29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

HALMASHAURI UBUNGO YAFUNGUA OFISI MAPATO SIMU 2000

Na KOKU DAVID


HALMASHAURI ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, imejipanga kuhakikisha inakusanya kodi kutoka kwa wananchi wake ili iweze kuwaletea maendeleo mbalimbali.

Katika kuhakikisha malengo yanatimia, halmashauri hiyo kupitia kwa Meya wake, Boniface Jacob, ilizindua ofisi rasmi kwaajili ya ukusanyaji ushuru na mapato ambayo itakuwa ndani ya kituo cha mabasi ya daladala cha Simu 2000, maarufu kama Mawasiliano, mali ya Halmashauri hiyo.

Katika ofisi hiyo ambayo  iko katikati ya eneo la Halmashauri, wakazi wa halmashauri hiyo wataweza kupata huduma zote ambazo awali walikuwa wakizifuata katika ofisi kuu iliyopo Kibamba, ambayo iko pembezoni.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa ofisi hiyo, Meya  Boniface Jacob anasema lengo la uzinduzi wa ofisi hiyo katika eneo hilo ni kuwarahisishia na kuwasogezea huduma wakazi wa kata zilizopo maeneo jirani na kituo hicho.

Anasema uwepo wa ofisi hiyo maeneo hayo utawapunguzia muda wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika ofisi kuu iliyopo Kibamba.

Anasema wanatarajia ofisi hiyo kuhudumia watu 600,000 kwa mwezi, hali itakayoiwezesha Halmashauri kukusanya mapato ya kutosha kufanya maendeleo katika maeneo mbalimbali.

“Watumishi wa Halmashauri ya Ubungo naomba tujipange vizuri ili kuhakikisha tunawajibika ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuwa waadilifu katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Walipakodi ni watu muhimu sana, hivyo tunatakiwa tuwahudumie vizuri pindi wanapofika ofisini kulipa kodi, ikiwa ni pamoja na kuwafanyia maendeleo kutokana na kodi watakazokuwa wakilipa.

“Kila mwenye kulipa kodi ana haki ya kuhoji maendeleo, hivyo na sisi tunatakiwa kujipanga na kuwahudumia vizuri, lakini pia wakazi wa Halmashauri ya Ubungo mnatakiwa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya halmashauri yetu,” anasema Jacob.

Anasema watumishi ambao watakuwa si waaminifu wanatakiwa kutolewa taarifa zao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Anaongeza kuwa, inatakiwa kuhakikisha mianya yote ya upotevu wa mapato inazibwa, ili mapato stahiki yakusanywe ili halmashauri iweze kufikia malengo iliyojiwekea katika masuala ya maendeleo.

Anasema sambamba na wafanyabiashara, pia madereva wa bodaboda ni walipa kodi ambao wanatakiwa kusajiliwa ili wafanye bishara zao kihalali.

Jacob anasema kuwa, baada ya kuwasajili madereva wa bodaboda, inatakiwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia kazi zao kuepuka kusumbuliwa na askari, ili waweze kufaidika na kazi yao na kusisitiza  pia walipe kodi.

“Kama tutawasajili wafanyabiashara wa bodaboda na kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara na halafu tukajua idadi yao, naamini tunaweza kukusanya hadi Sh bilioni 4 kutoka kwa wafanyabiashara wa bodaboda,” anasema Jacob.

Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Ubungo, Fulgence Luyagaza, anasema kutokana na mwongozo wa serikali wa kutoa huduma bora na za karibu kwa wananchi, Halmashauri ya Ubungo imelazimika kuwasogezea huduma karibu wananchi wake.

Anasema kuwa, ofisi hiyo itakuwa ikitoa huduma kwa wafanyabiashara pamoja na watu wote wanaoishi maeneo jirani na ofisi hizo, zilizopo ndani ya Kituo cha Simu 2000 Ubungo.

Anasema katika kuhakikisha kodi ya serikali inafika serikalini, ukusanyaji wa mapato katika ofisi hiyo utakuwa ukitumia Mfumo wa Mapato wa Kielektroniki kwaajili ya kukusanya maduhuli yote ya serikali.

“Huduma zitakazotolewa katika ofisi hii ni kutoa leseni za biashara pamoja na ada zote za halmashauri ambazo zilikuwa zinafuatwa katika ofisi kuu Kibamba,” anasema Luyagaza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Mujuni Bikombo, anasema kutokana na hamasa ya watu kufika katika ofisi hiyo kwaajili ya kupata huduma, halmashauri inatakiwa kuboresha ofisi kwa kuipanua ili kuweza kuhudumia watu wengi.

“Baada ya uzinduzi ofisi itaanza kazi mara moja na kwamba tunatarajia upanuzi wa ofisi utasaidia kuondoa changamoto ya msongamano wa watu watakaokuwa wakifika ili kupata huduma,” anasema Bikombo.

Kwa upande wake Jackson Temu, ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Simu 2000, anasema pamoja na kusogezewa huduma za kiserikali katika eneo hilo la soko, mbiundominu ya kuweza kufika katika soko hilo inahitaji matengenezo ili kuwawezesha wafanyabiashara wengi kuongezeka.

Anasema soko la Simu 2000 linaweza kuiingizia serikali mapato mengi iwapo wafanyabiashara wote walioko barabarani watahamishiwa katika soko hilo.

“Tumetekeleza agizo la serikali la kufanya biashara katika maeneo rasmi, lakini pia serikali inatakiwa kuwakusanya na wale wenzetu ambao bado wamepanga bidhaa kama zetu katika maeneo ya barabarani ambao wanasababisha sisi tulioko huku ndani kutokufanya biashara kwa sababu wateja wanaishia huko huko hawatufikii sisi.

“Barabara ya kufika katika hili soko ni mbaya, imejaa mashimo na vumbi na mvua ikinyesha ndio inakuwa haipitiki vizuri, hali inayosababisha sisi hatufanyi biashara, lakini tunatakiwa kulipa kodi kama ambavyo sheria inatutaka kufanya,” anasema Temu.

Anasema suala la kulipa kodi ni la kizalendo, ambalo kila mfanyabiashara anatakiwa kulitekeleza, lakini inatakiwa kutengeneza mazingira mazuri ya kumwezesha mfanyabiashara aweze kufanya biashara na kulipa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles