Mohamed Hamad, Simanjiro
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi, amesema zoezi la utambuzi wafanyabiashara ni fursa kwao kwani watalipa kodi kulingana na mitaji yao.
Myenzi ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 10, akizungumza na wafanyabiashara wadogo katika Mji Mdogo wa Simanjiro ambapo amesema serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwatambua na kuwakadiria kodi kulingana na mitaji yao.
“Hili zoezi ni kwa ajili yetu wenyewe kutambulika katika mfumo rasmi, kutunza kumbukumbu zetu sahihi na kupata fursa zingine ambazo zipo, kwani nchi hii ina mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ipatayo 19 inayowahusu wajasiriamali,” amesema Myenzi.
Aidha, amesema hatua hiyo pia ni fursa ya watu kujiunga katika vikundi na kupata elimu ya biashara, kwani wapo waliojiunga TRA lakini leo wanataka kurejea kuwa wajasiriamali ilihali walishakadiriwa mapato yao kuwa wanastahili kulipia huko.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara hao waliomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia zaidi kwani bado hawajaimarika kiuchumi kulingana na mdororo wa kiuchumi.