Mlinda mlango huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 23, alitolewa nje dakika ya 52 baada ya kumchezea vibaya mshambuliaji wa Swansea City, Bafetimbi Gomis,katika eneo la hatari.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha Jose Mourinho, alishindwa kuongelea uamuzi huo ambao ulitolewa na mwamuzi Michael Oliver dhidi ya mlinda mlango wake.
Kutokana na kadi hiyo, Chelsea imeamua kukata rufaa ambayo inatarajiwa kusikilizwa na Chama cha Soka nchini Uingereza (FA) na kama wakikataliwa basi mchezaji huyo ataukosa mchezo dhidi ya Manchester City siku ya Jumapili kwenye Uwanja wa Etihad.
“Penalti ilikuwa ya wazi, lakini mwamuzi hakuwa sahihi kutoa kadi nyekundu kwa kosa hilo, hayo yalikuwa maamuzi magumu kwa Michael Oliver ambaye ni mwamuzi chipukizi,” alisema Mourinho.