22.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 30, 2024

Contact us: [email protected]

DAWASA yapeleka matumaini mapya Msumi

*Uchimbaji wa visima virefu kama mpango wa awali waanza kutekelezwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza kazi ya uchimbaji visima katika eneo la Mbezi- Msumi Kata ya Mbezi ikiwa ni maagizo ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew (Mb) katika ziara yake aliyoifanya mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Ubungo hivi karibuni.

Katika ziara hiyo, Kundo aliwaeleza wananchi wa Msumi kuwa Serikali kupitia DAWASA imeandaa mkakati wa mda mrefu ambapo kwa kutenga kiasi cha Bilioni 18 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa utakaohusisha ujenzi wa tenki kubwa na ulazaji wa mabomba na mkakati wa muda mfupi wa kuchimba visima virefu ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa majisafi kwenye eneo hilo lenye wakazi takribani 144,000.

Akizungumza utekelezaji wa maagizo hayo Juni 26, 2024, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro, amesema hatua hii ni hatua ya mwanzo ya kuhakikisha eneo la Msumi linapata huduma kwani hapo awali eneo hilo halikuwa na mtandao wa maji kutoka DAWASA na hivyo wananchi kutegemea maji kutoka kwenye visima vya watoa huduma binafsi.

“Tupo hapa kujionea utekelezaji wa mkakati wa muda mfupi wa uchimbaji wa visima ambayo vitaenda kupunguza makali ya adha ya ukosefu wa maji katika eneo hili. Utofauti wa visima hivi tunavyochimba DAWASA na vile vya Wananchi ni kuwa visima vyetu ni virefu vyenye urefu kuanzia mita 170 kwenda chini na utaenda sambamba na ujenzi wa vizimba kwenye mitaa ili kusogeza huduma kwa wananchi,” amesema Lyaro.

Nae, Mwenyekiti wa Mtaa wa Msumi, Ismail Mbinda, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona hali ya eneo la Msumi na kutatua changamoto hii iliyodumu kwa mda mrefu.

“Kwa kweli tutakua wachoyo wa fadhila kama tusiposhukuru kwa hili, Serikali yetu tunaishukuru sana jitihada zinaonekana na hawa watu wa DAWASA wametupa ushirikiano mno tunaomba hili zoezi likamilike kwa muda ili watu wapate maji tukisubiri mradi mkubwa,” amesema Mbinda.

Naye, Mkazi wa Msumi Center, Nasma Abdallah amesema wanaishukuru Serikali na DAWASA kwa jitihada hizi kwani ukosefu wa maji ulisababisha kutumia mda mrefu na kwenda umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya maji ambayo bado hayakuwa salama na ya kutosheleza.

Utekelezaji wa mikakati ya kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika eneo la Msumi ni moja ya malengo ya Mamlaka ya kufikisha huduma kwa wote ifikapo 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles