NAIROBI, KENYA
MAJAJI wa Mahakama ya Juu leo wanatarajiwa kutoa uamuzi utakaoamua mwelekeo wa Kenya kuhusu uhalali wa uchaguzi wa Oktoba 26, ambao Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.
Majaji hao wako njia panda, ambapo kwa upande mmoja watahitaji kutekeleza sheria na pili kuzingatia hali ilivyo nchini hapa ili kuzuia isisambaratike.
Wakili Aulo Sowetto anayewakilisha wanaharakati wawili waliopinga uchaguzi wa Rais Kenyatta aliwataka majaji kuzingatia kuwa nchi hii inapaswa kuunganishwa na sheria na wala si Ilani ya vyama vya siasa au mawazo ya viongozi yanayoegemea upande mmoja.
“Nawakumbusha ninyi majaji mkienda faraghani kuamua kesi hii mkumbuke utangulizi wa uamuzi wa Septemba 1, 2017 kuwa nchi iliyo na fahari kamili ni ile inayotegemea mwongozo wa sheria na Mungu,” alisema Soweto.
Vile vile, majaji hao walikumbushwa wimbo wa taifa unaotambua Mungu kama nguvu ya Wakenya na haki iwe ngao na mlinzi.
Jaji Mkuu David Maraga, naibu wake Philomena Mwilu, Majaji Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola waliombwa wasishawishiwe wala kuyumbishwa na maelezo yaliyoonekana kama ya ukweli kuwa “uchaguzi ulikuwa halali ilhali ulikuwa kinyume”.
Majaji hao sita walipokea mawasilisho ya ushahidi kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Kilome, John Harun Mwau, wanaharakati wawili Njonjo Mue na Khelef Khalifa.
Majaji hao wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusu hoja za kisheria zilizowasilishwa na Mwau, Mue na Khelef katika uamuzi wao wa leo na ambazo ni msingi wa kesi hii:-
Hoja hizo ni pamoja na, “Iwapo sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa na Bunge Oktoba 2017 zinaweza kutumika kuamua kesi hii ya pili ya kumuondoa madarakani Rais Kenyatta.
Nyingine ni iwapo ghasia na vurugu zilizokumba maeneo mbalimbali ziliathiri uchaguzi wa rais mteule.
Nyingine; uhalali wa kikatiba wa kutofanyika uteuzi upya wa wagombea urais walioshiriki katika kinyang’anyiro kipya cha uchaguzi wa urais;
Iwapo kujiondoa kwa mgombea wa upinzani wa Nasa, Raila Odinga kunaathiri uhalali wa ushindi wa Kenyatta na athari za kutofanywa kwa uchaguzi katika maeneo ya uwakilishi bungeni kwenye kaunti nne;
Iwapo kutokuwa na imani kwa wapigakura na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kulichangia zaidi ya wapigakura milioni 10 kususa.
Athari za vitisho vya Rais Kenyatta kwa majaji wa mahakama kufuatia kutupiliwa mbali kwa ushindi wake wa Agosti 8,2017,
Ikiwa kutoshiriki kwa wapigakura hao milioni 10 kunatia dosari uhalali wa Serikali ya Jubilee na iwapo ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.
Washtakiwa katika kesi hii IEBC, mwenyekiti wake Wafula Chebukati na Kenyatta waliojaribu kutoa jawabu la maswali hayo mazito.