Na Allan Vicent, Nzega
Fedha zinazotolewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kunusuru kaya maskini zimerejesha heshima ya ndoa ya, Oliva Fubusa, baada ya Mume wake aliyekuwa amekimbia kutokana na ugumu wa maisha kurejea kwa mkewe.
Hayo yamebainishwa jana na Mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Ipilili kata ya Nzega Magharibi wilayani Nzegamkoani Tabora alipokuwa akielezea jinsi Mfuko huo ulivyomnufaisha mbele ya Maofisa wa TASAF kutoka Makao Makuu.
Amesema kuwa kabla ya kuingizwa katika mpango huo alikuwa anaishi na mume wake, Mussa Jackson, lakini walikuwa na hali ngumu sana kimaisha hali iliyopelekea kukimbiwa na mume wake huyo.
Amebainisha kuwa baada ya kuingizwa katika mpango huo mwaka 2015 maisha yake yalianza kubadilika baada ya kufungua genge na kuanza kuuza nyanya, viazi, dagaa, ndizi na kulima mahindi.
“Baada ya kuona maisha yangu yamekaa vizuri, nakula milo 3 kwa siku, watoto wangu 6 wanasoma shule, niliamua kumpigia simu mume wangu aliyekuwa amenikimbia kwa zaidi ya miaka 2 na kumweleza maisha niliyo nayo,” amesema.
Oliva amebainisha kuwa baada ya simu hiyo mume wake hakuamini alichokuwa akielezwa, alisita kujibu, akakaa kimya, lakini baada ya kuulizia kwa majirani akaambiwa mke wake hana njaa tena, sasa hivi anapokea ruzuku ya TASAF.
“Mpaka sasa ninavyoongea mume wangu amesharudi, leo kaenda porini kukata miti, maisha yanaendelea, ananisaidia kwenye biashara yangu na nimeanza kufuga bata na kuku na watoto wetu 3 tunawasomesha sekondari,” alisema Oliva.
Aliongeza kuwa baada ya kuanza kuwezeshwa na TASAF ameweza kujenga nyumba ya vyumba 2, amechimba kisima cha maji cha kutumia nyumbani na amepata maji ya bomba ya mradi wa ziwa Victoria ambapo ameunganishiwa kwa mkopo wa Sh 150,000 na atakuwa analipia kidogo kidogo.
Mtendaji wa Mtaa wa Ipili, Aloyse Kazungu, alikiri kurudi kwa mume wa Oliva baada ya kuona maisha yake yamebadilika na kuanzisha miradi inayompatia kipato kizuri, ameongeza kuwa jumla ya walengwa 25 wananufaika katika Mtaa huo.
Ameishukuru serikali kwa kuleta mfuko huo kwani umesaidia kuziondoka katika dimbwi la umaskini familia nyingi zilizokuwa zimekata tamaa ya maisha.