28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wang’ang’ania Ukuta

Katibu wa Kanda ya Pwani ya Chadema, Juma Mabina (kulia), akikabidhi bendera kwa moja wa vijana wa chama hicho kutoka Kigamboni, Simon Magest, kwa ajili ya maandalizi ya Operesheni Ukuta Dar es Salaam jana. Katikati ni Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Anatropia Theonest.
Katibu wa Kanda ya Pwani ya Chadema, Juma Mabina (kulia), akikabidhi bendera kwa moja wa vijana wa chama hicho kutoka Kigamboni, Simon Magest, kwa ajili ya maandalizi ya Operesheni Ukuta Dar es Salaam jana. Katikati ni Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Anatropia Theonest.

* Waanza kugawa bendera

NA EVANS MAGEGE,

KATIKA kile kinachoonekana ni msimamo thabiti wa kutokurudi nyuma dhidi ya mpango wa uzinduzi wa Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kugawa bendera zake kwa wafuasi wake ikiwa ni hatua mojawapo ya kuhamasisha jamii kuunga mkono operesheni hiyo.

Ugawaji wa bendera hizo ulianza rasmi jana kwa Kanda ya Pwani ambako viongozi mbalimbali wa chama hicho walifika katika ofisi hizo zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea katoni za bendera za chama hicho.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa bendera hizo, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casimir Mabina, aliwataka viongozi wote wa kanda hiyo kwenda kuwagawia wananchi bendera hizo ili kuongeza hamasa ya maandalizi ya uzinduzi wa Operesheni Ukuta ambayo inatarajiwa kufanyika Septemba mosi mwaka huu.

Katika ugawaji wa bendera hizo, Mabina ambaye aliambatana na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia chama hicho, Anatropia Theonest, aliwataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya kata pamoja na wafuasi wao kupeperusha bendera za chama hicho kwenye vyombo vya usafiri kuanzia Jumatatu wiki hii.

“Operesheni Ukuta ni lazima na tunawapeni bendera hizo mkawagawie wafuasi wetu na wale wanaounga mkono Ukuta na kuanzia Jumatatu peperusheni kila sehemu hadi siku ya uzinduzi, ikiwa ni kwenye gari, guta, bodaboda na baiskeli.

“Pia Chadema Kanda ya Pwani inawaomba wana Pwani wote na wananchi kwa ujumla kuungana katika kuujenga Ukuta bila kujali itikadi zetu kwa umoja tutasimama na kuushinda huu udikteta,” alisema Mabina.

Wakati Chadema wakiendelea na msimamo wao wa maandalizi ya kuzindua Operesheni Ukuta, tayari Rais John Magufuli ametoa onyo kwa kusema hajaribiwi na wala hataki nchi iingie kwenye vurugu, kwamba watakaokwenda kinyume na hapo atawashughulikia kikamilifu bila huruma.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli aliyoitoa hivi karibuni wakati akiwa ziarani Manyoni, mkoani Singida, inatajwa na wafuatiliaji wa mambo kuwa na kila aina ya tafsiri ya kutaka kuwadhibiti viongozi wa Chadema ambao wamenuwia kuihamasisha jamii kupinga mwenendo wa utawala wake kupitia kampeni ya Operesheni Ukuta.

“Nataka hao wanaotetea maandamano watangulie wao halafu wataona cha mtema kuni. Wasiwatangulize watoto wa masikini, wao wanakaa gesti wanalala, watoto wa masikini wanawapa viroba tangulieni huko, watangulie wao. Na mimi nataka watangulie wao siku waliyoipanga. Nataka nchi yenye nidhamu tutekeleze majukumu yetu tuliyoyapanga kwa ajili ya nchi hii.

“Lakini najua wakati mwingine ukikutana na nyoka ukampiga ukamuua, mkia lazima utikisike tu, unaweza kufikiri ni mzima kumbe nyoka alishakufa. Vyama vyenyewe (vya upinzani) vimechoka, wananchi wameshaona. Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa,” alisema Rais Magufuli.

Awali, Mabina alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa kupiga marufuku wapinzani kufanya mikutano ya hadhara umekiathiri chama hicho katika Kanda ya Pwani kwa sababu kila wanapotaka kufanya mikutano ya hadhara kupitia kwa viongozi wa kisiasa kwenye maeneo yao husika, Jeshi la Polisi linazuia.

“Wiki iliyopita tulikubaliwa kufanya mkutano wa hadhara pale Chalinze lakini muda mfupi kabla ya mkutano kuanza polisi hao hao wakazuia kwa sababu mkutano huo ulikuwa uhudhuriwe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye pamoja na viongozi wa Chadema nchi nzima, swali la kujiuliza hivi siku hizi Sumaye ndiye Chadema nchi nzima?” alihoji Mabina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles