29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

DC ALIYEJIUZULU AONDOKA UYUI

*Ikulu yathibitisha

Na AGATHA CHARLES-

DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, amethibitisha kujiuzulu kwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele.

Kupitia taarifa yake iliyoandikwa kwa kifupi na kutumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Msigwa, hakutaja sababu ya Mnyele kuomba kujiuzulu bali alisema: “Ombi la Mnyele aliyeomba kujiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora limekubaliwa na Rais Dk. John Magufuli. Nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora itajazwa baadaye.”

Taarifa hiyo ya Ikulu ilitumwa jioni ya jana wakati asubuhi yake Mnyele alikuwa tayari ameshaondoka katika kituo chake cha kazi cha Uyui na kuja Dar es Salaam.

Gazeti hili lilipata taarifa na baadaye kuthibitishwa na Mnyele mwenyewe kwa njia ya simu kuwa alikuwa yuko safarini akitoka mkoani humo na angefika Dar es Salaam jana jioni akitumia usafiri wa ndege.

Alitoa taarifa hizo alipozungumza na gazeti hili saa tano asubuhi alipokuwa uwanja wa ndege akisubiri kupanda ndege na kumtaka mwandishi amtafute baada ya saa 10 jioni.

“Tayari niko Dar es Salaam nimeshatoka Uyui, huko nitarudi kukabidhi mwenzangu atakapoteuliwa,” alisema Mnyele.

Gazeti hili lilipotaka kujua sababu za kuchukua uamuzi huo, alisema ulikuwa ni uamuzi binafsi na alimweleza Rais Magufuli hivyo hawezi kuutaja hadharani.

“Uamuzi wa mteuliwa na anayeteuwa ni privacy (siri), hizo ni sababu binafsi, mimi au rais hawezi kuweka hadharani,” alisema.

Jana gazeti hili liliripoti kuwa chanzo cha uhakika kilisema kuwa Mnyele aliandika barua ya kuomba kujiuzulu tangu mwaka jana kwa Magufuli kwa kufuata taratibu zote na ombi lake lilikubaliwa wiki hii.

Pia iliripotiwa kuwa aliwaaga watumishi wa halmashauri hiyo kwa kupita kila idara akianzia ofisini kwake.

Awali kabla ya taarifa ya Ikulu kutolewa, gazeti hili lilikuwa limekwishawasiliana kwa njia ya simu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ambaye alisema hakuwa na taarifa rasmi za kujiuzulu kwa Mnyele.

“Bado sijazipata, nikizipata tu nitazitoa,” alisema Simbachawene.

Juzi, gazeti hili liliripoti kuhusu kujiuzulu kwa Mnyele ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria msomi akiwa amedumu katika wadhifa huo kwa miezi minane tangu ateuliwe na Magufuli.

Moja ya sababu zinazotajwa na wadadisi wa mambo kumfanya Mnyele kuondoka katika nafasi hiyo ni masilahi yanayojumuisha posho na mshahara wa nafasi ya DC unaoelezwa kuwa ni mdogo.

Inadaiwa pia Mnyele alikuwa akihusika na kesi kubwa zilizomwingizia mamilioni ya shilingi na kwamba katika wadhifa huo hakuweza kuzipata.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2014, wakati wa Bunge la Novemba, jina la Mnyele lilitajwa bungeni wakati wa kujadili sakata la Kampuni ya IPTL na PAP.

Hilo lilitokana na kufunguliwa kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, mwaka huo chini ya hati ya dharura na kampuni hizo chini ya mawakili kutoka Kampuni za uwakili za Bulwark Associates Advocates, Asyla Attorneys na Marando, Mnyele & Co. Advocates.

Kutokana na hilo, lilitolewa zuio la mahakama kuwa suala hilo lisijadiliwe bungeni ndipo baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walimtuhumu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, kuhusika na kesi hiyo.

Hapo ilimlazimu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kufafanua kuwa Mwanasheria wa IPTL na PAP alikuwa ni Mnyele na kwamba ni kweli Marando anafanya kazi kampuni hiyo lakini hakuhusika kufungua kesi hiyo.

Mnyele ni DC wa pili kuachia wadhifa huo baada ya Ally Maswanya aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi na kukacha kabla ya kuapishwa Julai, mwaka jana.

Ingawa hakuweka wazi sababu, lakini ilidaiwa kuwa Maswanya ambaye ni Meneja wa Tigo, Kanda ya Ziwa alikuwa akilipwa mshahara wa Sh milioni 20 baada ya makato mbali na nyongeza na marupurupu.

Taarifa zaidi zilidai kuwa kila baada ya miezi mitatu anapatiwa nyongeza ya kati ya Sh milioni 10 au 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles