26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

MAUZO MAKUBWA YA HISA YADODA DSE

Na MWANDISHI WETU


KAMA ilivyohofiwa na wengi, uuzaji wa hisa mpya mwaka huu umeanza kwa kishindo, lakini zimeishia na mafanikio duni kutokana na sababu mbalimbali.

Kuna madai kuwa, baada ya kufungwa mnada wa awali (IPO) wa Kampuni ya Vodacom na ule wa TCCIA –Investments, umeonesha kufanya historia katika mambo makubwa mawili; ya kuwa na toleo kubwa kupita yote katika historia ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na kupata  mauzo  kiduchu chini ya asilimia 50 na kuwa wa wastani mdogo zaidi katika historia ya soko hilo  na hivyo kuleta maswali mengi kuliko majibu; na kubwa ni kulikoni sokoni? Ni wazi kuwa utahitajika muda zaidi kuuza hisa hizo zinazoshabikiwa na wengi.

Sababu za kudoda ni nyingi, lakini moja iliyopata kipaumbele na kuonekana kuna ukweli ndani yake ni kuwa mdomo wa soko la DSE ni mdogo sana na hivyo kushindwa kummeza samaki mkubwa katika umbo la Vodacom Tanzania na kudai kuwa toleo hilo lingetolewa kuwa la Afrika Mashariki (EAC) na SADC, ambazo kwa mwendelezo ni sehemu ya uchumi wa Tanzania kimuundo kama livyokuwa kwa kampuni ya Safaricom ya Kenya, iliyotumia EAC kama nyumbani kwao na kufanikiwa.

Madalali wa soko walitegemea hivyo na kuungana na wenzao wa EAC na SADC na hivyo ilikuwa pigo kubwa kwao ilipofanywa kuwa ya Watanzania pekee.

Cha kushangaza ni kuwa, Vodafone ambayo ni kampuni mama yenye uzoefu kutoka Safaricom ya Kenya imeshindwa kutumia uzoefu  huo mkubwa katika eneo hili uliomwezesha kuuza hisa zake na fedha kusaza (oversubscribed). Vodafone ya Uingereza ni mmiliki wa Kampuni zote hizi mbili na hivyo  kuacha  watu midomo wazi.

Sababu nyingine ni kuwa, Vodacom na wote waliohusika walifanya kosa la nyakati, kuwa robo ya kwanza ya mwaka sio vizuri kufanya toleo la hisa, tena kubwa kama hilo, kwani wawekezaji wote wakubwa (corporate investors) wengi hukabiliwa na malipo mengi ya kufanya, ikiwamo malipo ya kodi ya mapato, pango na gawiwo kwa  wawekezaji wake na hivyo ingekuwa vizuri zoezi lingefanyika kuanzia katikati ya Aprili, tarehe ambayo ndiyo iliyofunga mauzo  yake.

Ukweli huo unaungwa mkono na Charles Shirima, ambaye ni Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Soko la Hisa na Mitaji (CMSA) ambaye anadai kwa uzoefu wake, miezi ya Septemba hadi Machi ina majukumu mengi kipesa na hivyo hutoa matokeo yasiyoridhisha kwa IPO.

Jamii ya Watanzania haikushituka pale kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC, ilipotangaza kuongeza muda wa uuzaji wa hisa zake hadi Mei 11, baada ya kuruhusiwa na CMSA kuongeza muda huo.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania PLC, Rosalynn Mworia, alisema hatua hiyo inatokana na kupokea maombi mengi ya kutaka kununua hisa za kampuni hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema kuongezeka kwa muda wa mwisho wa kununua hisa kutawezesha wanaohitaji kununua hisa kwa makundi binafsi na taasisi zilizoomba muda uongezwe kushiriki kikamilifu katika mchakato huo.

“Vodacom inatoa shukrani kwa Watanzania ambao wamejitokeza kuwekeza kupitia kununua hisa na kuwakaribisha ambao bado hawajanunua kuchangamkia fursa hiyo katika muda huo wa nyongeza,” alisema Rosalyn.

“Mgawanyo na mchanganuo wa umiliki wa hisa inapendekezwa utafanyika kuanzia Mei 19, mwaka huu na kuendelea, kabla ya kumaliza mchakato wa mwisho wa kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam katika tarehe iliyopangwa ya Juni 6, mwaka huu,” alisema.

Kosa lingine ni lile la kiufundi ambapo  IPO hizo zilikosa kuwa na ‘underwriters’ ambao hudhamini  na hutumika kama  dodoki  kwa kununua hisa zote zinazobakia bila kuuzwa  na hivyo kuleta shaka tokea mwanzo na kama ilivyotokea kwa TCCIA-I ambao wanataka muda uongezwe, kwani watakamilisha mazungumzo na ‘underwriters’ katika kipindi hiki cha Aprili hadi Mei.

Hali hiyo imethibitishwa na Bonaventure, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Securities, ambaye anadai mauzo hayo yamebinywa na mwingiliano wa kisheria na kitaasisi, kwani ni sheria ya Bunge ilitumika na si kanuni za soko na hivyo kufanya wahusika kwenda shoti kutekeleza mahitaji ya sheria kuliko hali halisi.

Kosa kubwa lililo fanywa  na TCCIA –I  ni kuuza hisa zake  wakati mmoja na al-maarufu Vodacom na hivyo kupata kipigo cha mwaka, kwani katika mauzo yake ya hisa za thamani ya Sh bilioni 45, imepata Sh bilioni moja tu na hivyo kuanguka vibaya, kwani hiki ni kiasi kidogo sana cha makusanyo katika historia ya soko hilo cha asilimia  2.2 tu.

Sababu nyingine ni kwa serikali kukosa mkakati wa kuwekeza, kwani ingeweza kununua hisa, halafu ingekuja ziuza kwa faida baadaye na hivyo kusaidia wale walio na mahitaji hapo baadaye katika kile kinachoonekana kuwa  ni ‘mopping.’

Wajuzi wa mambo wanadai matokeo hayo hasi yamethibitisha bila shaka kile ambacho awali kilisemwa katika utafiti binafsi ambapo matokeo yake kiasi kikubwa yalilingana na matokeo haya ya mauzo na kuwaacha magwiji wa soko, Raphael Masumbuko wa Zan Securities na Bonaventure wa Tanzania Securities hoi.

Uchunguzi wa Insight Twitter ulionesha kuwa, walioamini soko litafanya vizuri ni asilimia 19, waliokuwa na wasiwasi ni asilimia 31 na wale walioona kwamba mambo yatakuwa mabaya ni asilimia 44 na wasio maono  ni asilimia 6 ya wapiga kura.

Wengi wa wapiga kura hao walifanya  hivyo wakidai kuwa hali ya uchumi imesinyaa na shughuli za uchumi haziendi vilivyo na hivyo ingekuwa muujiza kuuza sana.

Wiki iliyopita Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilionya mwenendo wa uchumi kuwa hauridhishi na serikali ifanye juhudi ya kuongeza upatikanaji wa fedha katika uchumi kwa kulipa madeni inayodaiwa na sekta mbalimbali na haswa madeni ya ndani.

Hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania ziliuzwa mwezi uliopita katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa ni kampuni ya kwanza ya simu za mkononi kutekeleza na kukubaliwa kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma, ikiwa na lengo la kupata shilingi bilioni 476.

Hisa hizo, ambazo jumla yake ni milioni 560, ziliuzwa kwa   shilingi 850 kwa hisa moja, ikiwa kampuni ya kwanza kwa ukubwa wa toleo la mauzo ya awali (IPO) nchini katika soko la msingi (primary).

Soko la upili (secondary market) litaanza mwezi Mei mwaka huu kama mambo yataenda sawa.

Profesa Honest Ngowi, ambaye ni mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, awali  alionesha wasiwasi wa kufanya vizuri na kuweza kukusanya kiasi cha mtaji wanaolenga.

“Haya makampuni ya simu yanaingia katika soko la hisa kutokana na msukumo wa serikali. Lengo ni kukusanya mtaji kutoka kwa umma na kinachokuja hapa ni kuwa yanaingia kwa kufuatana, yakilenga kukusanya mitaji kutoka kwa wateja wachache waliopo sokoni,” anaeleza Prof Ngowi, wakati kwa wananchi wengi ni wakati mgumu kiuchumi. Na ndicho kilichotokea.

Mchumi huyo nguli alifafanua kuwa, wateja ni wachache na wale wa siku zote na wengi ni mifuko ya hifadhi ya jamii.

Prof Ngowi aliongeza kuwa, hali ya kifedha kwa makampuni na hata watu binafsi ambao ni wateja walengwa wa hisa hizo siyo nzuri.

 Kwa kufananisha mafanikio, makampuni ya awali kama CRDB,NMB, Twiga Cement  na mengineyo yaliingia katika kipindi kizuri cha mahitaji ya uwekezaji na pili yaliingia moja baada ya jingine na kwa nafasi na sio kwa mkupuo na hivyo kuweka historia za kupata na kusaza mahitaji (oversubscription).

 Wakati huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Moremi Marwa, alisema hawezi kuzungumza chochote, kwa kuwa ni suala la kubashiri na hivyo si shani kwa yeye na nafasi yake akinukuliwa. 

 Marwa alisema kujiorodhesha kwa makampuni mapya ya simu DSE kutasaidia kuongeza wawekezaji kwenye soko hilo, ambalo kwa sasa lina wawekezaji 500,000 kupitia kampuni 25 ambazo zimejiorodhesha, zenye mtaji wa jumla ya Sh trilioni 21 tu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles