NEW YORK MAREKANI
TAJIRI namba moja barani Afrika, Aliko Dangote, yupo katika mipango ya kuinunua klabu ya Arsenal ya England katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Kwa mujibu wa orodha ya watu tajiri duniani iliyotolewa Jumatano iliyopita na televisheni ya Bloomberg ya jijini New York, Dangote ambaye ni raia wa Nigeria utajiri wake una thamani ya dola za Marekani bilioni 10.9.
Siku hiyo tajiri huyo aliweka wazi nia yake ya kuinunua klabu hiyo tangu mwaka uliopita.
Mnigeria huyo alisema anasubiri biashara zake kuimarika pamoja na uwekezaji wake wa ujenzi wa bomba la gesi na kiwanda cha kusafisha mafuta kabla ya kuinunua klabu hiyo.
“Hakuna tatizo la fedha, nitainunua klabu hiyo pengine miaka mitatu au minne, tatizo ni kwamba tuna changamoto nyingi ambazo natakiwa kukabiliana nazo kwa sasa lakini baadaye nitaangalia suala la ununuzi huo,” alisema Dangote akiwa katika mahojiano na televisheni ya Bloomberg jijini New York, Marekani.
Dangote ambaye ni shabiki mkubwa wa Arsenal, amepoteza kiasi cha dola bilioni 4.4 mwaka huu kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha ya Nigeria.
Utajiri wake mwingi upo katika kiwanda cha saruji kilichopo mjini Lagos.
Endapo tajiri huyo atainunua timu hiyo atakuwa mtu wa kwanza kutoka Afrika kumiliki timu iliyopo katika Ligi Kuu England.
“Tatizo si kuinunua klabu ya Arsenal na kuendeleza yaliyopo badala yake ni kufanya mabadiliko ndani ya klabu hiyo.
“Nimekuwa na mafanikio makubwa katika biashara na nafikiri naweza pia kuendesha klabu hiyo kwa mafanikio makubwa,” alisema Dangote.
Klabu ya Arsenal imeshinda ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13 huku wakijivunia 2004 kuwa mwaka bora zaidi katika klabu hiyo.