28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CUF waomba tamko la JPM mikutano ya hadhara

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemwomba Rais Dk. John Magufuli kutoa tamko kuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ya kisiasa kama alivyoahidi wakati alipoizuia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Salvatory Magafu, alisema wakati Dk. Magufuli alipopiga marufuku mikutano hiyo, aliahidi kuiruhusu muda wa uchaguzi.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu kwa nchi hii, hivyo ni muda mwafaka wa kuruhusu mikutano ya hadhara kuanzia muda huu wa kujiandikisha wapigakura.

“Tunalitaka Jeshi la Polisi liache kukiuka sheria na lifanye kazi bila ubaguzi wala upendeleo ili kuendelea kulinda amani ya nchi,” alisema.

Magafu alisema hivi karibuni baadhi ya viongozi wa CUF wakiwa wilaya za Liwale, Newala mkoani Lindi, Lushoto na Handeni mkoani Tanga walizuiwa kufanya mikutano ya ndani kwa kuvunjwa, na viongozi wao kuwekwa chini ya ulinzi kwa saa kadhaa.

Alisema licha ya kuzuiwa kufanya mikutano hiyo, hivi karibuni baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wamenukuliwa wakisema hawana taarifa ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilisikika ikisisitiza kutopata taarifa hiyo rasmi kutoka chama chochote. Kwa kuzingatia kauli hii ya ofisi ya msajili, chama kiliamua kufanya mkutano wa hadhara Vingunguti Relini leo (jana) Agosti 3 na kiliandika barua Julai 29 kwa Kamanda wa Polisi Buguruni kuomba kibali cha kufanya mkutano huo.

“Barua hiyo yenye kumbukumbu namba Cuf/W/IL/VOL36/2019 ilinakiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala.

“Jana (juzi) Ijuma saa 11:20 jioni tulipokea barua yenye kumbukumbu namba BUG/SO.7/2/A/VOL.II/191 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Buguruni iliyozuia mkutano wetu kwa madai kuwa kuna zuio la Serikali kufanya mikutano ya hadhara. Maelezo ya barua hii ya zuio yanapingana na kile ambacho ofisi ya msajili imekitamka hivi karibuni,” alisema Magafu.

Aidha Magafu alidai kuwa chama hicho kinajiandaa kuiandikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa barua kuhusu kuzuiwa kwa mikutano yao ya ndani na ile ya hadhara.

Aliongeza kuwa kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kama mlezi wa vyama kudai kuwa hajapokea taarifa rasmi kutoka chama chochote kuhusu kuzuiwa kufanya mikutano hiyo ilihali haoni vyama hivyo vikifanya kazi yake ya kisheria, basi hapaswi kuendelea kuwapo ofisini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles