Na JUDITH NYANGE
MKUU wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mary Tesha, amewasihi wanawake wote wanaojifungua kunyonyesha watoto wao kwa miezi sita bila kuchanganya na kitu kingine chochote.
Alisema hiyo ni kwa sababu maziwa ya mama yana virutubisho muhimu kwa ukuaji wa watoto wao.
Alikuwa akizungumza jana wakati wa hafla ya kupokea msaada wa katoni mbili za maziwa kwa ajili ya watoto wanaoshindwa kunyonya kutokana na matatizo mbalimbali.
Msaada huo ulitolewa na Kampuni ya Twincity katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.
Alisema maziwa ya mama yana virutubisho vya vitamin, calcium na vingine vingi ambavyo vinasaidia katika ukuaji wa motto.
DC alisema ndiyo maana wataalamu wa afya wanashauri motto anyonyeshwe mpaka atakapotimiza miezi sita bila kulishwa kitu kingine kama mama hana tatizo lolote la afya.
“Wapo baadhi ya wazazi ambao wanajifungua na kuogopa kunyonyesha kwa kuhofia maziwa yao kulala na kuanza kuwapa watoto wao maziwa ya ng’ombe.
Maziwa ya ng’ombe ni rahisi kuwa na vijidudu vinavyoweza kusababisha magonjwa mbalimbali na kumfanya mtoto kudhoofu kwa kukosa lishe bora.
“Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Save the Children, watoto 300 chini ya umri wa miaka mitano hufariki dunia kila siku kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa lishe na asilimia 42 hudumaa kutokana na tatizo hilo,”alisema Tesha.
Alisema inasikitisha kuona mtoto ambaye anabaki baada ya mama yake kufariki dunia wakati wa kujifungua anakua kwa kukosa lishe ambayo angeipata kwa kunyonya maziwa ya mama yake.
Tesha alisema changamoto za upungufu wa lishe husababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo watoto kuzaliwa na tatizo la mdomo sungura, kujifungua kwa upasuaji na wazazi kufariki dunia baada ya kujifungua na hivyo watoto wao kushindwa kunyonya vizuri.
Matatizo mengine ni mama kukosa maziwa, kuugua muda mrefu na hivyo kulazimika kuwaacha watoto wao nyumbani kwa kuepusha kupata maradhi yanayotokana na mazingira ya hospitali na kusababisha kukosa maziwa ya mama na kupata matatizo ya ukosefu wa lishe.
Aliwataka wazazi wanaopatiwa maziwa hayo wayatumie kama ilivyokusudiwa kwa sababu wapo baadhi wanahisi wana mahitaji zaidi ya maziwa na hivyo kuyauza ili watatue matatizo mengine yanayowakabili.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Twincity, Nina Kimaro, alisema maziwa hayo yana virutubisho vyote muhini na ni kwa ajili ya watoto kutoka kuzaliwa mpaka mwaka mmoja ambao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo kupoteza wazazi au kuzaliwa na tatizo la mdomo sungura na hivyo kushindwa kunyonya maziwa ya mama zao.
Mmoja wa waliopatiwa msaada huo, Ester Kasela, alishukuru kwa msaada huo pamoja na Serikali kwa kuendelea kujali afya ya mama na mtoto na kuendelea kuwaboreshea huduma zao katika vituo vya afya , zahanati na hospitali zote nchini ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Sekou Toure ile ya zamani siyo ya leo…huduma nilizoziona zinatolewa leo hapa mimi kama mzazi naushukuru uongozi na wauguzi.
“Tangu nimefika hapa nakaribia kumaliza wiki lakini sijamuona mzazi au mtoto aliyefariki, hii inaonyesha jinsi wauguzi wanavyojali afya ya mama na mtoto,” alisema Kasela.