28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Gas yazindua mpango wa punguzo la bei ya mitungi ya gesi kwa wanafunzi vyuo vikuu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kampuni ya kuuza nishati ya gesi ya kupikia majumbani ya Taifa Gas Limited imezindua mpango wake maalum unaotoa punguzo la bei ya nishati hiyo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kampuni hiyo kufanikisha adhma ya serikali inayolenga kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule (mbele katikati) akiwa kwenye picha pamoja na wawakilishi wa wanafunzi na uongozi wa vyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Takwimu, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Maji na wananchi wa eneo la Changanyikeni, Wilaya ya Kinondoni wakati wa hafla hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa program hiyo ilifanyika jana eneo la Changanyikeni, Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiambatana na uzinduzi wa duka maalum litakalowahudumia wanafunzi hao kwa punguzo hilo la bei. Kuashiria uzinduzi huo jumla ya mitungi ya gesi 300 ilitolewa bure kwa baadhi ya wanafunzi hao na wakazi wa maeneo jirani ili kuchochea hamasa ya mpango huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule aliongoza hafla hiyo iliyohudhiriwa na wawakilishi wa wanafunzi na uongozi wa vyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Takwimu, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Maji. Meneja Mauzo wa Taifa Gas, Joseph Nzumbi alimuwakilisha Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius kwenye uzinduzi huo.

Baadhi ya wawakilishi wa wanafunzi na uongozi wa vyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Takwimu, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Maji na wananchi wa eneo la Changanyikeni, Wilaya ya Kinondoni wakati wa hafla hiyo wakifuatilia uzinduzi wa mpango wa punguzo la bei ya nishati ya gesi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam wa Kampuni ya kuuza nishati ya gesi ya kupikia majumbani ya Taifa Gas Limited maalum ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kampuni hiyo kufanikisha adhma ya serikali inayolenga kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huduma hiyo, DC Mtambule alisema huduma hiyo imekuja wakati muafaka kipindi ambacho serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan inapambana kuhakikisha inafanya kila liwezekanalo kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kupitia makundi yao mbalimbali kuifikia nishati hiyo kwa urahisi.

“Ni faraja kubwa zaidi kwetu kama serikali kuona kwamba wakati tunaendelea kufanikisha mkakati wa kufikia nishati safi ifikapo 2034 tayari wadau kama Taifa Gas wameanza kubuni mbinu mbalimbali za kijamii na kimasoko zitakazotusaidia kama taifa kufanikisha adhma hiyo. Kupitia huduma hii ya punguzo la bei kwenye kila mtungi wa gesi wanafunzi wa vyuo vikuu watavutiwa zaidi na kuona matumizi ya gesi kama suluhisho sahihi la nishati ya kupikia…hongereni sana Taifa Gas,’’ alipongeza.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule (wan ne kulia) akikabidhi moja kati ya mitungi ya gesi 300 iliyotolewa bure na Kampuni ya kuuza nishati ya gesi ya kupikia majumbani ya Taifa Gas Limited kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam na wakazi wa eneo Changanyikeni wilayani Kinondoni ili kuchochea hamasa ya mpango wa punguzo la bei ya nishati ya gesi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam wa kampuni hiyo ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake katika kufanikisha adhma ya serikali inayolenga kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034. Wanaoshuhudia ni pamoja na wawakilishi wa wanafunzi na uongozi wa vyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini humo na maofisa wa Taifa Gas Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika jana jijini Dar es Salaam.

Awali akifafanua kuhusu mpango huo, Nzumbi alisema unahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam wenye vitambulisho halali ambao watapata mapunguzo tofauti kulingana na uzito wa mitungi ya gesi watakayonunua.

“Kwa mfano bei ya kujaza mtungi wa gesi wenye uzito wa kg 6 badala ya wanafunzi kuuziwa kwa Tsh 23,000 kupitia mpango huu watauziwa kwa Tsh 20,000 na kwenye mtungi wenye uzito wa kg 15 wanafunzi watajaziwa gesi kwa Tsh 50,000 badala ya Tsh 55,000. Tumeanza na Dar es Salaam na tutaendelea kwenye vyuo vingine zaidi maeneo mengine,’’ alitaja.

Zaidi, akiwasilisha salamu za Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius, Nzumbi alisema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba kila Mtanzania mwenye nia ya kutumia nishati safi ya gesi anapata fursa hiyo kupitia mikakati mbalimbali inayoendelea kubuniwa na kampuni hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya makundi tofauti ya kijamii.

Wakizungumzia program hiyo, wadau na wanufaika wakiwemo wakiwemo wakuu wa vitivo, wawakilishi wa wanafunzi na wakazi wa eneo la Changanyikeni waliipongeza wakibainisha kuwa itaongeza chachu kwa wanafunzi hao kutumia zaidi nishati ya gesi badala ya mkaa kutokana na punguzo bei ambalo ndio kiini cha mpango huo.

“Wanafunzi ni kundi ambalo bado halijaanza kujitengenezea kipato chao wao wenyewe hivyo wapo makini sana na masuala ya bei ya bidhaa wanazotumia hususani kwa wale wanaojipikia kwenye maeneo yao. Ujio wa mpango huu wa punguzo la bei ya mitungi ya Taifa Gas utakuwa kimbilio kwao ili waweze kuokoa fedha zao. Nawaomba sana wanafunzi waichangamkie huduma hii,’’ alisisitiza Wenslaus Richard, Mkuu wa Kitivo Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kauli iliyoungwa mkono na wanafunzi hao.

Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitungi hiyo kwa wanufaika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles