30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko azitaka sekta zote nchini kusoma na kusimamia Sera Mpya ya Taifa ya Biashara

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ametoa wito kwa sekta zote nchini kusoma na kusimamia Sera Mpya ya Taifa ya Biashara na kuifanyia kazi. Wito huo umetolewa leo, Julai 30, wakati wa uzinduzi wa sera hiyo mpya jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali, mawaziri, naibu mawaziri, na makatibu wakuu.

Dk. Biteko amezindua Sera Mpya ya Taifa ya Biashara na kusisitiza umuhimu wake katika kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya kimataifa. Alisema kuwa sera hiyo inatakiwa kutumiwa kama nyenzo ya kuondoa vikwazo vya biashara na kuweka mfumo wa sheria unaolenga kuimarisha na kukuza biashara.

“Ofisa wa serikali lazima utambue kuwa heshima yako ya kukaa hapo ofisini ni kuhakikisha umewezesha watu kufanya biashara na kupata faida, siyo kuwakwamisha. Kuna watu ambao kazi yao kubwa ni kukwamisha wengine,” alisema Dk. Biteko.

Aliongeza kuwa mchango wa sekta ya biashara kwenye pato la taifa bado ni mdogo, hivyo kuna umuhimu wa kutumia sera hiyo kuhakikisha biashara inarahisishwa na mchango wake unaongezeka kwenye pato la taifa.

“Watu walilalamikia sana kwamba sera yetu imepitwa na wakati. Sasa baada ya kuifanyia mabadiliko ni muda wa kuonyesha dunia kwamba tumefanya mabadiliko na tunakwenda na kasi ya dunia,” alisema Dk. Biteko.

Aliendelea kusema kuwa sera ni nyaraka tu, na kama haitafanyiwa kazi itabaki kama kitabu cha hadithi. Aliwataka maofisa wa serikali kubadilisha mtazamo na fikra zao, na kutekeleza yaliyoandikwa kwenye sera hiyo.

“Hakuna faida ya kuwa na sera nzuri lakini wakawepo maofisa ambao kazi yao ni kukwamisha wafanyabiashara. Tunahitaji sera kuwa kiunganishi baina ya wafanyabiashara na serikali,” alisema Dk. Biteko.

Aliwataka wafanyabiashara wote nchini wafahamu kuwa serikali iko kwa ajili yao na inapenda kuona wananufaika na biashara wanazofanya. Hata hivyo, aliwaonya wale wenye tabia ya kukwepa kodi.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alisema sera hiyo imewezekana kutokana na msaada wa wadau mbalimbali zikiwemo balozi za nchi mbalimbali na kampuni ya Trade Mark Afrika. Alisema wadau wengi wamehusishwa na lengo lilikuwa kupata sera inayoakisi hali halisi ya sasa.

“Wadau wengi sana wamehusishwa na lengo letu ilikuwa kuhakikisha tunapata sera inayoakisi hali halisi ya sasa. Nawapongeza wataalamu wa wizara yangu, wamefanya kazi usiku na mchana na kupitia sera hii tunatarajia kuongeza sana mauzo ya nje ikiwemo masoko ya Afrika,” alisema Dk. Jafo.

Waziri wa Viwanda Zanzibar, Omar Shaban, alisema sera hiyo inaenda kujibu changamoto za ndani na kutatua kero ikiwemo za Muungano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Trade Mark, Elibariki Shammy, alisema miundombinu imeboreshwa kwenye mipaka ikiwemo Tunduma kupunguza foleni na vizuizi vya biashara kwenye korido zinazoathiri biashara.

“Tumepunguza vizuizi vya ukaguzi barabarani kutoka zaidi ya 50 hadi sasa hivi vizuizi ni vitatu tu,” alisema Shammy. Aliongeza kuwa serikali inasikiliza sauti ya sekta binafsi na kufanyia kazi, na kujengea uwezo vijana, wanawake, na makundi maalum kwa fursa ambazo serikali inatoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles