31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yadhibitisha dhamira yake ya kuendeleza wahandisi wanawake

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMPUNI ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited (GGML), imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya nchi kwa kuwawezesha kuimudu vema fani ya uhandisi.

Hayo yamebainishwa juzi na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akizungumza katika Kongamano la nane la wahandisi wanawake (TAWECE) lililofanyika mkoa wa Mjini Magharibi Visiwani Zanzibar.

Alisema GGML inatambua na kuthamini umuhimu wa wanawake katika fani ya uhandisi hasa kwa kuzingatia ni wabunifu wa kipekee pindi wanapokabidhiwa jukumu ndio maana haikusita kudhamini kongamano hilo lililoshirikisha wanawake wahandisi zaidi ya 800.

Alisema GGML imejikita kwenye utofauti, usawa na ujumuishaji (DE & I), ambayo ndio kiini cha mkakati wa kampuni hiyo kwenye usimamizi wa wafanyakazi wake.

“Tunaamini uwepo wa wahandisi wanawake unaongeza uwezo wa kampuni yetu, na tumeendelea kuweka mazingira ya kuheshimu tofauti na kuruhusu wafanyakazi wote kufikia uwezo wao bila kujali jinsia wala historia yao,” alisema Shayo.

Alisema GGML iliunga mkono kikamilifu mipango ambayo iliwahimiza wanawake kusoma taaluma ya uhandisi kwa kutoa ufadhili wa masomo, ushauri na mafunzo ya kazi ili kuondokana na dhana potofu za kijinsia na kuunda fursa sawa kwa wote.

“Kampuni ilifanya kazi ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika sekta ya madini na kuchangia pakubwa katika juhudi za maendeleo, hasa katika elimu. Iliwekeza katika miradi iliyokuza elimu ya sayansi kwa wasichana, na kuwawezesha kushiriki kikamilifu na kufikia malengo yao katika nyanja za sayansi na uhandisi,” alisema Shayo.

Aidha, akifungua kongamano hilo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema, Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinatambua na kuthamini mchango wa wahandisi wanawake nchini kutokana na kazi za uhandisi wanazozifanya.

Alisema makongamano kama hayo yamekuwa na mchango mkubwa wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza ubunifu wa sanyansi na kuleta chachu ya maendeleo ya Taifa ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Alisema, fani ya uhandisi ina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa nchi pia ni uti wa mgongo wa shughuli nyingi za kiuchumi. Hivyo aliwataka vijana na wanawake kuzitumia fursa ziliopo ili kuyafikia malengo yao.

Pia, aliwashauri wahandisi wanawake kufungua kampuni na kujiajiri kupitia ukandarasi na uhandisi nakueleza hatua hiyo itachangia sana maendeleo ya nchi kwa kujenga miundombinu imara itakayodumu kwa muda uliokusudiwa.

Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Mhandisi Gemma Modu alisema takwimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake katika uhandisi bado ni mdogo ikilinganishwa na wanaume.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo akizungumza katika kongamano hilo.

Aliisihi jamii kuachana na mitazamo potofu juu ya wahandisi wanawake kwa kuangalia mapungufu yao yanayotokana maumbile ya jinsia zao zikiwemo uzazi na uhalisia wao, na kuwataka waajiri kuona umuhimu wao na kutambua mchango wao kwa maendeleo ya taifa kwa kuwatumia kwenye kazi za vitendo badala ya kuwapa kazi za ofisini pekee.

Uzinduzi wa Kongamano la nane la wanahandisi wanawake Tanzania kwa mwaka huu, 2023 ulikwenda sambamba kaulimbiu isemayo “Nguvu ya Ushirikishwaji na Uhusishwaji wa Wanawake katika kazi za Kihandisi”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles