23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Hoseah: TLS haiwezi kuendelea kutegemea wanachama tu

*Asisitiza TLS itawekeza ili kujiimarisha kiuchumi

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Mgombea wa nafasi ya Urais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Dk. Edward Hoseah amesema chama hicho hakiwezi kuendelea kutegemea michango ya wanachama pekee badala yake kinapaswa kuwekeza.

Dk. Hoseah ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 9, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa uwekezaji ndio njia pekee ya kukikwamua kiuchumi na kwamba iwapo atapata nafasi ya kuchaguliwa tena atalitekeleza hilo.

“Dhana yangu ni kuona TLS inafanya uwekezaji ili mwanachama apunguziwe mzigo wa kulipa ada ambazo anaona ni kubwa.

“Kama kiongozi lazima utafute mbinu mbadala na mbadala huo ni kuwekeza, hivyo nikifanikiwa kuingia madarakani tena TLS tutawekeza, tutapunguza kuwategemea wanachama,” amesema Dk. Hoseah.

Dk. Edward Hoseah.

Akifafanua zaidi kuhusu uwekezaji Dk. Hoseah amekitolea mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo amesema kuwa kinanufaika kupitia uwekezaji wake wa jengo la kibiashara la Mlimani City.

“Mfano mzuri ni chuo kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinanufaika na uwekezaji wake pale Mlimani na TLS ndivyo tunavotaka kufanya.

“Hivyo, badala ya kuwategemea wanachama kimapato chama kitawekeze kama ilivyo moja ya majukumu ya TLS,” amesema.

Amesema wengi wa wanachama wamekuwa hawana uwezo wa kulipia michango ya mara kwa mara kwani michango yao ni Sh milioni 900 pekee huku uendeshaji wa TLS ukiwa Sh bilioni 6 na kusisitiza kuwa anajivunia baraza lake.

“Nafurahi na baraza langu la uongozi lililopita kwamba tuliweza kufanikisha suala la ardhi, huwezi kuwa chama ukategemea tu michango ya wanachama, lazima ujiongeze.

“Maisha ni magumu Wanasheria wenzangu wamekuwa wakisema kuwa gharama za kuhuisha vyeti vyao ni kubwa hivyo wangependa zipungue, na hasa vijana, katika hili sioni njia mbadala zaidi ya kuwekeza,” amesema Dk. Hoseah.

Amefafanua kuwa tayari chama hicho kimefanikiwa kupata ardhi katika mikoa ya Dodoma na Mbeya huku akishukuru ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiupata kutoka serikalini.

“Tumepata kiwanja Dodoma ambacho tumepewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, pia tumepata kiwanja kingine jijini Mbeya heka 10 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Juma Homera, hivyo hivi vitatusaidi kuwekeza na ndio maana kauli mbiu yangu imekuwa ni kuwekeza.

“Hatuwezi kuwakamua wanachama wetu kila mwaka, dunia nikuwekeza ili kupunguza mzigo kwa mwanachama ambao nao uwezo wa fedha ni mdogo, tuache kulalamika na kulia kwamba hatuna fedha tuwekeze,” amesema Dk. Hoseah.

TLS kinatarajia kufanya uchaguzi Mkuu katika nafasi ya Rais, Makamu wa Rais na Mweka hazina.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Mei 27, mwaka huu jijini Arusha, ambapo tayari kampeni za wagombea urais zimeanza tangu Aprili 15 na zinatarajiwa kuhitimishwa Mei 26, mwaka huu siku ambayo pia utafanyika uchaguzi katika nafasi nyingine ukiwamo ya viongozi wa kanda.

Uchaguzi huo ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambao hufanyika kila baada ya mwaka mmoja.

- Advertisement -
Previous article
Next article
4 reasons to learn how to breathe correctly

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles