Uchaguzi huu pia ni kiambo kwa kiambo, nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, shuka kwa shuka,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa.

Alisema kutokana na umati mkubwa uliojitokeza katika mkutano huo, ni dhahiri chama hicho kimeshinda na kwamba wengine wataendelea kuwa wasindikizaji.

“Huu umati unaonyesha ni jinsi gani tulivyoshinda, wengine wataendelea kuwa wasindikizaji na wale wasindikizaji wazoefu wataendelea kutusindikiza tu,” alisema.

Alisema CCM ina haki ya kuchaguliwa tena kutokana na kuongoza nchi vyema na kwamba pale ambako amani ilikosekana ilisababishwa na wengine.

Rais Kikwete aliwaambia wananchi hao kuwa wasiwape nafasi tena wapinzani na kwamba Zanzibar itendelea kuwa na amani endapo watamchagua Dk. Ally Mohamed Shein.

Rais Kikwete alimrushia kijembe mgombea urais wa CUF, Maalim  Seif Sharif Hamad, ambaye anadai Serikali ya Zanzibar haijafanya maendeleo yoyote wakati alikuwa sehemu ya Serikali hiyo kama makamu wa kwanza wa rais na alishindwa kuleta maendeleo.

Rais Kikwete alitumia hotuba yake kwa njia ya maswali ambapo alikuwa akiwauliza wananchi nao walijibu huku wakimshangilia.

“CCM imeongoza vema na nchi imetulia, Zanzibar imetulia haijatulia? …ambapo wananchi wakiitikia…imetulia

“Hao wanaolalamika msiwape, ni jambo la kusikitisha hao wanaolalamika wako kwenye Serikali, kama mtu ni Makamu wa Rais halafu anasema Serikali imeshindwa kwa nini hajiuzulu?

“Huwezi kuwa kwenye serikali, wewe mwenyewe ni makamu wa kwanza wa rais halafu serikali hiyo haina maendeleo sasa kwanini hujaondoka, msiwape nafasi…washindwe,”alisema Rais Kikwete.

Alieleza kushangazwa na watu ambao wamekuwa wakisema Dk. Shein ni mpole wakati hekima na busara zake ndivyo vilivyomfikisha hapo huku wengine wakifanya fujo.

“Hao wanaofanya fujo waendelee kuwa wa pili lakini Shein ni mzalendo wa kweli na ana uchungu na Zanzibar, hana sura mbili na hana ndimi mbili lakini anayo sura moja ya kizanzibari, anayo lugha moja ya kutetea mapinduzi na kulinda muungano.

Dk. Shein

Kwa upande wake, mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk. Shein alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali yake imelinda mapinduzi na ataendelea kulinda kwa kuwa hakuna maendeleo bila mapinduzi.

“Tutaendelea kuyalinda mapinduzi yetu kwa sababu ndiyo ngao na nguzo  na hakuna amani na mshikamano bila mapinduzi,”alisema.

Alisema sera ya CCM ya kujenga umoja wa kitaifa, amani na utulivu ni nguzo ya pili.

“Amani ni msingi mkubwa ya maendeleo ya dunia nzima. Amani hii haikuja bure, ilitafutwa kwa udi na uvumba.  Hadi leo amani ndiyo sera yetu kubwa na tutaendelea kuidumisha.

“Nimekabidhiwa ilani leo na Rais Kikwete tutahubiri amani. Amani itabakia amani, kupendana baina ya bara na visiwani, Zanzibar na wapemba sote ni wamoja ni ndugu. Tutaendeleza amani hii kwa miaka mitano ijayo,”alisema mgombea huyo.

Alisema uzoefu alioupata kuongoza Zanzibar ilihitaji uvumilivu wa hali ya juu na kwamba kutokana na uzoefu huo hatashindwa kuendeleza amani.

“Nilipata kusema katika uchaguzi uliopita kuwa sitaogopa mtu leo narudia sitaogopa mtu yeyote bali Mwenyezi Mungu. Nitajenga heshima yangu na wao wanijengee heshima. Nitafanya hivyo kwa kipindi kijacho nitaitetea Zanzibar na Tanzania nzima,”alisema.

MUUNGANO

Alisema Muungano ni suala la msingi kwa kuwa hakuna mbadala mwingine na kwamba hakuna muungano nchi nyingine Afrika iliyoweza kudumisha.

“Ni lazima tufanye uamuzi wa pamoja wa kumchagua Dk. John  Magufuli na Samia Suluhu Hassani. Wala msidanganyike, msitishike na hakuna mtu au kikundi cha watu ambacho kitaweza kuvunja muungano.

“Nyerere na karume waliunganisha kwa ridhaa ya wananchi wenyewe hivyo hauwezi kuvunjwa na mtu mmoja. Hawawezi kututishia kwa kauli nasema haiwezekani mambo haya yana taratibu zake. Muungano ni jambo kubwa sana, tutaendelea kuutetea kwa nguvu zetu zote.

UCHUMI

Alisema tayari serikali imekwishatunga sheria ya mafuta na kwamba hawatanii katika hilo na kwamba wameshaandika maelewano ya awali ili watoe kibali ya kuanza kuchimba gesi.

Aidha alisema jitihada za utaalamu wa hali ya juu zikifanyika baada ya miaka mitano au sita wataanza kuchimba mafuta.

“Mambo yakipamba moto wataalamu hawa watafanya hivyo na hili litainua uchumi wa nchi yetu.

“Kuhusu Barabara, huduma za afya, elimu, yote nitaeleza mambo mazuri kweli  kweli yote yapo humu kwenye ilani. Nitafanunua kinagaubaga  katika mikutano yangu ya kampeni.

“Wote wanaopenda maendeleo yetu waje wanichague mimi, tuko 14 lakini CCM ndiyo namba moja. Kazi hiyo tutaikamilisha tukimchagua Magufuli na Samia Suluhu,”alisema.

Dk. Shein ambaye alihitimisha hotuba yake saa 11:55 jioni, aliwataka wananchi hao kutunza vitambulisho vyao kwa kuwa kuna watu wanaviwangia.

“Vitunzieni vitambulisho vyetu kuna watu wanaziwangia, mvitunze mpaka Oktoba 25, wembe ni ule ule. Mko tayari?,” Dk. Shein aliwahoji wananchi hao huku akijibiwa; “Tupo tayari”.

Awali Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema anamshangaa Maalim Seif aliposema kuwa endapo atachaguliwa ataibadilisha Zanzibar kuwa kama Singapore wakati chama chake kina nusu ya baraza la mawaziri.

“Wana nusu ya baraza la mawaziri. Tulitarajia angetupa nusu ya Singapore, aache kutudanganya, alikuwa waziri kiongozi hakuleta Singapore. Kashagombea mara nne, sasa ni mara ya tano na hapati tumwambie bye bye,”alisema Kinana.

Bilal

Naye Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal katika mkutano huo aliwataka wananchi waache tofauti zao na kuwa kitu kimoja ili waweze kushinda kwenye  uchguzi huo.

“Huu ni mkutano wa aina yake kwa kuwa sijawahi kuona watu kuwa wengi hapa Kibanda maiti kama hivi, nafahamu kuja huku ni kutaka kufahamu juu ya wasiwasi  mliokuwa nao juu ya  uongozi wa nchi hii,”alisema Dk Bilal.

Dk. Bilal alisema anawaombea tiketi wagombea wao wa  urais ambao ni  Dk. John Magufuli, Samia Suluhu, Dk. Mohamed Shein, wakiwamo na wagombea wa nafasi nyingine za uongozi kama vile ubunge, udiwani, uwakilishi na  udiwani.

“Nyerere alisema nchi yetu itayumba bila ya uongozi wa CCM hivyo mkae  mtulie mtafakari, wagombea wote hao ndio watakao tuwezesha kushinda pia nawaomba tusahau tofauti zetu ili tuwe wamoja,”alisema Dk Bilal.

Mwinyi

Naye Rais Mataafu Ally Hassani Mwinyi alisema amekuwapo katika ufunguzi huo ili kuhakikisha ushindi unapatikana kwa chama chake katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

“Leo ni siku ya kulala pamoja ambapo tukiondoka kila mmoja wetu anajua nafasi yake ili CCM ishinde na kura zote tumpe Dk Shein.

“Mliopo hapa mmeiona hatari inayowakabili wapinzani, hali kama hii sijapata kuiona mahali popote Zanzibar, Mwenyezi Mungu yupo kwa wengi na sisi ndio wengi,”alisema Mwinyi.

Mkapa

Rais Mstaafu Benjamini Mkapa alisema kwamba anaimani na Dk. Shein kwa kuwa amefanyanaye  kazi na kupata nafasi ya kuufatilia uongozi wake alipokuwa na Rais Jakaya Kikwete akiwa kama makamu wa rais.

“Amedhihirisha umakini , uadilifu, pamoja na uchapakazi wake nina imani anastahili kupewa kipindi kingine cha uongozi wa Zanzibar kwa kuwa tunataka kiongozi atakayeenzi muungano wa nchi hii na asiyesahau wakombozi wa taifa hili.

“Zaidi ya hapo muwe na imani mikononi mwake taifa litakuwa salama hivyo wapigieni kura wanaCCM zaidi ni  fahari sana kwangu nina imani na Dk. Shein, shein kweli… Kweli, Mna imani na Shein? Mikono juu,”alisema Mkapa.

Naye Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Karume alisema ni hekima kwa CCM kukubali mfumo wa vyama vingi na kudai kwamba ni muhimu kwa wananchi kuisimamia na kuilinda amani ili nchi iendelee kuwa na umoja.

Pia rais huyo mstaafu alihoji kwa baadhi ya wanasiasa wanaotumia lugha ya matusi wakiwa jukwaani kama ni lazima wafanye hivyo.

“Kwani lazima  wanasiasa wanapokuwa jukwaani watukane? Mimi sina tabia ya kumsema mtu kwa kuwa baada ya kumsimfu baadae utaanza kumkashifu,” alisema.

Awali watu walianza kuingia katika uwanja huo saa sita mchana huku wakiongezeka kadri muda ulivyokuwa unakwenda, huku vikundi mbalimbali vya burudani vikiendelea kutumbuiza.

Dk Shein aliingia uwanjani hapo akiambatana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali hku ulinzi ukiimarishwa kila kona ya uwanja huo.

Wasanii mbali mbali waliotumbuiza kampeini hizo mbali na Diamond Platinums, Mzee Yusuph, Peter Msechu na Amini.

Elizabeth Hombo, ADAM MKWEPU, DAR na Arodia Peter Zanzibar

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles