Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
HAKUNA swali linaloulizwa na wengi kama ni aina gani ya biashara ambayo mtu anaweza kufanya ili kufanikiwa na kupata kipato.
Nimekuwa nikisikia maswali mengi na majibu yake hata mimi nashindwa kupata kutokana na kutokuwa mzoefu na biashara.
Hata hivyo, si kwamba mtu akisomea mambo ya biashara ndio anakuwa na uelewa zaidi kuliko ambaye hajasomea, la hasha! Bali kuna baadhi ya watu huwa na uzoefu au uelewa wa mambo ingawa hawajayasomea darasani.
Hivi karibuni nimekuwa nikipata maswali mbalimbali kuhusu kama mfanyabiashara anatakiwa kujua kwanza ni aina gani ya biashara ambayo anaweza kuifanya na ikamuingizia faida.
Lakini kuna watu au wafanyabiashara wa karne hii ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa tofauti zaidi katika uchaguzi na kupanga mipango juu ya biashara gani inafaa kufanya kwa wakati huo.
Kuna baadhi ya watu na haswa wafanyabiashara walio wengi huwa wanalalamika sana pindi wanapoona kuwa biashara yao inakuwa mbaya zaidi, badala ya kujua na kutafuta tatizo ni nini wanaanza kulaumu na kuanza kuwatuhumu wafanyabiashara wenzake kuwa wanamfanyia hiyana na kuziba riziki yake.
Imani hizo kwa wafanyabiashara walio wengi zimetawala sana kwani wanashindwa kujua tatizo liko wapi na hatimaye wanashikana uchawi, na katika biashara nawahakikishia hakuna uchawi wala ndumba kwa wale wanaoamini. Zipo mbinu na njia sahihi za kufanya mambo kwa mikakati bora.
Kikubwa zaidi ni kujua mbinu za biashara unayoifanya, inataka ufanye nini ili ufikie malengo unayoyatarajia kutokana na biashara unayoifanya kwa wakati huo.
Mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika bila utafiti kwa kudai kuwa na biashara mbaya lakini ni kutokana na kutokujua tu na kukosa msingi mzuri wa biashara yako na uwezo wa kuimudu.
Ngoja nikwambie mfanyabiashara mwenzangu unajua siri kubwa ya biashara, ni kujua ni kitu gani wateja wako wanataka katika mazingira hayo na kinachoendana na wakati.
Ingawa kila bidhaa huuzika kwa maana kwamba inategemeana ni aina gani ya mzigo na ni wa gharama gani.
Lakini vilevile kuna baadhi ya bidhaa ambazo unaweza kuweka kwa ajili ya kuuza lakini nao pia inategemea ni mzigo wa aina gani na unauzia katika mazingira gani.
Hiyo itakusaidia kujua kuwa unaweza kukaa na mzigo wa biashara yako kwa muda gani toka umeweka kwa akili ya kuuza, kwani kuna bidhaa nyingine ambazo zilitakiwa kuisha kuuzwa ndani ya siku au wiki moja kwa mfanyabiashara mwingime huchukua hata mwezi mzima.
Hata hivyo, ni muhimu zaidi kubadilisha aina ya bidhaa kwa ajili ya kuwaletea wateja wako vitu tofauti kwani ukiona biashara unayofanya haikulipi, basi si vyema ukaendelea kuifanya unaweza kufanya mabadiliko na kuanzisha biashara nyingine.
Nakushauri mfanyabiashara mwenzangu kuwa kila biashara unayoifanya inalipa, kama utazingatia haya basi katika uchaguzi utakaopanga ni kitu gani au biashara gani unataka uifanye, ni lazima uwe na malengo stahiki hususani kujua ni aina gania ya biashara ambayo unaweza kuifanya kwa wakati huo na iendane na mazingira.
Hivyo basi, ni bora mtu kuuliza biashara gani inalipa badala ya kukurupuka na kuanzisha biashara na hatimaye inakuja kuanguka na kuanza kulalamika kwa kupata hasara ambayo ni matokeo hasi juu ya biashara hiyo.
Ni vyema zaidi kwa mfanyabiashara wa kiwango chochote kile, kwa maana ya mdogo unaechipukia au mfanyabiashara mkubwa, unakijua unachokifanya katika biashara yako.
Ingawa unaona utaonekana mjinga kwa kuuliza mambo ya msingi na kufanya vitu ambavyo huvijui na hata vikikushinda inakuwa ni vigumu zaidi kutatua peke yako wakati ungeuliza na kujua ingekusaidia sana katika kuiendeleza biashara yako.