Na Crispin Gerald – DAWASA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa salamu za Krismasi kwa wateja wake na kuwahakikishia upatikanaji wa maji wa hali ya juu msimu huu wa sikukuu.
Upatikanaji wa huduma ya maji unatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Mamlaka ya kuhakikisha huduma ya maji inaimarika kwa wateja wote.
Mkurugenzi wa Biashara DAWASA, Ritamary Lwabulinda, amesema kuwa kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, wateja wasiwe na wasiwasi juu ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa kuwa Mamlaka imefanya maboresho makubwa ya kuhakikisha huduma ya majisafi inapatikana kwa ubora wa hali ya juu.
“Huduma ya majisafi imeendelea kuimarika kwenye eneo la huduma la DAWASA kutokana na nguvu kubwa iliyowekwa kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji iliyowezesha kuimarika kwa huduma.
“Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji Pugu – Gongo la Mboto unaohudumia wakazi takribani 450,000, mradi wa maji Jet – Buza unaohudumia wakazi wapatao 173,810, mradi wa maji Mkuranga unaohudumia wakazi 25,000.
“Mradi wa usambazaji maji kutoka Bagamoyo mpaka Chuo Kikuu Ardhi unaohudumia zaidi ya wakazi 60,000, miradi hii mikubwa na midogo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma kwa wateja,” amesema Ritamary.
Ameongeza kuwa kwa mwaka ujao, Mamlaka inatarajia kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mengi, kwani kazi ya kukamalisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya majisafi itakayoongeza wigo wa huduma ya maji inaendelea kwa kasi.
“Maeneo ambayo kwa sasa yanapata maji kwa mgao, yatasahau tabu hiyo na yataanza kupata maji kwa saa zote,” ameeleza Ritamary.
Mkurugenzi Ritamary amesema kuwa katika msimu wa sikukuu huduma na vituo vya huduma DAWASA zitaendelea kuwa wazi na kwa wakati wote ili wateja waweze kufanya malipo ili kupata huduma.