27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ni simanzi Bukoba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (watano), akiongoza wananchi katika kuaga miili ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera Uwanja wa Kaitaba jana
WaziriMkuu, Kassim Majaliwa (watano), akiongoza wananchi katika kuaga miili ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera Uwanja wa Kaitaba jana

* Majaliwa aongoza maelfu kuaga miili 16

* Yumo mjamzito, waathirika kulipwa fidia

NI simanzi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jana kuongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba Mjini kuaaga miili ya watu 16 waliofariki dunia, kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea juzi.

Tetemeko hilo lilitokea juzi  alasiri na kusababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa.

Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Akitoa salamu za Serikali kwa waafiwa na wananchi wa mkoa huo, Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Rais, Dk. John Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.

“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu  Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” alisema.

Alisema Kamati ya Maafa ambayo ipo chini ya ofisi yake itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba Mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Kutokana na wananchi wengi waliopatwa na tatizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka  kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na hayafai kutumika.

Majaliwa alitoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.

Mapema Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera, ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole kwa waathirika hao.

“Kama wapo wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hospitali kubwa, Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.

“Ndugu Watanzania wenzangu, tukio hili limesababisha simanzi  kubwa,  si kwa Kagera pekee, bali kwa Watanzania wote, tumekuwa tukiyasikia matukio kama hayo  katika nchi nyingine, lakini kwa sababu yametufika na sisi tutawasiliana na watalaamu  wa maafa kutoka ofisi yangu ili kuwasiliana na wanajioolojia ili kufuatilia kujua kama tetemeko hili ni endelevu au ndio limefikia mwisho,” alisema.

Pia ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia kama kuna tetemeko jingine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu alisema wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka.

“Pamoja na tathimini tunayoendelea kufanya kwa kina, mkoa unaendelea kuwatafutia makazi ya muda waathirika wote,”alisema.

Alisema waliamua kupeleka majeneza hayo Uwanja wa Kaitaba ili kuwapa nafasi waombolezaji kutoa heshima zao za mwisho, kisha kukabidhiwa kwa jamaa zao kwa ajili ya maziko.

Alisema Serikali pia imegharamia sanda, majeneza na usafiri kwa marehemu wote kwenda ambako familia zimepanga mahali pa kuzika kwa mujibu wa imani za dini zao.

“Tulipokea majeruhi  253 katika hospitali ya rufaa ya mkoa, lakini mpaka leo baada ya jitihada za madaktari na wauguzi, majeruhi 83 waliruhusiwa kutoka hospitali baada ya matibabu hivyo wamebaki 170 ambao bado wanaendelea kuhudumiwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kutoka Dodoma, tetemeko hilo la ardhi lililotokea juzi saa 9:27 alasiri likiwa na ukubwa wa kipimo cha Ritcher 5.7 na kwamba kitovu chake kilikuwa kaskazini magharibi ya mji wa Bukoba katika miji ya Nsunga na Buyango.

Akizungumza kwa niaba ya wafiwa, Advera Respisius alisema msaada wa Serikali umekuwa wa maana kubwa kutokana na baadhi ya familia kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za sanda, majeneza na hata usafiri wa kusafirisha wafiwa wao kwenda vijijini kwa ajili ya maziko.

“Kwa niaba ya wafiwa wenzangu, maana na mimi nimefiwa na mtoto wangu aliyekuwa mjamzito wa miezi nane, natoa shukrani zangu kwa Serikali kwa kutusaidia jeneza, sanda na usafiri, janga hili limetukumba tukiwa hatujajipanga kwa baadhi yetu ilikuwa ni kazi ngumu kumudu vitu hivi, tunashukuru,” alisema.

ASKOFU KILAINI

Akizungumza wakati misa ya kuwaaga maheremu hao, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini alisema watu waliopatwa na tukio hilo wawe wavumilivu, huku akiiasa jamii kushirikiana nao kwa kila hali.

Alisema wananchi watumie muda mwingi kusali kwa sababu hakuna mtu anayejua siku wala saa anapoweza kupatwa na matatizo.

UWANJA WA KAITABA

Katika Uwanja wa Kaitaba kuanzia saa 2 asubuhi, mamia ya wananchi walikuwa wamefurika, hali iliyosababisha kuwapo na msongamano mkubwa.

Magari yaliyobeba miili ya marehemu yalianza kuingia saa 6 mchana, ghafla waombolezaji wengi walionekana wakitaharuki  huku wengine wakilia.

Hali hiyo ilizidi pale majenezi 16 yalipoanza kushushwa kwenye magari ya Serikali ambayo yalikuwa yanatokea Hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Baada ya miili yote kuwasili, nyimbo za maombolezo zilikuwa zikipigwa, huku waombelezaji wakimsubiri Waziri Mkuu.

Majaliwa aliwasili uwanjani hapo saa 7:30, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro aliwaomba wananchi watulie.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa pole kwa wananchi wote walioathirika
na tetemeko la ardhi katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Tabora ambalo limesababisha
vifo vya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene alitoa wito kwa Watanzania wote katika maeneo yaliyopatwa na tetemeko hilo na wengine kutoka nje ya sehemu hizo, kuguswa na tukio hilo na kuwasaidia waathirika. Nao Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetuma salamu za pole kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kutokana na vifo vya zaidi ya watu 15 vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea juzi.

Katika salamu hizo zilizotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka kwa niaba ya umoja huo, alisema wamepokea kwa
masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya vifo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles