27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dar yazama

mvuamvua 2Jonas Mushi na Hadia Hamisi, Dar es Salaam
MVUA kubwa iliyonyesha tangu juzi imesababisha maafa makubwa katika Jiji la Dar es Salaam, huku watu wawili wakipoteza maisha baada ya kuzidiwa na maji katika maeneo tofauti jana.
Mbali ya vifo hivyo, wakazi wengi wa jiji hilo wameachwa bila makazi kutokana na nyumba zao kujaa maji.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema mvua hiyo imesababisha kifo cha mtu mmoja katika eneo la Mto Ng’ombe uliopo Manzese.
Alimtaja mtu huyo kuwa ni Said Idd (73) ambaye maiti yake ilionekana jana ikiwa inaelea kwenye mto huo.
Alisema alilazimika kutangaza baadhi ya barabara kufungwa kutokana na wingi wa maji, ili kunusuru maisha ya watu na mali zao.
“Hali ya mvua katika Jiji la Dar es Salaam ni mbaya, nimeagiza baadhi ya barabara zifungwe ili kunusuru maisha ya watu,”alisema Kamanda Kova.
Baada ya tangazo hilo, polisi walilazimika kufunga barabara ya Jangwani ambako daraja kubwa lililojengwa hivi karibuni, lilikuwa limefunikwa na maji.
Licha ya kufunga eneo hilo, Kova aliwataka wakazi wa jiji amba wako katikati ya mji kuondoka mapema na wale walioko eneo la Kariakoo kutumia barabara ya Umoja wa Mataifa.
Alisema maeneo ambayo yalionekana kuwa hatari zaidi ni Kinondoni, Kariakoo, Jangwani, Muhimbili, Upanga na Posta.
“Kama mtu anataka kupita maeneo haya au kwenda kufanya shughuli yoyote asiende,”alisema Kamanda Kova.
Alisema katika eneo la bonde la Kinondoni Mkwajuni, polisi walilazimika kuokoa watu ambao walikuwa wamezingirwa na maji ndani ya nyumba zao.

DIWANI
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makumbusho wilayani Kinondoni, Haroub Ally aliiambia MTANZANIA kuwa katika eneo lake mtu mmoja alipoteza maisha.
Alisema tukio hilo, lilitokea katika Mtaa wa Mbuyuni ambako, Masumbuko Deoglas (45) ambaye nyumba yake ilijaa maji alifariki dunia kutokana na maji kumzidi nguvu.
Karibu barabara zote zenye daraja kubwa zinazounganisha maeneo ya kuingia katikati ya jiji na pembezoni zilifunikwa na maji.
Kutokana na hali hiyo, maeneo hayo yalikuwa na msongamano mkubwa wa magari barabarani.
ENEO LA JANGWANI
Eneo hilo limekuwa hatarini kila mvua inaponyesha, huku nyumba nyingi zikiwa katika hali mbaya.
Mitaa ya Jangasua, Jangwani Minazini, Upanga Magharibi, Mgomeni Suna na Dosi hali ilikuwa mbaya huku baadhi ya nyumba zikifunikwa kabisa na maji.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dosi, Ally Bachu alisema baadhi ya wananchi walikwama kwenye makazi yao kutokana na maji.
Alisema baada ya hali hiyo, wananchi walilazimika kuokolewa kwa kutumia katapila ambako kwa kawaida huonekana katika shughuli za ujenzi wa barabara.
Katika eneo la Afrika Sana lililopo barabara ya Shekilango wilayani Kinondoni, soko lilizingirwa na maji kutokana na kuziba kwa mitaro na maji kuelekea eneo la Bamaga katika makutano ya barabara hiyo na ile ya Ali Hasani Mwinyi.
Daraja maarufu la Salender, Kawe, Bunju na Mlalakuwa maji yalikuwa yakipita juu kiasi cha kuhatarisha maisha ya watumiaji.
Pia barabara za Mwai Kibaki, Msasani kwa Mwalimu Nyerere, MayFair, Legho barabara ya Sinza hayakupitika kwa zaidi ya saa sita.
MBEZI
Katika hali ya kushangaza, wakazi wa eneo la Mbezi Maramba Mawili walilazimika kuvunja ukuta wa mkazi mwenzao Christopher Kaswalala uliojengwa katika mkondo wa maji, ili kuruhusu maji yapite.
Ukuta huo unadaiwa ulikuwa chanzo kikubwa cha kukwamisha maji ambayo yangeweza kuhatarisha maisha ya watu, ambapo zaidi ya nyumba kumi zilijaa maji.
Amri ya kuvunja ukuta huo ilitolewa na Mwenyekiti wa mtaa huo, Mohamed Kilwa.
“Wakati anajenga ukuta huo tulimpa onyo, alipuuza na kuendela kujenga sasa ninaamuru ukuta uvunjwe ili maji yapite kwenye mkondo wake kama ilivyokuwa awali,” alisema Kilwa.
Katika eneo la Kwembe hali ilikuwa mbaya zaidi ambako zaidi ya magari 20, yaliyokuwa yameegeshwe yalijikuta yakisombwa na maji.
MTANZANIA ilishuhudia walimiliki wa magari hayo wakihaha namna ya kuyanasua.
VITUO VYA MABASI
Baada ya wananchi wengi katika eneo la Jwangani kuonekana hawana makazi kwa muda, walilazimika kujikusanya katika vibanda vilivyojengwa maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi.
Katika vibanda hivyo, MTANZANIA lilishuhudia akina mama wakiwa na watoto, vijana na wazee wakiwa wameweka magodoro yao.
Mmoja wa wakazi waliokutwa katika eneo hilo, Rukia Mohamed alisema. “Haya ndiyo yamekuwa makazi yetu ambayo kama unavyoona hakuna chakula, wala huduma zingine kama vile vyoo,” alisema.
Hadi saa saba mchana, wakazi hao walikuwa hawajapata msaada wowote kutoka katika mamlaka husika.
Naye Mariam Pazia, alisema wameamua kufanya makazi katika eneo hilo la kituo cha basi wakiwa na godoro, kwa sababu vitu vingine vimesombwa na maji.
“Nilifanikiwa kutoka na godoro ndani na watoto wangu wawili tena wadogo…sikupata msaada wa kuhama kabla maji hayajaingia,” alisema Pazia.
TABATA
Katika eneo la Tabata Kimanga eneo la Bonde la Mchicha karibu mazao yote yalikuwa yamefunikwa na maji.
Bonde hilo linalounganisha barabara ya Ubungo External, Kimanga na Kisukuru hadi Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Barabara hiyo, inayotengenezwa kwa kiwango cha lami ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Segerea, Kinyerezi, Ukonga na Majumbasita.
Hadi jana, barabara hiyo ilikuwa haipitiki kutokana na kipande kinachoingia Kisukuru kuharibiwa vibaya na maji.
WANANCHI WAANDAMANA
Habari kutoka mtaa wa Temeke Wailes, zinasema wananchi wa Kata ya Miburani waliandamana kwenda ofisi za serikali ya mtaa wao kuhoji matumizi ya fedha walizochangishwa kwa ajili ya kutengeneza mitaro ya maji machafu.
Mkazi wa mtaa huo, Andrew Richard aliliambaia MTANZANIA kuwa wananchi walifanya uamuzi huo baada ya makazi yao kujaa maji, licha ya kuchangishwa fedha ambazo alidai zimeishia mikononi mwa wajanja, huku hakuna kazi yoyote iliyofanyika.
“Kila mwananchi alichangishwa Sh 40,000 kutengeneza mitaro ili mvua ikinyesha maji yasiingie kwenye makazi, lakini hakuna mitaro iliyotengenezwa na hivi sasa maji yamejaa kwenye makazi yetu,” alisema Richard.
HALI YA HEWA
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi alisema mvua za masika zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kukatika mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema ndani ya msimu huu, kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua nyingi. “Mfano mvua zilizonyesha Zanzibar zimenyesha kwa muda mfupi, lakini kwa wingi hadi kuleta mafuriko.

ZANZIBAR
Habari kutoka Zanzibar, zinasema mji wa Unguja jana nao ulikumbwa na mafuriko makubwa.
Hali hiyo, ilisababisha shughuli nyingi kusimama, huku mamlaka zinazohusika zikiwaasa waanchi kuchukua hadhari.
Kutokana na hali hiyo, boti za kampuni mbalimbali ambazo kwa kawaida hufanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Zanzibar zilizuiwa kutokana na bahari kuchafuka.
Boti ambazo zilipangwa kuondoka jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar jana saa mbili asubuhi, hazikuondoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles