Susan Uhinga , Tanga
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein, amewataka Watanzania kuwapuuza wanaobeza kuwa Mwenge wa Uhuru uwekwe Makumbusho ya Taifa kuwa si watu wazuri na kwamba wana lengo la kukiuka mawazo ya muasisi wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Dk. Shein ameyasema hayo leo wakati wa sherehe za kilele cha mbio za mwenge huo, zilizoambatana na kumbukumbu ya hayati Mwalimu Nyerere zilizofanyika kitaifa katika Viwanja vya Mkwakwani, mkoani Tanga.
Amesema Serikali itahakikisha inauenzi na kuudumisha mwenge wa uhuru ili kuendeleza mambo muhimu yalioachwa na Mwalimu Nyerere.
“Hatutakatishwa tamaa na watu wanaoupuza na kuubeza mwenge wa uhuru na tutahakikisha tunapambana nao ili kulinda heshima ya taifa hili,” amesema.
Aidha, amesema amefurahishwa na uwezo na ubunifu unaofanywa na vijana na kuahidi serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwaendeleza katika nyanja mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Shein amewaasa vijana kufanya kazi za halali na kujiepusha na mambo maovu yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani taifa linawategemea na kwamba vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa.
“Vijana msijihusishe na madawa ya kulevya kwani kwa kufanya hivyo tunapoteza nguvu kazi ya taifa ambayo ilikuwa ikitegemewa katika uzalishaji mali,” amesema Dk. Shein.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku 10 kwa halmashauri zilizofanya vibaya katika utekelezaji wa miradi ya serikali kufika ofisini kwake na kutoa taarifa kwanini miradi hiyo imekuwa chini ya kiwango.