27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Corona; Wananchi wanavyoishi kwenye ‘mstari’ wa kifo Dar

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

UNAPOINGIA katika eneo la kusubiria feri eneo la Kigamboni Feri Dar es Salaam utasikia ujumbe kwenye spika takribani nne zilizopo hapo ikiwa ni kukukumbusha kuhusu tahadhari ya ugonjwa wa corona.

Ujumbe unaosikika kwenye spika hizo ndogo ni kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ambao unasisistiza tena kwa sauti kali ikisema kuwa: “Narudia tena sasa sio hiari kwa mtu anayeingia kwenye gari, kivuko, kwenye mwendokasi kuvaa barakoa sio hiari tena, ni moja ya sharti,” inasikika sauti hiyo.

Sauti hiyo ya Makalla ambayo ailiitoa Agosti 2, mwaka huu inaendelea kuhimiza kuwa: “Nimefanya uchunguzi, unaenda kwenye kivuko feri mtu anaingia na barakoa kwa sababu tu kuna usimamizi, akifika ndani anaivua na anapotaka kutoka anaivaa, unapovaa barakoa unajikinga wewe na mwenzako.

“Niwatake wasimamizi watu wote wanaohusika na vyombo vya usafiri kuwe na abiria waliokaa tu, unavaa barakoa kwa usalama wako sio wa kuniridhisha mimi Mkuu wa mkoa, kinga ni bora kuliko tiba,” anasisitiza Makalla kwenye tangazo hilo.

Wakati ujumbe huo ukiendelea kupenya taratibu kwenye masikio ya abiria wanaokatiza huku na kule kwa ajili ya kuwahi kupata nafasi kwenye panton; askari wa getini naye anapigilia msumari kwenye jambo hilo hilo.

“…Nyie…wewe vaa barakoa kuna hatari huko, unaingia kwenye hatari. Wewe mama vaa barakoa usituletee balaa,” anasikika Askari huyo huku wengi wakimpa kisogo kwa kudhani kuwa wanamkomoa.

Hiyo ndiyo picha ya haraka kwenye eneo hilo linalotumika na abiria kusubiria kivuko mara baada ya kukata tiketi.

Kwenye pantoni nako hali siyo shwari, kwani wananchi wengi wanaokatiza huku na kule wanavua barakoa mara tu baada ya kuwa wamekanyaga mguu wao kwenye kivuko hicho cha Kigamboni.

Wafanya biashara wa pipi na karanga ndani ya vivuko hivyo ni miongoni mwa makundi machache ambayo yameamua kuchagua fedha dhidi ya kifo. Kwani hakuna tahadhari zozote wanazochukua.

Kwani wakati kivuko cha MV Magogoni kikiendelea kukata mawimbi kwa ajili ya kusaka upande wa pili wa Dar es Salaam (Kigamboni) nao wanakisindikiza kwa miruzi na sauti nzuri za kuita wajeta.

“…pata pipi hapa…, kamata big G hii kwa afya yako …kinywa kitanuka usipochangamsha meno…,” wanasikika vijana hao ambao wengine kwa muonekano wao walipaswa kuwa shule.

Kumbuka kuwa wakati wa zoezi lote hili la ufanyaji biashara ya pipi na karanga hakuna hata mmoja aliyevaa barakoa licha ya kupokea fedha kutoka kwenye mikono ya watu mbalimbali ambao nyendo zao za usalama hazijulikani.

Abiria nao kwa maana ya waliosimama chini na juu ya kivuko nao hawana habari juu ya usalama wao kwani wako “bize” kuangalia madhari nzuri ya Dar es Salaam na mawimbi ya maji yanavyopanda na kushuka.

Ukiwa ndani ya kivuko hicho utaona wengine wakiendelea kuchokonoa vipande vya nyama vilivyokwama kwenye meno kwa kutumia vijiti vyao, sasa ujiulize anafanya hivyo akiwa amevaa barakoa au la.

Wanafunzi nao wakati wakirejea nyumbani kutoka katika shule zilizoko katikati ya Jiji wanaendelea kufukuzana huku na kule ndani ya kivuko hicho cha magogoni huku wakicheka kwa furaha.

Jambo la kusikitisha ni kwamba hakuna hata mmoja anayeshtuka kuwakumbusha juu ya usalama wao kwa kujikinga kwa kuvaa barakoa.

Kwani licha ya wazazi ambao wanaonekana kama wangekuwa ni msaada kwa watoto hao, hakuna hata mmoja anayewakumbusha kuvaa barakoa ikiwamo kutulia na kutogusana na watu mbalimbali ambao hawajui nyendo zao.

Nashtuka kuona tukiwa upande wa pili wa kivuko nami nalazimika kushuka na kuendelea na maisha mengine lakini ukweli ni kwamba bado mkazo zaidi kwenye eneo hilo la kivuko ambalo hukutanisha watu wengi kwa wakati mmoja unahitajika.

Hiyo itasaidia kuokoa maisha ya walio wengi dhidi ya janga la corona. Kwani pamoja na kuwepo kwa ndoo wenye maji na sabuni kwa ajili ya kunawa kwa abiria wanaoingia kwenye kutumia kivuko hivho lakini hakuna mkazo wala ulazima wowote uliowekwa kuhakikisha kuwa kila mtu anasafisha mikono yake kwa sabuni na maji tiririka badala yake ni utashi wa mtu binafsi anapojihisi kuwa kuna haja ya kufanya hivyo.

Mkazo huo siyo tu kwamba utawafanya watu kuwa wasafi bali utaokoa maisha ya waliowengi wakiwamo watoto wa shule ambao ni kama wameachwa bila uangalizi.

Aidha, kama itazipendeza mamlaka husika za Mkoa wa Dar es Salaam basi zitilie mkazo kidokezo cha mkuu wa mkoa kupenya hadi ndani ya vivuko ili kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi.

Kwani kwa sasa  ni kama ujumbe huo ulipo unaingilia sikio la kushoto na kutokea lile la kulia, haijulikani ni nani wa kulaumiwa kwenye uzembe huo unaoendelea licha ya mkuu wa mkoa kuzihimiza mamlaka zinazohusika kusimamia hilo.

Mmoja wa Askari anayehudumu katika kivuko cha Mgogoni amabye hakutaka jina lake litajwe kwa kudai siyo msemji, anasema kuwa bado baadhi ya watu wanaotumia kivuko hicho wmeendelea kuchukulia pao uvaaji wa barakoa hatua ambayo inawaweka hatarini.

“Kila siku tunahangaika na watu hapa kaka, unakuta mtu mzima kabisa lakini hajavaa barakoa ukimuuliza anakwambia mimi ndiye nanjua afya yangu, sasa unadhani utafanyaje, wazazi nao wanashindwa kuwangalia Watoto wanao wakati wa kwenda na kurejea nyumbani kwni hawana barakoa Pamoja na kwamba wanaingia kwenye pantone ambalo linahusisha watu wengi tofautitofauti, naamini mamlaka zinaangalia hili na zitakuja na majibu lakini kwa upande wetu tunajitahidi kufanya sehemu yetu,” anasema askari huyo.

Mtanzania Digital imefanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa mkoa, Amos Makala kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo bila mafanikio baada ya simu yake kutokupatikana.a

Hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutoa chanjo kwa mamia na maelfu ya Watanzania waliolengwa kufikiwa na chanjo hiyo nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles