24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

DC AAGIZA MAOFISA WANNE WAKAMATWE

Na Pak Mwillongo-Bagamoyo


 

alhaji-majid-mwangaMKUU wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Alhaji Majid Mwanga ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa Ofisa Ardhi wa wilaya hiyo, Patrick Tsetse na wenyeviti watatu wa vitongoji kwa tuhuma za ufisadi.

Maofisa hao wanatuhumiwa kufanya hayo katika fedha za malipo ya fidia kwa wakazi wa Kijiji cha Pande wilayani humo wanaotakiwa kupisha ujenzi wa bandari.

Akizungumza na wakazi wa Mlingotini na Pande wilayani humo, Mwanga alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kukamilika uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola kufuatiwa kuwapo kwa malalamiko ya wakazi wa maeneo hayo kuhusu kupunjwa malipo wakati wa ulipwaji wa fidia.

“Baada ya uchunguzi wa Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama tumebaini kuwapo ufisadi mkubwa katika suala zima la ulipwaji wa fidia kwa wakazi wa Pande na Mlingotini.

“Uchunguzi huo umebaini kuwa hawa wenyeviti wenu wa vitongoji wameshiriki kwa namna moja au nyingne katika kufanya ufisadi huo kwa kushirikiana na aliyekuwa Mthamini wa mradi, Patrick Tsetse.

“Nakuagiza OCD awachukue hawa wakaisaidie polisi katika uchunguzi na kuanzia leo si wenyeviti chagueni watu wengine watakaojaza nafasi,” alisema.

Alisema tume iliyoundwa ilibaini kuwapo madudu mengi ikiwamo baadhi ya wananchi waliolipwa fidia kutumia picha za uongo za majengo na kupiga picha katika maeneo yasiyo yao  kuweza kujipatia fedha.

“Kwa ujumla hamuwezi amini kuna watu 11 wamelipwa   Sh milioni tisa kufidiwa mazao katika shamba ambalo si lao kitu ambacho kinaacha maswali mengi bila majibu juu ya uhakika wa watu waliofanya tathmini katika mchakato huo.

“Kuna mtu amelipwa Sh milioni 120 wakati hana hata eneo kwa hivyo kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe,”alisema Mwanga.

Akizungumzia kuhusiana na tathmini  ya pili inayotarajiwa kufanyika tena, Mwanga alisema inatarajiwa kuanza leo.

Hivyo aliwataka wakazi wote wa Pande kujitokeza   kufanyiwa tathmini upya.
Alisema Serikali ipo tayari kupima na kujenga miundombinu katika eneo hilo na kuwakabidhi wakazi wa Pande na Mlingotini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles