25.3 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Afisa JWTZ atunukiwa Nishani CISM

Na Meja Selemani Semunyu, JWTZ

MKURUGENZI wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM), Kanali Joseph Bakari, ametunukiwa Nishani iitwayo ‘Officer’ kwa kutambua moyo wa kujituma, bidii na juhudi zake katika kuendelea michezo Jeshini ikiwa ni sehemu ya kutekeleza malengo ya CISM kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kueneza amani duniani.

Kwa Mujibu wa Mtandao wa CISM Nishani hiyo ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani International Military Sports Council -CISM),yenye makao yake makuu Jijini Brussels nchini Ubelgiji, imetolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka ulioanza Mei 1,2022, jijini Lima Peru.

Mkutano huo ambao ni wa kwanza kwa wanachama kukutana uso kwa uso tangu mwaka 2019 kutokana na janga la Uviko 19, uliohudhuriwa na nchi wanachama 65 kutoka katika mabara ya Afrika, Amerika, Asia na Ulaya.

Nishani hiyo alivishwa na Rais wa Baraza hilo Brig Gen Herve Piccilliro kutoka Ufaransa mbele ya wajumbe takribani 400 waliohudhuria mkutano huo kutoka pande zote duniani.

Kanali Bakari anakuwa ni Mtanzania pekee kupata nishani ya pili ya utendaji bora katika baraza hilo. Mwaka 2008 aliwahi kutunukiwa nishani iitwayo Grand Knight nchini Suriname mjini Paramaribo kufuatia juhudi zake za kukuza vipaji vya michezo kupitia kituo cha Twalipo Youth Sports ambacho alikianzisha.

Baraza la michezo ya Majeshi hutunuku nishani kwa yeyote ambaye kwa matendo yake ametekeleza malengo ya CISM na kwa utendaji wake amechangia maendeleo ya michezo kwa majeshi ya nchi wanachama.

Kanali Joseph Bakari katika akiwa na maafisa wenzake baada ya kutunukiwa Nishani hiyo

Baadhi ya Wanajeshi waliotunikiwa nishani Pamoja na Kanali Bakari katika madaraja mbalimbali ni Pamoja na Maj Gen Katirima Manoni Phinehas (Uganda), Kanali Moussa Moise Keita (GUINEA), Mteule Bongseok Kim (USA), Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Peru Luteni Jenerali David Guillermo Ojeda Parra, Kapteni wa Wanamaji Spyridon Andriopoulos (UGIRIKI), Meja Jenerali Grancisco Javier Costa Gallegos (PERU), Luteni Kanali Lars Gerhardsson (SWEDEN), Luteni Kanali Jan Van den Dool (UHOLANZI).

Aidha, mkutano huo pia uliazimia kuendelea kusimamia msimamo wa kutoingilia mgogoro unaoendelea kati ya nchi mbili wanachama wa Baraza hilo ambazo ni Urusi na Ukraine, kufuatia nchi ya Ukraine kutoa shinikizo kwa baraza hilo ili iifungie na kuitenga nchi ya Urusi kushiriki kwenye shughuli za baraza hilo kutokana na mgogoro huo.

Akiwasilisha maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi Rais wa CISM Brigedia Jenerali Herve Piccilliro alisema kwa mujibu wa kanuni baraza hilo sio chombo cha kisiasa, halitakuwa upande wowote na hivyo haitaifungia wala kuitenga Urusi au kuifuta uanachama, isipokuwa nchi wanachama zipo huru kutoshirikiana na Urusi kama sehemu ya maagizo ya nchi zao.

Katika hatua nyingine mkutano huo ulifanya chaguzi kwa nafasi za Rais , Katibu Mkuu na Mhazini.

Katika nafasi ya Rais aliyekuwa anagombea nafasi hiyo akiwa ni mgombea pekee na ambaye alikuwa madarakani Brigedia Jenerali Herve Piccilliro alishindwa kutetea nafasi yake baada ya kupata kura 27 za Ndio, 22 za Hapana na 16 za kutofanya uamuzi wa kuchagua ( abstention). Hivyo hakuchaguliwa kutokana na kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote ( absolute majority).

Kwa matokeo hayo nafasi ya Rais wa baraza hilo imeshikiliwa kwa muda na Rais wa Bara la Ulaya Kanali Dirk Schwedi hadi uchaguzi ujao mwakani.

Katika nafasi ya Katibu Mkuu mgombea pekee Kapteni wa Wanamaji Recchia wa Italia alichaguliwa na kwa nafasi ya Mhazini Kanali Sven Serre wa Ubelgiji alichaguliwa.

Aidha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo aliyemaliza muda wake Kanali Dorah Mamby Koita wa Guinea alichaguliwa kuwa Balozi maalum wa Baraza hilo.

“CISM” ( International Military Sports Council/ Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani ni moja kati ya Shirikisho kubwa duniani linalojishughulisha na michezo anuai (multdisplinary).

Baraza hilo linaloundwa na majeshi ya nchi wanachama  140 Tanzania ikiwemo.
Dhima Kuu ya Shirikisho hilo ni kutumia michezo kama njia na zana ya kueneza amani duniani badala ya vita.

Hivyo kupitia Shirikisho hilo nchi wanachama zinaaswa na kupewa wito kuwa yale waliyokuwa wanayafanya katika uwanja wa vita sasa wayafanye katika viwanja vya michezo.

Shirikisho hilo huandaa mashindano zaidi ya 20 ya dunia kwa Mwaka mashindano ya Mabara na kikanda katika michezo zaidi ya 30.

Shirikisho limekuwa likisisitiza Masuala yahusiyo uongozi,  uamuzi, ualimu,  tiba na katazo la matumizi ya nguvu za kusisimua misuli katika michezo.

Aidha, Mkurugenzi wa baraza hilo, Kanali Bakari aliwasilisha mada mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles