Na SHERMARX NGAHEMERA
TANZANIA imebarikiwa kuwa na madini mengi na mojawapo ni ugunduzi wa gesi ya helium, uliofanyika mwaka jana mkoani Rukwa, yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 15 na Kampuni ya Helium kutoka Norway.
Ugunduzi huo unaifanya Tanzania iwe na hazina kubwa ya rasilimali hiyo ya kimkakati katika medani ya viwanda, teknolojia na kijeshi, kutokana na matumizi yake mujarab.
Neema hiyo ya wazi imeanza kuleta sintofahamu kati ya Wizara ya Nishati na Madini na Shirika lake la usimamizi wa maendeleo ya petroli (TPDC) na kumfanya waziri mhusika kugomba hadharani juu ya mwenendo wa shirika hilo katika kushughulikia neema hiyo.
Aling’aka katika ulegevu ilionao kwenye kushughulikia kazi zake za mafuta ya petroli na gesi na hivyo kuchelea kuona linataka kuuendeleza ugoigoi katika mwenendo wa kushughulikia gesi ya helium.
Kiini cha matatizo ni undumilakuwili uliooneshwa na TPDC kutaka kumnyang’anya tonge mdomoni mvumbuzi wa gesi hiyo, Helium One ya Norway na kuipa kampuni ya Heritage Oil ya Uingereza, ambayo nayo inatafuta mafuta katika Bonde la Ufa mkoani Mbeya na Ziwa Nyasa.
Waziri Prof Sospeter Muhongo aliona mawazo hayo ya TPDC si sahihi na kusisitiza Helium One iendelee na shughuli na kuikoromea TPDC iachane na shughuli za Helium ili kufuta utata wake kwenye jambo hilo.
Prof Muhongo alisema kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi kuwa TPDC haina uwezo kimkakati na kirasilimali kushughulikia helium na bora iachane nayo bila kuifikiria.
Alisema kuwa, Serikali ina mpango kabambe wa kuanzisha shirika lake nje ya TPDC litakaloshughulikia na helium, kwani TPDC halina uwezo na dira ya kushughulikia rasilimali hiyo ambayo mtazamo wake ni wa kisasa na wenye ushindani mkubwa.
Alisisitiza umuhimu wa rasilimali hiyo kushughulikiwa vizuri ili kuleta matarajio yenye tija katika uchumi wa Taifa unaoelekezwa kwenye viwanda.
Waziri Muhongo ana imani kubwa na uwezo wa gesi hiyo kubadili hali ya uchumi wa nchi na kuwa chanya kwa kusisimua ukuaji wa uchumi kwa kuchagiza ujenzi wa viwanda uhusianavyo na vile vya sekta nyingine.
Muhongo alisema upungufu wa gesi hiyo duniani unaifanya iwe na umuhimu pekee, kwani hazina iliyoko Tanzania kwenye Bonde la Ufa pekee ni mara mbili ya ile iliyopo Marekani na hivyo kuipa nchi hii umuhimu pekee duniani kirasilimali.
Rekodi zinaonesha kuwa, Tanzania katika sehemu moja tu ina hazina ya helium ya kiasi cha futi za ujazo bilioni 54 (bcf), ni mara saba ya uhitaji wa soko la dunia kwa sasa. Imeipita Marekani yenye hazina ya futi za ujazo bilioni 24.2.
Hivyo basi, Tanzania inategemewa ulimwenguni kuziba pengo la upungufu wa helium iliyopo kwa sasa, kwani gesi hiyo ikitumika huwezi kuirudishia tena, yaani si jadidifu.
Matumizi na mahitaji yake yameongezeka katika teknolojia mbalimbali za kimkakati.
Helium One inaamini kuwapo nchini kwa hifadhi ya rasilimali hiyo zaidi ya futi za ujazo bilioni 180 za gesi ya helium nchini.
Kuleta mabadiliko
Kuwapo kwa gesi hii kunafungua fursa lukuki za uchumi na kuifanya helium kuwa nguzo muhimu katika ujenzi wa uchumi huo, kwani hata Rais John Magufuli amezungumzia kwa tambo na bashasha juu yake.
Alisema wakati alipoonana na waandishi wa habari pale Ikulu kufanya tathmini ya kazi yake katika mwaka wake mmoja madarakani kuwa helium ni madini mkakati kwa serikali yake.
Alitoa wasifu wa utajiri wa madini wa Tanzania ni pamoja na kuwapo madini ya gesi ya helium na kuipamba kwa sifa zake zote.
Dk. Magufuli alisema umasikini wa Tanzania ni ule wa kugeuza rasilimali zake ziwe fedha na kuwafaa wananchi wake na si kukosa hazina ya rasilimali amali.
Lakini wachumi wanasema kuwa rasilimali tu haifai na haitoshi kwa maendeleo ya nchi. Wanadai kuwa, kukosa utaalamu au rasilimali watu na mitaji ndio umasikini wenyewe na hivyo kama nchi tunahitaji kufanya ya ziada kupata ujuzi kwa kusomesha watu wetu ili wamudu kuongeza thamani ya kila kitu na kuleta utajiri wa kweli nchini.
Taifa likiwa na rasilimali watu wenye utaalamu mbalimbali huwa ni tajiri hata likikosa rasilimali za hazina na mifano iko mingi, ikiwamo Uingereza, Japan, Singapore, Denmark na Uswisi.
“Tanzania ina madini kedekede na mengine yanapatikana hapa tu, ikiwamo tanzanite na Mereranilite, hilo la pili ni madini mapya yaliyogunduliwa na watafiti wa Chuo cha Michigan cha Marekani mwaka jana,” alisema.
Katika hafla hiyo kwa mara ya kwanza kabisa kiongozi wa juu Tanzania, Rais Magufuli, alisema kuwa nchi inayo hazina ya mafuta ya petroli kwenye Ziwa Tanganyika na hivyo kuvunja mwiko wa kusema hakuna petroli nchini. Inasemekana mwiko huu aliuweka Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, akiogopa watu wataacha kufanya kazi wakijua kama kuna mafuta nchini.
Mafuta hayo ya ziwani yatachimbwa na Kampuni ya Kifaransa ya Total katika upande wa Magharibi wa Ziwa Tanganyika, upande wa DR Kongo na Tanzania kupata mgawo wake kama sheria za kimataifa zinavyodai katika mazingira kama hayo ya ziwa.
Rais Magufuli alijinasibu kuwa lile bomba la Uganda litatumika vilevile kusafirishia mafuta yatakayochimbwa katika Ziwa Tanganyika na hivyo kuwa na mzigo wa kutosha.
Bomba la kusafirisha mafuta ghafi ya Uganda limekuja wakati muafaka. Alipokuja Rais Joseph Kabila nchini jambo hilo lilizungumzwa na kukubalika na marais hao wawili.
Nchi iliyobarikiwa
Rais Magufuli alisema ugunduzi wa helium unathibitisha kubarikiwa kwa nchi hii, kwani ni madini ambayo yanategemewa kuongeza pato la nchi kwa kuwa yanahitajika sana kwa tafiti na matumizi ya vifaa vya teknolojia ya hali ya juu, kwani sifa yake kubwa ni wepesi wake na kutochangamana na gesi nyingine, yaani ni ‘inert gas’ na hivyo ni muhimu sana kwa shughuli na uchumi za kileo na hivyo kuwa na uhakika wa soko lisilo na ushindani mkubwa.
Helium One awali ilisema kuwa gesi hiyo itaanza kuchimbwa kibiashara ndani ya miaka mitano kutokana na taarifa yao waliyotoa kule New York, Marekani.
Kampuni hiyo inamilikiwa na Norway na hivyo kuleta mahitaji mahsusi ya ukaribu kati ya nchi hizo mbili za Norway na Tanzania. Ikumbukwe kuwa, hata kwenye gesi asilia kampuni ya Norway, Statoil ndiyo yenye gesi nyingi na vinara wa shughuli hiyo nchini na wahusika wakuu wa ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi kule Lindi (LNG Plant ) kupitia Kampuni hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Helium One, Thomas Abraham-James, amesema hapo awali akiwa New York kuwa kama mambo yakienda sawa, wataanza uzalishaji mwaka 2020, lakini haizidi 2021 na vilevile itategemea na utashi wa Serikali ya Tanzania ambaye ni mwenye rasilimali hiyo.
Abraham-James anasema mwaka ujao wataendelea na uchimbaji wa visima vingine vya gesi ili kujihakikishia ukubwa wa hazina hiyo na vilevile kuendelea na zoezi la kutafuta mitaji ya kufanyia shughuli yenyewe. Kitendo cha TPDC kinaonekana kuvunja imani hiyo.
“Helium One inatafuta dola milioni 40 kuendelea na kazi,” alisema Ofisa Mkuu Mtendaji huyo na kuongeza: “Kauli ya Serikali kuhusu uwekezaji ndio muhimu kufanyika haraka mradi huu”.
Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Maji na Umeme (Ewura) inahusika na sekta ya gesi na imeshatayarisha randamu za uwekezaji kwa sekta zilizo chini yake, lakini suala hili la helium halimo.
Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo, alithibitisha kuwa sheria inataka kila mgodi unaoanzishwa serikali lazima iwe na hisa zake zaidi ya zile za asili za (10 % carryover rights) ili kunufaika na rasilimali zake.
Matumizi
Helium hutumika katika teknolojia ya kutengeneza vifaa vya maabara, roketi, mitambo ya kinyuklia, vifaa vya elektroniki vingi na vinavyotumika katika maisha ya kila siku kama mashine za kudurufu na zile za afya za CT –Scan.
Julai mwaka jana, wanasayansi kutoka vyuo vikuu vya Oxford na Durham nchini Uingereza wakishirikiana na Helium One walithibitisha kuwapo kwa hifadhi kubwa zaidi ya helium katika Ziwa Rukwa.
Mkurugenzi wa Helium One, Thomas James, anasema kulikuwa na uhaba wa helium duniani kuanzia 2011 hadi 2013 iliyosababisha kupanda kwa bei katika soko la dunia na tangu hapo imekuwa ngumu kuipata, na hii itakuwa fursa kwa Tanzania uzalishaji wake utakapoanza.
Mwanafizikia William Ramsay, kutoka nchini Uingereza, aligundua gesi hiyo Machi 27, 1895, lakini kwa Tanzania, historia ya helium ilianza tangu mwishoni mwa miaka ya 1950, vipimo vya wakati huo vilionesha dalili za kuwapo kwa helium katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na tafiti za uchimbaji wa awali wa mafuta miaka ya 1980, maeneo mengi yalionyesha kuwapo kwa helium na lilithibitishwa na washauri kutoka Marekani, kwa maelezo ya James.
Helium katika maeneo mengi ulimwenguni inapatikana sehemu za miamba iliyopo ardhini, lakini Tanzania iko kwenye bonde la ufa na hivyo kuwa mradi rafiki wa mazingira.
Helium One iliwahi kutafuta gesi hii katika nchi za jirani zilizo kwenye bonde la ufa kama Malawi, Uganda, Zambia na Kenya, lakini nchi hizo hazikuwa na mazingira ya kuwapo kwa helium kwa wingi kama Tanzania.
Uhaba wa helium soko la dunia
Kutokana na upungufu uliotokea miaka ya hivi ya karibuni, dunia ilikumbwa na uhaba wa helium, tangu hapo upatikanaji wake umekuwa ukiyumbayumba na bei yake inaendelea kupanda.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, Chris Ballentine, ambaye alihusika katika utafiti huo, alisema
helium iliyopo Tanzania inaweza kuziba pengo katika soko la dunia kwa kiasi kikubwa, alikadiria kuwa hifadhi zilizogundulika zinaweza kutumika kwa miaka 15 hadi 20.
Ballentine anasema kuwa, ongezeko la utumiaji wa vifaa vya tiba, roketi, hifadhi za helium duniani zinapungua na kuirejesha ni ngumu.
“Tatizo la helium ni nyepesi mno, na gesi yake haiwezi kutumika mara mbili, helium kuwa inapotea hewani, lakini kugundulika kwake kutaleta mabadiliko ya uchumi kwa kizazi kijacho na kwenye mahitaji ya helium,” alisema.
Anasema kwa kufanya hivyo, tutaifikia helium na kuibadilisha kuwa hifadhi na hapo tunaweza kutathmini mapato na uzalishaji yatakavyokuwa.
Uzalishaji wa helium
Mkurugenzi wa Helium One Tanzania, Thomas James, kwenye mahojiano yake na Tanzania Invest, alisema kampuni hiyo itakuwa inamalizia uchimbaji mwishoni mwa mwaka huu na inatarajia kuwa na hifadhi za helium.
Na mradi wa Rukwa kuanzia sasa hadi mwishoni mwa 2017 zitahitajika kiasi cha dola za Kimarekani milioni 40 kwa ajili ya uchimbaji.
James alisema kuwa wanaendelea na mchakato wa kutafuta mtaji kutoka kwa wawekezaji binafsi (private equity), mtaji huo utatumika katika kukusanya taarifa za uchimbaji na utafiti chini ya ardhi.
“Kufikia Aprili mwaka huu tunatarajia kuanza uchimbaji katika awamu ya tatu au nne, tunaamini tutakuwa na hifadhi. Tutapata maamuzi ya mwisho ya kuingia uwekezaji na uzalishaji, lakini tupo tayari kwa wawekezaji”.
James anasema kianzio cha uzalishaji ni takribani futi za ujazo bilioni 10, ambayo inaweza kutoa thamani ya matumizi ya mtaji na pia inahitaji eneo na kiwanda kikubwa cha uzalishaji helium.
Uhitaji wa dunia
Kwa sasa ulimwengu mzima hutumia futi za ujazo bilioni sita kila mwaka na soko haraka linaongezeka ukilinganisha mafuta na gesi asilia.
Kampuni ya Helium One Tanzania iliandika kwenye tovuti yake kuwa soko la dunia la helium linatarajiwa kufikia zaidi ya dola bilioni 6 mwaka huu na thamani yake imeongezeka kwa asilimia 100 kipindi cha miaka 10 iliyopita.
"Katika suala helium ya Tanzania kuongoza soko la dunia, lakini hii mpaka vyanzo vya helium vibadilishwe kuwa hifadhi na uzalishaji unaweza kuanza. Na itawawezesha watumiaji kupanga na kuwekeza katika helium," Ballentine alisema.
Marekani inaongoza, ambayo huzalisha asilimia 75 ya helium yote ulimwenguni, ikifuatia Algeria, Urusi, Qatar na Poland.