23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Chupa milioni 2 za sumu ya pamba zawasilia Simiyu

Na Derick Milton, Simiyu

Bodi ya Pamba nchini (TCB) imeanza kusambaza sumu ya kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu ambapo tayari chupa milioni mbili zimepokelewa mkoani humo.

Idadi hiyo ya sumu ndiyo mahitaji halisi ya wakulima mkoani humo, ambapo kwa awamu ya kwanza zimewasili chupa 600,000 na ndani ya wiki hii wanategemea kusambaza chupa zote milioni mbili kwa wakulima.

Katibu Tawala msaidizi sehemu ya miundombinu Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mashaka Luhamba akipokea Sumu za kuua wadudu washambuliao zao la pamba kutoka kwa Mwakilishi wa Bodi ya Pamba mkoa wa Simiyu, Saidi Juma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukabidhi magari yaliyobeba dawa hizo kwa uongozi wa mkoa huo, Mwakilishi wa Bodi ya Pamba, Saidi Juma amesema sumu hizo zitatosha kwa wakulima wote mkoa mzima.

Amesema kuwa kwa awamu ya kwanza, wamepokea magari yanye chupa 600,000 huku kiasi kingine cha sumu kilichobaki kikitegemewa kuwasili ndani ya wiki hii.

Amesema kuwa sumu hizo ambazo zimeanza kupokelewa zitaanza kuwapelekwa kwa wakulima haraka iwezekanavyo ili waweze kupulizia kutokana na wadudu kuanza kushambulia zao hilo la pamba.

“Sasa hivi ndicho kipindi cha kupulizia sumu hizi kwani wadudu wanaanza kushambulia pamba, baada ya zoezi hili la kukabidhi sumu hizi zitatakiwa kuanza kupelekwa kwa wakulima moja kwa moja,” amesema Juma.

Aidha, Mwakilishi huyo amewatoa wasiwasi wakulima wa zao hilo, kuwa bodi imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mkulima anapata dawa za kutosha.

“Wakulima wasiwe na wasiwasi, dawa zipo za kutosha na kila mkulima atapata dawa kulingana na shamba lake, tunawaomba mara watakapopata dawa waanze kupulizia mara moja,” ameongeza Juma.

Hata hivyo, amezitaka kamati za kudhibiti wizi wa dawa hizo ambazo zimeundwa kuanzia ngazi ya wilaya hadi vitongoji katika mkoa huo kufanya kazi yake ipasavyo ili kusiwepo na tatizo la wizi wa sumu hizo au wakulima kuuziwa.

“Katika usambazaji wa awali kumetokea sumu hizi kuibiwa na kufanyiwa biashara, tunatoa rai na tahadhari kwa yeyote atakayehusika hatua kali za kisheria dhidi yake zitachukuliwa,” ameeleza Juma.

“Kule wilayani hadi vitongoji, kuna kamati ambazo zinahusisha wakulima wenyewe na viongozi wa serikali, ambazo zinadhibiti jambo hilo, ni wakati sasa wa kamati hizi kuanza kufanya kazi ili kila mkulima apate dawa kulingana na shamba lake,” amesema Juma.

Akipokea magari yenye sumu hizo, kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa, David Kafulila,Katibu Tawala msaidizi sehemu ya miundombinu Mhandisi Mashaka Luhamba amesema kuwa dawa hizo zimekuja wakati muafaka.

Mhandisi Luhamba amesema kuwa kama mkoa walifanya juhudi kubwa za kuhamasisha wakulima walime pamba na wengi waliitikia, hivyo kuletwa kwa dawa hizo itawezesha mkoa kufikia malengo yake ya kuzalisha tani 150,000.

“Baada ya kupokea sumu hizi, bila ya kuchelewa leo (Februari 28), zinaanza kupelekwa kwa wakulima, tayari tumetoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya kusimamia zoezi la ugawaji na kuhakikisha kila mkulima anapata dawa,” amesema Mhadisi Luhamba.

Mhandisi Luhamba ametoa onyo kwa mtu yeyote mwenye nia ya kutaka kuiba sumu hizo kuacha mara moja fikra hizo, kwani hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote ambaye atahusika ikiwemo kufikishwa mahakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles