29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

BILIONI 5/- ZA UDA ZAIVURUGA UKAWA

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

SIKU tatu baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa siku tano kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupangia matumizi Sh bilioni 5.8 zilizotolewa na Kampuni ya Simon Group kwa mauzo ya asilimia 51 za hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), agizo hilo tayari limewagawa madiwani Ukawa kiasi cha baadhi yao kutaka kupigana.

Akizindua awamu ya kwanza wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART), Jumatano wiki hii Rais Magufuli, alitoa siku tano kwa Jiji la Dar es Salaam kufanya uamuzi juu ya matumizi ya Sh bilioni 5.8 zilizotolewa na mmiliki Simon Group ambaye pia ni mbia kwenye mradi huo wa mabasi yaendayo haraka.

Kutokana na agizo hilo, jana kiliitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam huku ajenda kuu ikihusu mapendekezo ya kutumia fedha hizo.

Kutofautiana kwa madiwani wa Ukawa kulianza kuonekana mapema wakati walipojifungia katika kikao chao cha ndani saa chache baada ya kumalizika kikao cha Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambavyo vyote vilifanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. 

Inaelezwa kuwa kutofautiana huko kulichochewa na msimamo wa wajumbe watano wa Ukawa wanaounda Kamati hiyo ya Fedha kupiga kura ya ndio kukubali fedha hizo zitumike.

Katika kamati hiyo ambayo inaundwa na wajumbe 10, watatu wakiwa ni CCM huku saba wakiwa ni Ukawa, hata hivyo wajumbe wawili tu wa Ukawa ndio waliopiga kura kukataa fedha hizo kwa hoja kwamba kuzikubali ni kubariki mchakato ‘tata’ uliotumika kuliuza shirika la UDA.

Taarifa toka ndani ya Kamati hiyo ya Fedha zinaeleza kuwa waliopiga kura ya ndio ni pamoja na Abdalah Chaurembo, Abdalah Mtinika na Mariam Rulida (wote CCM).

Kwa upande wa Ukawa walioungana na CCM kupiga kura ya ndio ni pamoja na Meya Isaya Mwita (Chadema), Diwani Patrick Asenga (Chadema), Leila Madibi (CUF), Mussa Kafana (CUF) na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF).

Kwa mujibu wa taarifa hizo, waliopiga kura za hapani ni Meya wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema) na Meya wa Ilala, Charles Kuyeko (CUF).

Chanzo chetu toka ndani ya kikao hicho cha Ukawa kililidokeza gazeti hili kuwa; wakati wakiwa katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe walitofautiana hoja juu ya kutumika au kutotumika kwa fedha hizo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Meya wa Ubungo, Boniface na Diwani wa Kata ya Tabata, Asenga waliishiwa uvumilivu kiasi cha kukunjana na kutaka kupigana.

MTANZANIA Jumamosi ambalo lilikuwepo nje ya Ukumbi wa Karimjee wakati kikao hicho cha ndani kikifanyika, lilishuhudia Asenga akitolewa nje huku akiwa ameshikiliwa na wajumbe wawili waliokuwa kwenye kikao.

Baada ya Asenga kutolewa, Ofisa Uhusiano wa Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, alisikika akiwaambia wajumbe hao wa Ukawa kuwa wakiendelea na vurugu hizo na kumgusa Meya wa Jiji Mwita, ataita polisi.

Wakati hayo yakitokea waandishi walimfuata Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, kuhoji kilichotokea ambapo alisema: “Hilo sokomoko lote ni fedha za UDA, tulishaamua katika kamati ya fedha lakini sasa kamati za vyama ndio zimekaa tunashangaa wanapigana wenyewe kwa wenyewe…huyo Asenga ametoka au bado yuko ndani…ngoja nikamsaidie atapigwa na Boni (Meya wa Ubungo).”

Muda mfupi baada ya mvutano huo kuibuka kiliketi kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji ambalo kwa kawaida kinajumuisha wajumbe 18 kati yao tisa wakiwa ni madiwani kutoka halmashauri tatu za Jiji, mameya watatu kutoka halmashauri tatu, wabunge watano kutoka kwenye baadhi ya majimbo ya jiji na Meya wa Jiji.

Jana waliohudhuria kikao hicho ambacho kilitawaliwa na mvutano mkali ni wajumbe 12 tu ambao walilazimika kupiga kura ya wazi kuamua mustakabali wa fedha hizo.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Meya wa Jiji, Mwita na ambacho waandishi wa habari waliruhusiwa kuingia wajumbe 11 ndio waliopiga kura.

Kati ya waliopiga kura kwa awamu ya kwanza, CCM walikuwa sita Ukawa watano.

Mkurugenzi wa Jiji, Sipora alitangaza matokeo ambapo waliokubali fedha zitumike walikuwa sita huku waliokataa wakiwa watano.

Baada ya matokeo hayo, Ofisa Utumishi wa Jiji alimtaka Meya wa Jiji, Mwita kupiga kura ya turufu ili ihesabiwe na zile za wajumbe wengine.

Meya kura yake iliungana na waliokataa fedha hizo kutumika na kufanya matokeo kuwa sita kwa sita hivyo kushindwa kufikia mwafaka.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwita alisema watamwomba Rais Dk. Magufuli awaongezee muda ili wapate nafasi ya kujipanga zaidi.

“Baraza linapofanyika lazima wabunge wawepo tumehitisha baraza lakini hawakutokea tukakubaliana tupige kura ili tuweze kufanya maamuzi zaidi, waliosema fedha zisitumike kwa sasa wameshinda. Nafikiri Rais kwa busara yake ataangalia lakini sisi bado tulikuwa tunataka tujipe muda ili tuone athari ya kuzitumia fedha hizi ama kutozitumia,” alisema.

KAULI YA ASENGA

Baada ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji kumalizika, MTANZANIA Jumamosi lilimfuata Asenga na kumuuliza juu ya taarifa za kuzuka ugomvi kati yake na Meya Jacob ambapo alijibu kwa kifupi: “Hayo ni masuala mengine binafsi ambayo hayahusiani na hiki kilichotuleta hapa.”

Naye Meya Jacob alisema: “Ni mihemko ya kisiasa tu mmoja anasema ndiyo na mwingine anasema hapana. Kule kulikuwa ni kulaumiana kwa kelele tu lakini si kwamba kulikuwa na vurugu…bila ubishani ule lile suala lingepita.”

Alipoulizwa Meya wa Jiji kuhusiana na vurugu hizo alikiri wajumbe hao wa Ukawa kutofautiana.

 

 “Ni kweli wajumbe walitofautiana, mjumbe mmoja alimrushi…alimsema vibaya mwenzake, alikuwa ni Asenga walitofautiana na Jacob kwahiyo wakataka ku…si jambo baya sana walirushiana maneno lakini tunashukuru niliwaambia watulie na tukayaweka vizuri mambo na kuendelea na kikao,” alisema.

Mvutano kwenye baraza

Kikao cha baraza kilianza saa 7:56 mchana ambapo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Liana, alisema ajenda ilikuwa ni mapendekezo ya kutumia fedha za mauzo ya hisa za Halmashauri ya Jiji zilizokuwa UDA.

Baada ya kutoa utangulizi huo, Meya wa Jiji, Mwita aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, aliruhusu madiwani kuchangia ambapo mchangiaji wa kwanza alikuwa ni Diwani wa Kata ya Kibonde Maji, Abdallah Mtinika (CCM), aliyeunga mkono fedha hizo kutumika.

 “Mwenyekiti mimi ningeshauri utuhoji tu wajumbe ili tupige kura tufanye maamuzi tukaendelee na shughuli nyingine kwa sababu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishasema tena kwa maandishi hivyo tulihitimishe kwa faida ya wana Dar es Salaam,” alisema Mtinika.

Baada ya kauli hiyo, mwenyekiti wa kikao alimtaka Mkurugenzi wa jiji, Liana, kutoa ufafanuzi na ndipo aliposema katika kikao cha Kamati ya Fedha zilishapigwa kura ambapo wajumbe saba walikubali fedha hizo zitumike kama mapendekezo yalivyo na wawili walikataa na kudai zoezi la uuzwaji UDA lilikuwa batili.

Baada ya kauli hiyo, Meya wa Ubungo, Boniface, aliomba kuchangia na akakataa fedha hizo kutumika akidai hazitoshi kujenga kituo cha mabasi ya mkoani kinachotarajiwa kujengwa Mbezi Luis na kwamba zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 30 kufanya shughuli hiyo.

“Hizo Sh bilioni 5 zitaenda kufanya usafi au kulipa fidia kwa sababu fidia peke yake tunadaiwa Sh bilioni 2.5…tutumie vizuri agizo la Rais tupeleke ujumbe kwa Rais kwamba hatuwezi kuzitumia,” alisema Jacob.

Aliposema hayo, Mwita alisema: “Jacob naomba urudi kwenye ajenda ya msingi, naomba ushawishi baraza hatutaki kujadili watu ambao hawapo hapa.”

Baada ya agizo hilo, Jacob alisema: “Simbachawene (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ni wasaidizi wa rais na wamezungumzia suala hili kama nimewatukana niambie niwaombe radhi, lakini kama sijawatukana naendelea kutoa hoja.

“Mei 2 mwaka jana tulikataa tusizichukue fedha hizi kwa sababu uuzwaji haukuzingatia kanuni na taratibu halafu leo tuje tukubali tena tutaonekana watu wa ajabu, binafsi siwezi kurudia matapishi. Tupige kura na maamuzi ya kikao ndiyo yazingatiwe,” alisema Jacob.

Naye Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge (CCM) alisema: “Majibu yamekuja hatuwezi kuendelea kuvutana, UDA tunayoipinga imeshaanza na mradi umeshazinduliwa, halmashauri zinaongozwa na kanuni, miongozo na maelekezo kutoka juu.

“Mwenye dhamana ametuagiza tukae, tusipoamua yeye anaweza kuamua, sisi tunaosema Sh bilioni 5.8 ni ndogo hatujawahi kuja na mbadala kwamba thamani halisi ni ipi. Jiji limekaa na Mamlaka ya Mapato (TRA) wameshachukua chao, tukiendelea kulumbana tunapoteza muda,” alisema.

Baada ya Mnyonge kutoa kauli hiyo, Mkurugenzi wa Jiji alisimama tena kutoa ufafanuzi na akasema Jiji baada ya kuona hawapati gawio kwenye Uda na wanaendesha mradi huo kwa hasara, walizingatia hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu miradi inayoendeshwa kwa hasara, ndipo baraza likaamua Jiji liuze hisa zake.

Baada ya maelezo hayo, Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdalah Chaurembo alisema: “Meya (Mwita) chama chako kimeshika jiji tunataka ufanye vitu vionekane, umeanza vizuri kwenye makusanyo watu wanaona.

“Kama tumekosea kulingana na misimamo yetu basi tukubaliane tulimalize, tusitafute sehemu ya kujificha tumwogope Mungu…na Boni ukinipiga nakuloga,” alisema Chaurembo ambaye alikuwa ameketi jirani na Meya Boniface.

Siku tano za Magufuli

Januari 25, akizindua awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, Rais Magufuli aliagiza halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha inatoa uamuzi wa matumizi ya Sh bilioni 5.8 zilizotolewa Simon Group kama sehemu ya ununuzi asilimia 51 ya hisa za UDA vinginevyo yeye atawafundisha namna ya kuzitumia.

 “Niwaombe katika fedha hizi asilimia 51 ambazo wameendelea kubishana nazo watoe majibu ndani ya siku tano kwamba ni namna gani watazitumia, wasipofanya hivyo nitamwagiza Waziri wa Tamisemi tuamue kwa niaba yao namna ya kuzitumia vizuri hizi fedha.

“Na ningeomba hizi fedha wasizitumie kwa ajili ya kugawana, hizi fedha zitumiwe kwa ajili ya wana- Dar es Salaam, ikiwezekana ipangwe mikakati ya kuleta maendeleo ili fedha hizi ziweze kuleta reflection (taswira) na si kwa sababu ya kugawana huko. Kwamba tumepata pesa sasa tunagawana na ninamshukuru Simon kwa kulipa hilo deni kwa sababu huo ulikuwa mtego wake na mimi nakuhakikishia umeushinda sasa tuendelee vizuri kwa kuleta maendeleo ya Watanzania,” alisema Rais Dk. Magufuli.

 

Ripoti ya CAG 2014/15

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2014/15, ilikosoa uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), ikisema suala hilo halikuwa na baraka za Serikali na kushauri shirika hilo lirudishwe serikalini hadi mgogoro huo utakapokamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha ripoti yake bungeni Aprili 25 mwaka jana, CAG, Profesa Mussa Assad, alisema ukaguzi umebaini kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa shirika hilo aliwekewa na mwekezaji Sh milioni 320 kwenye akaunti yake binafsi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hisa za Uda zilithaminishwa kwa Sh 744.79 kila hisa Oktoba 2009 na ilivyofika Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa 656.15.

Inasema katika uuzaji huo, bodi ya wakurugenzi ya Uda ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo bila kuwepo na sababu za kufanya hivyo.

“Kwa mujibu wa majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali, Serikali haitambui uuzwaji wa hisa hizo. Kulingana na mkataba wa kuwasilisha hisa wa Februari 11, 2011 mnunuzi (mwekezaji) atalipa jumla ya Sh bilioni 1.14 kama bei ya ununuzi wa hisa zote ambazo zilikuwa hazijagawiwa, ingawa mkataba haukuonyesha akaunti ya benki ambayo malipo yangefanyika.

“Mnunuzi (mwekezaji) alilipa Sh milioni 285 pekee katika akaunti namba 0J1021393700 ya benki ya CRDB inayomilikiwa na UDA. Hakukuwa na malipo mengine ya ziada yaliyofanywa na mwekezaji kuhusiana na ununuzi wa hisa za UDA.

“Mwenyekiti wa Bodi alipokea kiasi cha Sh milioni 320 kupitia akaunti yake binafsi kutoka kwa mwekezaji ambayo kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ilikuwa ni ada ya ushauri alioutoa kwa mwekezaji,” alisema CAG.

Alisema malipo hayo yalizua mgongano wa kimasilahi.

“Ninashauri Shirika la UDA lirudishwe chini ya usimamizi wa Serikali hadi hapo mgogoro huu utakapotatuliwa,” alishauri CAG.

Itakumbukwa sakata la uuzwaji wa UDA lilionekana kuwaunganisha wabunge wa Bunge la 10 wa chama tawala na wale wa upinzani hususani wa Dar es Salaam wote wakipinga uuzwaji wake.

Wabunge hao walidai kuwa shirika hilo liliuzwa kwa bei ya kutupwa inayofikia Sh milioni 280 tofauti na thamani yake halisi.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, aliwahi kuazimia kupeleka hoja binafsi katika Bunge la sasa akidai kuwa kashfa ya UDA ilitokea wakati jiji likiwa chini ya CCM na kwamba katika uongozi wa sasa wa Ukawa watalimaliza.

 “Naliambia Bunge msije mkathubutu, maana nimesikia mara zile Sh bilioni 5 alizolipa Simon Group zipangiwe matumizi, naomba niwaambie sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu, sasa kama hatujitambui na Serikali inataka kuingilia, hatuwezi kutumia hii shilingi bilioni 5 kuhalalisha haramu kuwa kitu kitakatifu,” alisema Mdee.

UDA ilianzishwa mwaka 1974 na Serikali ilikuwa na hisa 100, mwaka 1985 Serikali iligawa hisa zake asilimia 51 Jiji na yenyewe ikabaki na 49, hisa jumla ilikuwa milioni 15 katika hizo milioni 15, hisa milioni 7.5 ndiyo zilikuwa zimelipiwa, hisa nyingine milioni 7.8 zilikuwa hazijalipiwa, kwa hiyo Serikali ilivyogawa hisa, Jiji lilipata milioni 3.3 na Serikali ikabaki na milioni 3.4.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles