MADRID, HISPANIA
MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya Barcelona, Samuel Eto’o, anaamini nyota mpya wa Real Madrid, Eden Hazard atakuja kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia ya Ballon d’Or akiwa na kikosi hicho.
Hazard amejiunga na Real Madrid wakati huu wa majira ya joto akitokea Chelsea kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 150, baada ya kuitumikia Chelsea kwa miaka saba. Hivyo Eto’o amedai mchezaji huyo ataacha historia nchini Hispania kutokana na uwezo wake.
‘Hazard atakuja kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or akiwa na Real Madrid, mwanzo hakuwa na thamani kubwa, lakini sasa thamani yake itakuwa kubwa sana kwa kuwa yupo katika moja ya timu kubwa hivyo macho ya wengi yatakuwa kwake kutokana na ujio wake,” alisema Eto’o.
Hata hivyo Eto’o aliongeza kwa kumfananisha mchezaji huyo na nyota wa Barcelona na timu ya Argentina, Lionel Messi. Hazard na Messi sasa watakutana mara kwa mara kwenye Ligi ya nchini Hispania tofauti na ilivyo awali akiwa na Chelsea.
“Hazard akiendelea kufanya vizuri ataweza kuwa kama Messi, ana nafasi kubwa ya kutengeneza jina zaidi katika timu hiyo ya Real Madrid,” aliongeza Eto’o.
Eto’o alicheza jumla ya michezo 199 ndani ya Barcelona tangu mwaka 2004 hadi 2009, huku akiwa pamoja na Messi kwenye kikosi hicho. Hata hivyo aliwahi kucheza alicheza jumla ya michezo saba akiwa Madrid tangu mwaka 1997 hadi 2000.
Maandalizi ya msimu mpya wa ligi, Real Madrid hawajaanza vizuri katika michezo yao ya kirafiki, huku mwishoni mwa wiki iliopita wakikubali kichapo cha mabao 7-3 dhidi ya wapinzani wao Atletico Madrid.
Hata hivyo walipokea kichapo kingine kutoka kwa mabingwa wa nchini Ujerumani, Bayern Munich, lakini waliweza kuibuka na ushindi dhidi ya Arsenal kwa mikwaju ya penalti. Kiwango hicho kilichooneshwa na Madrid kimewashangaza wengi hasa kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichokitumia kwa ajili ya kuongeza wachezaji wakati huu wa kiangazi.