UTAJIRI mkubwa alioubeba ndio umefanya leo hii aendelee kukumbukwa, huyu ni Bi Shakila, kama alivyofahamika na mashabiki zake, huku wazazi wake wakimpa jina la Tatu Said.
Katika simulizi hii ya maisha ya Bi Shakila ndani ya muziki wa taarabu iliyotuchukua takribani majuma matatu, leo tunahitimisha.
Wiki iliyopita tulikomea pale ambapo Bi Shakila anamkaribisha Patricia Hilary ndani ya bendi iliyokuwa inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Mgulani, jijini Dar es Salaam akitokea Tanga.
Bi Shakila alijiunga na JKT Taarabu mwaka 1985, ambapo alifanikiwa kutunga nyimbo nyingi zilizoipandisha chati bendi hiyo, kama ule Natafuta Mbebaji.
Mkongwe huyu ni mwenyeji wa Kanda ya Kati, kabila lake likiwa ni Mnyiramba, huku mama yake akiwa ni Mzigua kutoka mkoani Tanga, kiukweli ujio wake ndani ya bendi ya JKT Taarabu ulileta mapinduzi makubwa, hasa kwenye upande wa albamu.
Albamu kama Mguu Mjini Mguu Shamba, aliyoshirikiana kikamilifu na mtoto wake aitwaye Mwape, ni albamu kubwa mno kwenye historia ya muziki wa taarabu nchini.
Albamu hiyo ilitanguliwa na albamu nyingine kama vile Uliza Kwanza, Mama na Mwana na Mzigo iliyotoka mwaka 2009.
Nyimbo zilizozinogesha albamu hizo ni mchanganyiko wa zile zote ambazo zilifanya vizuri akiwa kwenye bendi za Black Star na Luck Star.
Imezoeleka muziki wa taarabu mara nyingi huwa unabeba maudhui ya mapenzi. Kwa Shakila, licha ya kutunga nyimbo za mapenzi zenye mafumbo, aliamua kutanua wigo wake na kuimba nyimbo za siasa za kuwasifu baadhi ya viongozi wa Bara la Afrika.
Mfano ni ule uitwao Viva Frelimo, uliokuwa unakisifia chama kilichopigania uhuru nchini Msumbiji chini ya Rais Samora Machel.
Uwezo wake wa kutunga mashairi, ubunifu na kujua kuchezea sauti yake nyororo inamfanya leo hii aendelee kuishi kwenye mioyo ya mashabiki wa muziki wa taarabu. Alihakikisha anawakamata mashabiki popote pale ambako bendi zake alizozitumikia zilikuwa zikitumbuiza.
Bi Shakila anaingia kwenye orodha ya nyota wakongwe wa muziki wa taarabu ambao wengine wameshatangulia mbele za haki, ila nyimbo zao zimekuwa ni urithi tosha kwa kizazi kipya cha muziki nchini.
Wakongwe wa muziki hao ni kama vile Abeid na mkewe, Salama Abeid, Issa Matona, Mwinyifadhi Abdallah, Mohamed, Mwanahela Salum, Fatma Baraka maarufu kama Bi Kidude, Abbas Mzee na Patricia Hilary, ambaye hadi sasa bado anasukuma gurudumu la muziki huo.
Huu ndio mwisho wa mfululizo wa simulizi za Bi Shakila, ambaye amefariki ghafla Agosti 19, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake Mbagala Charambe na akazikwa siku iliyofuata hukohuko Mbagala Charambe, ambapo mazishi yake yaliongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete.
Maoni yalete hapa 0714288656