22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

LUKUVU USICHEKE NA WENYEVITI WA MITAA MATAPELI

TATIZO la matepeli limezidi kuumiza raia ambao wamejikuta katika matatizo makubwa ya kuporwa mali zao.

Matapeli hawa wapo wa aina nyingi na maeneo tofauti tofauti katika miji mikubwa na hata maeneo ya vijijini.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi juzi amebainisha kuwapo matapeli wengi katika ngazi ya Serikali za mitaa, ambao wamegeuka kuwa wajasirimali.

Lukuvi alibainisha hayo wakati akikabidhi hatimiliki 4,000 kwa wakazi wa Kimara, Dar es Salaam.

Akionekana kukerwa, Waziri Lukuvi alisema kuwa baadhi ya wenyeviti wa Serikali za mitaa wamekuwa wakishirikiana na matapeli katika uuzaji wa ardhi dhidi ya wananchi wanyonge.

Kibaya zaidi, Waziri Lukuvi anasema wamefika hatua ya wao kutoa taarifa kwa matapeli juu ya ardhi wanazozijua, kwamba hazina wamiliki ama wamiliki wake halali wamefariki dunia.

Huu ni unyama uliopitiliza kwa viongozi hawa wa mitaa, ambao wamepewa dhamana kubwa ya kuishi na jamii inayowazunguka.

Tena kibaya zaidi, wapo wanaotumia vibaya mihuri waliyopewa kwa kuitumia kuuza mali za masikini ambao hata hawana uwezo wa kwenda kupambana nao mahakamani kwa sababu ya jeuri ya fedha.

Baada ya kuuza viwanja hivyo, wanatoa vibali kwa jeuri bila wasiwasi wowote ule. Hili ni jambo baya ambalo linapaswa kukemewa na kila mtu.

Wote tunatambua kuwa kesi nyingi za migogoro ya ardhi, huanzia ngazi hizi hizi za mitaa.

Tunadhani sasa umefika wakati wa wenyeviti hawa kuwekewa sheria kali dhidi ya utumiaji wa mihuri ili kudhibiti matumizi haramu dhidi ya wananchi wanyonge.

Tunasema hivyo, kwa sababu nyaraka zote za muaziano ya ardhi, utakuta zimetiwa sahihi na mihuri yao, sasa hapo wanaweza kubisha nini kama si wao wanaozalisha migogoro hii?

Tunaamini hatua ya Waziri Lukuvi kuwatolea uvivu wenyeviti hawa wasio waaminifu, utasaidia maofisa wake ambao wametapakaa nchi nzima, kushirikiana na mamlaka nyingine kuangalia upya suala hili.

Lakini pia, jambo hili lishirikishe hata wakuu wa wilaya ambao ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Kwa upande mwingine, tunapongeza hatua ya Serikali kutoa hatimiliki kwa wananchi, tukiamini zitasaidia kuinua uchumi wao kwa kuzitumia kama dhamana ya kupata mikopo benki.

Licha ya hayo, kwa namna moja au nyingine, utaratibu huu wa kutoa hatimiliki kwa wananchi wanaomiliki ardhi na makazi, utaisaidia Serikali kupata mapato tofauti na miaka ya nyuma.

Tunaamini kufikia hatua ya waziri kukabidhi hati hizo, ni wazi kuwa maeneo mengi sasa hayana migogoro ya ardhi, huku viwanja vikipimwa na mamlaka husika.

Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa kuwa na hati ambayo inaweza kumsaidia katika mambo mbalimbali yakiwamo ya kukopa fedha kwenye taasisi za kibenki.

Tunatoa rai sasa kwa Waziri Lukuvi kuwabana maofisa mipango miji kusimamia maeneo yote nchi nzima ili yapimwe.

Sisi MTANZANIA, tunasema Waziri Lukuvi anapaswa kuungwa mkono katika jambo hili ili siku moja tuwe na taifa lisilokuwa na migogoro ya ardhi kila kukicha kwa sababu jambo hili limechukua miaka mingi.

Waziri Lukuvi, tunaamini kutokana na kazi nzuri unayoifanya sasa, utashirikisha wizara nyingine ambazo zinahusika ili kuwabana wenyeviti wa mitaa wasio waadilifu.

Haiwezekani taifa likaingizwa katika matatizo na watu wachache ambao wamepewa dhamana ya kusimamia maendeleo, wao wanazalisha migogoro  kila kukicha.

Tunamalizia kwa kusema katika hili, kila mtu anayeitakia mema nchi yetu, amuunge mkono Lukuvi dhidi ya utapeli huu ambao unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles