Na WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
Serikali imetakiwa kuuweka Uchumi wa Bluu(Blue Economy) katika mpango wa maendeleo kutokana na fursa nyingi za zilizopo ikiwamo ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Mkufunzi wa Sheria za Kimataifa za masuala ya Bahari, Dk. Tumaini Gurumo ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa Wanahabari yaliyoandaliwa na Taasisi ya PS Counseling Consultants yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Dk. Tumaini, amesema kuna haja ya Serikali kununua Meli kubwa na vifaa vingine vya uvuvi ili kufaidika na rasilimali za baharini.
Ameeleza kuwa zipo fursa nyingi lakini ukosefu wa Meli unawakosesha Wanzania ajira na kushindwa kufikia rasilimali zilizopo katika kina kirefu cha bahari.
“Kukosekana kwa meli za mafunzo ya vitendo kwa ni kizuizi katika kupata fursa kwa sababu inawakosesha Watanzania ajira, ni vizuri serikali ikaweka Uchumi wa Bahari katika mipango kama ilivyo kwa Uchumi wa Kijani,” amesema.
Amefafanua kuwa Uchumi wa Bahari unaweza kuongeza kasi ya maendeleo nchini kwa sababu kuna rasilimali nyingi zinatoka baharini ikiwamo madini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa PS Counseling Consultants, Dk. Mkumbo Mitula, amesema elimu zaidi inahitajika kwa jamii ili kupata uelewa wa kutumia fursa za baharini.
“Uwekezaji katika uchumi wa Bluu ni muhimu lakini inahitajika elimu kuanzia ngazi za chini kama zinavyofanya nchi nyingine,” amesema Mitula.