22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Tumewakamata pabaya

1

*Sumaye asema hakuna wa kukifufua chama hicho

NA MAREGESI PAUL, KIOMBOI na Shabani Matutu Dar

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa,  amesema wamekikamata pabaya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa Watanzania sasa wanataka mabadiliko.

Amesema pia kwamba, kitendo cha mamilioni ya Watanzania kutaka mabadiliko, pia kinaungwa mkono na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wanaokosoa Ukawa, wawe na hoja za msingi badala ya kutukana.

Lowassa aliyasema hayo mjini Kimboi, Jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kiomboi Bomani.

“Nimekuja hapa kwa heshima kubwa ili niwaombe kura kwa sababu uchaguzi ni mchezo wa hesabu, bila kura za kutosha hatuingii Ikulu ng’o.

“Nawaambia tusiwapowashinda mwaka huu, hatutawashinda tena, lazima waondoke kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko, tunazo baraka za Mungu na Mwalimu Nyerere.

“Wameanza kutuiga lakini wajue tunayoyafanya tumetoka nayo mbali, tumewakamata pabaya kwa sababu wananchi wanataka mabadiliko na sisi tuko tayari kwa mabadiliko, mabadiliko haya ni ‘unstoppable (hayazuiliki),”alisema Lowassa.

Akizungumzia ajira kwa vijana, Lowassa alisema atakapoingia madarakani, Serikali yake itaanzisha Benki kwa ajili ya vijana wanaoendesha boda boda pamoja na benki ya wachimbaji wadogo wadogo.

Kwa mujibu wa Lowassa, sekta nyingine zitakuwa zikipatiwa ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili kulingana na wakati husika.

“Nasema tutaondoa umasikini nchini kwa sababu nitaunda Serikali inayofanya kazi kwa kasi na asiyekuwa na uwezo wa kukabiliana na kasi yetu, atupishe.

Awali akihutubia mkutano mwingine katika Kijiji cha Ilogelo Jimbo la Singida Kaskazini, mgombea urais huyo alisema kama Watanzania hawatapiga kura za kuiondoa CCM madarakani, watakuwa wamejiangamiza.

Alisema kwamba, ingawa CCM wamekuwa wakitoa ahadi nyingi kwa wananchi, wamekuwa hawatekelezi ahadi hizo, jambo linalowafanya Watanzania wasiwe tena na sababu ya kukiamini chama hicho.

“CCM hawataki mabadiliko ingawa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Watanzania wasipopata mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM.

“Najua wananchi wanataka mabadiliko ndiyo maana niliwahi kusema siwezi kuzuia mafuriko kwa mikono lakini wakanidharau.

“Matokeo yake sasa yanaonekana kwa sababu  tulipokwenda Iringa, mafuriko yalikuwa ni haya haya, tulipokwenda Ruvuma, mafuriko ni haya haya, tulipokwenda Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma, mafuriko yalikuwa ni haya haya.

“Sisi hapa tumejitokeza kuongoza mabadiliko ili yaje, lakini jambo la msingi kwenu ni kupiga kura ili mabadiliko hayo yaje.

“Msipopiga kura tukashinda, mtakuwa mmejiangamiza na msipopiga kura za uaminifu, mtaibiwa, CCM ikishinda mambo yatakuwa ni yale yale.

“Nawaambieni bila kura za kutosha tumeliwa na ili tushinde, mwambie hata rafiki yako aliyeko popote, iwe na Dare es Salaam au kwingineko nchini, kwamba Lowassa anataka kura yako.

“Kama mtanionyesha imani ya kutosha kwa kunipa kura za kutosha, nawaahidi utumishi uliotukuka kwa sababu imani huzaa imani” alisema Lowassa na kushangiliwa.

Pamoja na hayo, Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu, aliwataka pia Watanzania wasidanganywe na maneno ya baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania.

Alisema kwamba, katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu, yatatolewa maneno mengi yakiwamo yasiyokuwa na maana na kwamaba jambo la msingi ni wananchi kuwa na msimamo wa kuiondoa madarakani CCM.

Akizungumzia mazao ya alizeti, nyanya na vitunguu yanayolimwa mkoani Singida, alisema atakapoingia madarakani, atajenga viwanda vya kusindika mazao hayo badala ya utaratibu wa sasa ambapo mazao hayo yananunuliwa na Wakenya.

 

LISSU

Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema Lowassa ndiye kiongozi anayeifaa Tanzania kwa kuwa ana uwezo mkubwa kisiasa kuliko mwanasiasa yeyote nchini.

Pamoja na hayo, Lissu alitumia muda mwingi kuwaeleza wananchi jinsi Lowassa asivyohusika na kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Katika maelezo hayo aliyoyatoa katika mikutano ya Singida Kaskazini na Iramba Magharibi, Lissu alitumia kitabu cha ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyosomwa bungeni mwaka 2008 na aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe.

 

MSINDAI

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Singida ambaye pia ni mgombea ubunge katika Jimbo la Singida Mjini kupitia Chadema, Mgana Msindai, aliendelea kusema CCM haina tena sifa za kuongoza Tanzania kwa kuwa imepoteza mwelekeo.

Pamoja na hayo, alimshutumu aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), kwamba ameshindwa kuwasaidia ajira vijana wa jimbo hilo licha ya kuliongoza kwa miaka 15.

 

MGEJA

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema kitendo cha baadhi ya vigogo wa CCM kuhamia Ukawa ni dalili ya chama hicho kupoteza mwelekeo.

Alisema ni aibu kwa Watanzania kuendelea kukiunga mkono CCM wakati shida zimekuwa zikizidi kila mwaka ingawa nchi ina rasilimali za kutosha.

Sumaye: Hakuna wa kuifufua CCM

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema kwa sasa hakuna njia au mtu atakayeweza kuifufua CCM.

Sumaye alisema wamezunguka maeneo mengi ya nchi kila walipokuwa wakienda wamebaini Watanzania hivi sasa wanahitaji mabadiliko na hawana mpango wa kuongozwa tena na CCM.

Aidha Sumaye alipingana na wale wanaosema amejiunga  Ukawa kwa uchu wa madaraka, na kusema kuwa uchu wake wa kujiunga Ukawa ni kutaka kuing’oa CCM.

“Sikuja Ukawa kutafuta cheo kwa sababu nimeshakuwa waziri mkuu na hata hapa Ukawa hakuna nafasi ninayotaka kwa sababu nafasi ya urais yupo Lowassa na nafasi ya waziri mkuu siwezi kupata kwa sababu sijagombea ubunge ila ninachofanya ni kuhakikisha CCM inaondoka madarakani,” alisema.

Sumaye alisema kwa kuingia kwake Ukawa, amejikuta akipata vitisho kutoka serikalini ikimtishia kumny’anyang’anya mashamba yake, kitu anachokiona ni sawa na kumpiga chura teke.

“suala la kunitisha kuninyang’anya mashamba yangu ni kunikomaza zaidi kwa kuwa naamini suala hilo ni sawa na  kumpiga chura teka.” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles