TRA WAENDESHA OPERESHENI ENDELEVU KUVAMIA VITUO VYA MAFUTA

0
499

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAMKATIKA kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi kwa mujibu wa sheria, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali ili kuweza kukusanya kodi kutoka kwa kila mwenye mapato.

Mamlaka hii imeziba mianya mbalimbali ya upotevu wa mapato katika bandari, mipakani, ikiwa ni pamoja na kufanya operesheni katika bandari bubu ili kukamata wafanyabiashara za magendo kwa lengo la kukwepa kodi.

Hiyo ni baadhi ya mikakati iliyowekwa ili kuweza kupunguza wakwepa kodi, lakini pia kuongeza mianya ya ukusanyaji kodi.

Sambamba na hayo, hivi karibuni mamlaka hii imeanzisha operesheni ya kuvamia vituo vya mafuta ili kukamata wasiotoa stakabadhi baada ya kutoa huduma kwa wateja wao.

Operesheni hii, ambayo itakuwa endelevu, itakuwa ikifanyika nchi nzima, lengo likiwa ni kukamata wakwepa kodi.
Hivi karibuni katika operesheni ya kukamata wafanyabiashara wa vituo vya mafuta ambao wanakwepa kodi jijini Dar es Salaam, kati ya vituo vitatu ilivyotembelewa, Mamlaka hiyo ilivikamata vituo viwili na kuvitoza faini ya Sh milioni 4.5 kila kimoja.

Vituo vilivyovamiwa katika operesheni hiyo ni Victoria, Oil Com Kijitonyama pamoja na Oil Com Makumbusho, ambacho hakikutozwa faini kutokana na kuwa kilikutwa kikitekeleza sheria ya kutoa stakabadhi.

Katika operesheni hiyo, TRA ilishuhudia wafanyabiashara hao wa vituo vya mafuta wakiwahudumia wateja bila kuwapa stakabadhi, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mbali ya wateja, pia gari la ofisa wa TRA ambaye alikuwa katika operesheni hiyo alihudumiwa katika moja ya vituo hivyo lakini hakupewa stakabadhi, hali iliyodhihirisha kuwa uvunjaji wa sheria katika vituo vya mafuta ni mkubwa.

Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Diana Masala, anasema kati ya vituo vitatu walivyovamia, viwili vilikutwa na makosa ya kutokutoa stakabadhi na kwamba kila kimoja wamekitoza faini kama sheria inavyosema.

Anasema zoezi hilo litakuwa endelevu na litakuwa likifanyika nchi nzima, ili kukamata wafanyabiashara wanaokiuka sheria ya kutoa stakabadhi pamoja na wateja ambao hawadai stakabadhi.

Anasema sambamba na kukamata wasiotoa stakabadhi, pia watakuwa wakikagua vituo vya mafuta ambavyo havijafunga mashine za kodi za kielektroniki (EFDs) kwenye pampu za mafuta.

Anasema pia watakuwa wakikagua wafanyabiashara wasiokuwa na mashine hizo, ikiwa ni pamoja na wale wasiotoa stakabadhi baada ya kutoa huduma kwa wateja wao.

Diana anaongeza kuwa, sheria haitawashughulikia wafanyabiashara pekee na kwamba hata mtu atakayeweka mafuta kwenye gari lake na kuondoka bila kudai stakabadhi pia atatozwa faini kama sheria inavyosema.

Anasema faini kwa mtu asiyedai stakabadhi baada ya kuhudumiwa inaanzia Sh 30,000 hadi Sh milioni 1.5.
Anasema wafanyabiashara wa vituo vya mafuta waliiomba Mamlaka ya Mapato kuwaruhusu kuendelea kutumia mashine za EFDs za kawaida na si zile zilizounganishwa moja kwa moja kwenye pampu kutokana na kuwa gharama zake ni kubwa.

Anasema TRA ilikubali ombi la wafanyabiashara hao, lakini wamekuwa si waaminifu na badala yake wanakwepa kodi kwa makusudi, huku wakijua kuwa kufanya hivyo wanavunja sheria.

Diana anasema ili kuepuka kuchukuliwa hatua kali, TRA inawataka kuacha mara moja tabia ya kukwepa kodi na kwamba iwapo wataendelea kukaidi, mamlaka itawafungia biashara zao kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na uvamizi katika vituo vya mafuta, pia walivamia katika Baa ya Hongera iliyopo Sinza, Africa Sana na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na kuwatoza faini ya Sh milioni 4.5.

Baada ya operesheni ya kuvamia vituo vya mafuta, maofisa hao wa TRA ambao walifika katika eneo hilo kwaajili ya kupata huduma ya chakula, walifanya ukaguzi na kubaini kuwa baa hiyo inatoa huduma bila kutoa stakabadhi, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here