Judith Siaga TUDARCo na Mashirika
Umoja wa Ulaya umetangaza leo Jumatano Septemba 15, kuwa utachangia dozi nyingine milioni 200 za chanjo ya virusi vya corona kwa mataifa maskini.
Hatua hiyo inayoongeza maradufu ahadi yake ya mchango wa chanjo wenye lengo la kupiga jeki juhudi za kukabiliana na janga hilo la kiafya duniani.
Aidha, ahadi hiyo mpya imetangazwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, wakati wa hotuba yake ya kila mwaka ya mwelekeo wa kisera na kiutendaji ndani ya Umoja wa Ulaya.
Von der Leyen amesema dozi milioni 200 za nyongeza zitatolewa katika kipindi cha hadi katikati ya mwaka unaokuja na kuutaja mchango huo kuwa uwekezaji mkubwa kwa afya na mshikamano wa ulimwenguni.
Msaada huo wa EU unakuja wakati mataifa masikini bado yanajikongoja kwenye kampeni ya utoaji chanjo inayotatizwa na uhaba wa chanjo zenyewe pamoja na upinzani dhidi ya chanjo unaotokana na upotoshaji.