Walter Mguluchuma -Katavi
JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi, limemkamata na linamshikilia Diwani wa Kata ya Ikuba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi, Emanuel Washeri (43) kwa tuhuma za kuwahamasisha wananchi kulishambulia kwa kulipiga mawe gari la Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda ambae alikuwa kwenye gari hilo akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama waliokuwa wakifuatilia utaratibu wa mpango wa stakabadhi gharani .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa saba mchana katika Kijiji cha Kashishi Kata ya Ikuba Tarafa ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele
Alisema siku hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda alikuwa ameongozana na kamati yake ya ulinzi na usalama huku wakiwa na askari polisi wawili walifika kwenye Kijiji cha Kashishi Kata ya Ikuba kwa lengo la ufatiliaji wa mpango wa stakabadhi gharani .
“Wakati wakiwa kwenye kijiji hicho walikamata gari lenye namba za usajili T 924 DNE aina ya Fuso mali ya Matamba Enterprises iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Yusuph Zephania mkazi wa Sumbawanga mkaoni Rukwa wakiwa wanapakia mazao aina ya ufuta nyumbani kwa diwani Emanuel Washeri kinyuma na maelekezo ya kamati hiyo ya ulinzi na usalama.
Kamanda Kuzaga alisema ndipo lilipotokea kundi la vijana lililokuwa likiongozwa na watu wawili ambao ni Mwandu Ngarika(25) na Bila Charles(28) walihamasishwa na diwani huyo kufanya fujo kwa mkuu huyo wa Wilaya ya Mlele .
“Baada ya kuhamasishwa walianza kufanya fujo kwa kumrushia mawe Mkuu wa Wilaya Rachel Kasanda pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama .
“Hali hiyo ya vurugu ilipelekea askari polisi waliokuwa kwenye msafara huo kuchukua hatua ya kuwatawanya watu hao ili kumwokoa Mkuu huyo wa wilaya asiodhurike na watu hao,” alisema
Kamanda Kuzaga alisema askari hao walifyatua risasi za moto hewani na mabomu matatu ya kishindo ambayo hata hivyo hatakuleta madhara kwa wananchi .