KLABU ya Tottenham Hotspur inayoshiriki Ligi Kuu ya England, imemtambulisha rasmi leo Novemba 2, 2021 Antonio Conte kuwa kocha mkuu wa timu hiyo hadi mwaka 2023.
Conte raia wa Italia anachukua mikoba ya Mreno Nuno Espirito Santo aliyeachishwa kazi Jumatatu kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi hicho ikiwamo kipigo cha mabao 3-0 nyumbani kutoka kwa Manchester United, Jumamosi Oktoba 30,2021.
Kupitia mitandao yao, klabu ya Tottenham imethibitisha kuwa kuanzia sasa Conte ndiye atakayekinoa kikosi hicho hadi 2023, huku kukiwa na makubaliano ya kuongeza mkataba huo.
“Tunayo furaha kutangaza kuteuliwa kwa Antonio Conte kuwa kocha wetu mkuu kwa mkataba unafikia ukingoni msimu wa joto wa 2023 na kuna makubaliano ya kuongeza,” imesema klabu hiyo.
Conte alikuwa bado hajajiunga na klabu yoyote tangu alipoondoka Inter Milan katika majira ya joto, huku akikataa ofa mbalimbali.