23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

GEREZA LA MAHABUSU MOROGORO LAPATA MAJI

Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO

WAFUNGWA na familia za askari wanaoishi katika Kambi ya Gereza la Mahabusu, Wilaya ya Morogoro, wameondokana na changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu, baada ya kupata kisima kirefu cha maji.

Hayo yalielezwa juzi na Mkuu wa Magereza, Mkoa wa Morogoro, Ramadhani Nyamka, alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa mradi huo wa kisima kirefu uliofadhiliwa na Taasisi ya Islamic Foundation.

Kwa mujibu wa Nyamka, mradi huo ni mkombozi kwa mahabusu na familia za askari, kwa kuwa watakuwa wakipata maji bila shida, tofauti na ilivyokuwa kwa siku zilizopita.

“Kero ya maji katika gereza hili imekuwa ni ya muda mrefu na ilikuwa ikitishia afya za wafungwa kutokana na umuhimu wa maji kwa binadamu.

“Kwa hiyo, kutokana na umuhimu wa kisima hiki, tutahakikisha kinatunzwa na kinadumu kwa muda mrefu, ili tusirudi tena kule tulikotoka kwenye shida ya maji,” alisema Nyamka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Mahabusu la Morogoro, Zephania Neligwa, alisema mahabusu wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu kutokana na kukosa maji ya kuoga na kwa matumizi mengine.

“Gereza letu lina msongamano wa mahabusu na lilikuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu, kuhara na magonjwa ya ngozi, kwa sababu mahabusu hawakuwa na maji ya kuoga.

“Yaani hata chumba cha kuhifadhi wafungwa watatu, kinahifadhi wafungwa saba mpaka wanane wakiwa hawajaoga, wakati usafi wa vyumba vya mahabusu bila maji ni sawa na bure.

“Kwa hiyo, tunashukuru ujio wa kisima hiki kwa sababu kitatusaidia katika matumizi yetu ya kila siku,” alisema Neligwa.

Naye Katibu wa Taasisi ya Islamic Foundation, Mohamed Issa, alitoa wito kwa Serikali iwaruhusu kuhudumia wafungwa katika magereza yote nchini kiroho na kimwili, hasa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ikiwamo kuwalipia madeni wafungwa wanaodaiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles