33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chagonja ahamishiwa Zimamoto

BINa Mwandishi Wetu

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya utendaji ndani ya Jeshi la Polisi kwa kumhamisha Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, CP Paul Chagonja.

Habari za uhakika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana, zinasema Rais Magufuli amemteua Kamishina Chagonja kuwa Kamishina mpya wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Rais amefanya mabadiliko madogo ndani ya Jeshi la Polisi, amemhamisha Kamishina Chagonja tangu jana (juzi) kwenda Zimamoto…nadhani ni mabadiliko ya kawaida tu.

“Kama unavyojua Rais Magufuli anakwenda na falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ inaonekana amedhamiria kuboresha maeneo yote…huwezi kujua leo wizara hii kesho wizara nyingine, tunapaswa kujiandaa kila kukicha ndugu yangu,”kilisema chanzo chetu cha habari.

Kamishina Chagonja, amekuwa katika nafasi hiyo kwa muda mrefu tangu utawala wa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu Said Mwema.

“Chagonja ametumikia nafasi hii muda mrefu kidogo kuanzia wakati ule wa IGP Mwema mpaka sasa IGP Mangu (Ernest), naamini kutokana na uzoefu wake imeonekana anafaa kwenda huko,”kilisema chanzo hicho.

Kamishina Chagonja katika utumishi wake, amewahi kuwa Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi na baadae Mkuu wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam.

Januari 22, 2013, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimteua Pius Makuru Nyambacha kuwa Kamishina Jenerali wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

Hivi sasa nafasi hiyo inakaimiwa na Kamishina Jenerali Rogatius Kipali.

Alipotafutwa msemaji wa kikosi hicho, Puyo Nzalayaimisi simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.

Hata hivyo Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alipotafutwa kuzungumzia  mabadiliko hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita bila bila kupokewa.

LEMA

Januari mwaka huu bungeni mjini Dodoma, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alimshambulia kwa maneno makali Kamishna Chagonja, kwa kumtuhumu kuwa anaweza kuwa anashirikiana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi na kupora silaha.

Lema alitoa maneno hayo makali, wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Akichangia hoja hizo, Lema aliliambia Bunge kuwa Chagonja anaweza kuwa anahusika katika matukio ya ujambazi katika vituo vya polisi kwa sababu anataka kudhoofisha utendaji kazi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.

Katika maelezo yake hayo, Lema alilifananisha taifa na chumba kinachotumiwa na vijana wa kihuni kuishi ambacho hakina utaratibu unaoeleweka wa muda wa chakula na malazi.

“Mheshimiwa mwenyekiti, geto ni mahali ambapo watu wanaishi bila kufuata utaratibu, yaani katika geto, wakati wa kulala anayewahi ndiye anayelala kitandani. Geto chakula kinapopikwa kinaweza kuliwa hata kama hakijaiva, kwa hiyo nchi hii naifananisha na geto kwa sababu watu wanaiba fedha za umma kama wanavyotaka.

“Katika ripoti za Bunge zilizosomwa hapa jana (juzi) zimejaa wizi, kila ukurasa wa taarifa ya Zitto (aliyekuwa mwenyekiti wa PAC) ni wizi tu, wizi tu, hivi huu wizi utakwisha lini? Hata zile bunduki zinazoibwa katika vituo vya polisi zinaweza kuwa ni ‘sabotage’ (hujuma), zinazofanywa na Chagonja dhidi ya IGP,” alisema Lema.

Alisema amefanya uchunguzi wake binafsi uliobaini kuwa Jeshi la Polisi limegawanyika na kwamba haamini kama Rais Jakaya Kikwete (mstaafu) amekwishafanya mabadiliko ya uongozi ndani ya jeshi hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles