
MANCHESTER, ENGLAND
NYOTA wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Steven Gerrard, amemtaka nahodha wa timu hiyo, Wayne Rooney, kuendelea kucheza nafasi ya kiungo badala ya ushambuliaji.
Gerrard amedai kwamba mchezaji huyo amekuwa na uwezo mkubwa wa kuubadilisha mchezo wakati akipewa nafasi ya kuwa kiungo japokuwa pia anafaa katika safu ya ushambuliaji.
Rooney alianza kubadilishwa namba na kocha wake, Van Gaal kwenye klabu ya Manchester United, hivyo hali hiyo ikamfanya kocha wa taifa, Roy Hodgson, kumchezesha namba za katikati.
“Si jambo rahisi mchezaji ambaye amezoea kucheza nafasi ya ushambuliaji na baadaye kuja kuwa kiungo namba nane au tisa, si wachezaji wote wanaweza kufanya hivyo.
“Rooney alikuwa mshambuliaji mzuri lakini kwa sasa anakuja kuwa mtengenezaji mzuri, ninaamini anaweza kutokana na kile ambacho anakifanya tangu akiwa Manchester na kwenye michuano ya Euro 2016, anastahili sifa.
“Ni bora aendelee na hali hiyo kwa ajili ya kuongeza msaada katika safu ya kiungo kwa kuwa washambuliaji bado wapo wengi na wana uwezo mkubwa, hivyo ni vizuri kuendelea na nafasi hiyo ya sasa,” alisema Gerrard.
Gerrard alikuwa kiungo kwa kipindi chake akiwa timu ya Taifa ya England pamoja na klabu yake ya Liverpool na sasa anakipiga klabu ya LA Galaxy ambayo inashiriki ligi nchini Marekani.