24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

GADIEL YAMETIMIA

Na Mohamed Kassara -Dar es salaam

KLABU ya Simba imemtangaza rasmi, beki  Gadiel Michael  kuwa mchezaji wake, baada ya kusainiana naye mkataba wa miaka miwili.

Gadiel ametua Simba, baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na Yanga aliyojiunga nayo akitokea Azam FC.

Usajili huo unafanya idadi ya wachezaji waliosajiliwa na Simba wakitokea kwa watani zao Yanga kuwa watatu, baada ya mlinda mlango, Beno Kakolanya na kiuingo mshambuliaji, Ibrahim Ajib.

Gadiel ataungana wachezaji wengine wapya  waliosajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao ambao ni , Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Viera, Wilker Henrique da Silva wote kutoka Brazil, Sharaf Eldin Shiboub (Sudan), Francis Kahata (Kenya) na Deo Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo(DRC).

Wengine ni Ajibu, Kakolanya, Kennedy Juma kutoka Singida United na Miraji Athuman kutoka Lipuli FC.

Wachezaji hao wataungana na nyota wengine waliokuwamo katika kikosi cha timu hiyo msimu uliopita, John Bocco, Pascal Wawa, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Clatous Chama, Jonas Mkude, Rashid Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Dilunga, Said Ndemla na Mzamiru Yassin.

Beki huyo aliyekulia katika timu ya vijana ya Azam, atakuwa na shughuli pevu ya kuwania namba  na mpinzani wake katika nafasi ya ulinzi wa kushoto, beki mwingine wa  muda mrefu wa Simba, Mohamed Hussein.

Tshabalala ambaye alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, amekuwa mhimili mkuu wa nafasi hiyo, licha ya changamoto aliyoipata msimu uliopita kutoka kwa Mghana, Asante Kwasi.

Akiwa Yanga,  Gadiel mwenye miaka 22, alijihakikishia nafasi hiyo, baada ya kumbwaga Haji Mwinyi ambaye alikuwa mshindani wake wa karibu kwenye upande huo wa kushoto.

Hata hivyo, Gadiel  ni chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki fainali za Afcon chini Emmanuel Amunike, akipiku Tshabalala.

Katika michezo mitatu ya makundi, Gadiel alicheza michezo miwili dhidi ya Senegal na Kenya, huku Tshabalala akicheza mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria.

Ujio wa Gadiel, utaongeza ugumu kwa kocha, Patrick Aussems kuamua nani aanze na nani asubiri  benchi katika kikosi hicho, kinachokabiliwa na mtihani wa wa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuishia hatua ya robo fainali msimu uliopita.

Beki huyo anaingia katika rekodi ya kuzichezea timu zote kubwa za Dar es Salaam, Simba, Yanga na Azam, ilivyokuwa kwa winga Mrisho Ngassa na kipa  Ivo Mapunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles