Na Hadija Omary, Lindi
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Nje, Donald Maliki ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Lindi,mkoani Lindi kuzifanyia kazi hoja 36 za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za miaka sita iliyopita.
Hoja hizo za mwaka 2009/16 hadi sasa utekelezaji wake haujakamilika.
Maliki alitoa agizo hilo juzi wakati wa kikao maalum cha baraza la Madiwani.
Kikao hicho kilijadili na kujibu hoja mbalimbali zilizomo kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17.
Akisoma ripoti ya CAG kwenye kikao hicho kilichohudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi,Godfrey Zambi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi,Madiwani na wakuu wa idara, Maliki alisema licha ya halmashauri hiyo ya wilaya kutekeleza ipasavyo hoja za miaka ya nyuma, bado kuna hoja 36 hazijajibiwa.
Alisema anaamini hoja hizo zinafanyiwa kazi, lakini ipo hoja moja ya mwaka 2009/10 haikujibiwa.
Mwaka 2011/12 hoja mbili hazikujibiwa na 2012/13 hoja moja haikujibiwa.
Mwaka 2013/14 hoja tatu hazikupata majibu, 2014/15 hoja saba hazikujibiwa na 2015/16 hoja 22 nazo hazijajibiwa hadi sasa.
Hata hivyo Maliki alisema mwenendo wa hati za ukaguzi katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kwa Halmashauri hiyo umekuwa mzuri.
Alisema mwaka 2012/13 2013/14, 2014/15, 2015/16 na 2016/17 Halmashauri hiyo ilipata hati zinazoridhisha
Alibainisha kuwa matokeo hayo yametokana na ukaguzi wa kumbukumbu za hesabu, tathimini ya shughuli za Halmashauri na tathimini ya mfumo wa udhibiti wa ndani unahitaji umakini zaidi.
Hata hivyo Maliki aliwaasa viongozi hao kujibu hoja kwani utoaji wa hati inayoridhisha hauna maana kuwa taasisi husika ina asilimia 100 ya ufanisi katika mfumo wake wa udhibiti wa ndani.