20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wamiliki shule binafsi waendelea kubanwa

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

SERIKALI imetoa wiki mbili kwa wamiliki wa shule za binafsi kuhakikisha wanawasilisha vibali vya ada wanazotoza hivi sasa na watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Pia imewataka wamiliki wa shule hizo kutoongeza ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia Januari, 2016 hadi watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Oliver Kato alisema kibali hicho kiwe kimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu kikielezea uhalisia wa viwango vya ada vinavyotakiwa kutozwa.

“Tumebaini kuna baadhi ya shule zisizo za Serikali zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu… utaratibu huu umekuwa ukifanywa na wamiliki hawa kila mwisho wa mwaka na kusababisha usumbufu kwa walimu,”alisema Oliver.

Alisema wamebaini baadhi ya shule, zimekuwa na tabia ya kuongeza ada bila kuwasiliana na Kamishna wa Elimu.

“Kutokana na tabia hii, tumeanza utaratibu wa kukagua vibali vyote kutoka shule moja hadi nyingine ili kukomesha vitendo hivi,”alisema Oliver.

Alisema wamiliki wote wanapaswa kuwasilisha vibali vyao tangu Desemba 3, mwaka huu ambapo Serikali imetoa wiki mbili kutekeleza agizo hilo.

Aliongeza kutokana na utaratibu wa awali  Waraka wa Elimu Na 4 wa mwaka 2008, uliweka viwango vya ada vinavyotozwa shule za msingi na sekondari binafsi na za Serikali.

Alisema ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za Serikali ni Sh 150,000 na za bweni ni Sh 380,000 kwa mwaka.

“ Waraka huo ulielekeza ongezeko lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika,”alisema Oliver.

Alisema ada zote kwa shule zisizo za Serikali zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na mamlaka husika.

Alizitaka pia kuwasilisha taarifa za Msajili wa Shule aliyeko Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada kinachotozwa kwa sasa na tarehe aliyopata kibali hicho.

Alisema serikali inatambua zipo shule ambazo zinatoa elimu kwa kufuata mitaala ya nje ya nchi na kueleza kuwa shule hizo haziguswi na agizo hilo.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alikaririwa na gazeti moja la kila siku akidai hawawezi kufungua shule zao ifikapo Januari, mwakani  kupinga hatua ya Serikali kuwazuia kupandisha ada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles