23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wawili kortini kwa kutakatisha bil 14.9/-

court5

NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM

WATU wawili akiwamo raia wa Kongo, Jean Claude Bishikwabo (48), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa matano likiwemo la utakatishaji fedha wa Sh bilioni 14.9.

Bishikwabo alisomewa mashtaka jana na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo, mbele ya Hakimu Mkazi Respicius Mwijage, aliyedai kuwa alitenda kosa la kwanza kati ya Oktoba 2015 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam kwa kujipatia Dola za Marekani 700,000 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 1. 5. kutoka Kampuni ya Nzuri Trade Limited.

Lukondo alidai mahakamani hapo kuwa Bishikwabo alijipatia kiasi hicho kwa kusambaza korosho tani 1,710 kutoka Wilaya ya Masasi, Mtwara hadi Kampuni ya Nzuri huku akijua hana uwezo nalo.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Lukondo alidai kuwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 2015 na Januari 2016, akiwa jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa alifanya muamala wa dola za Marekani 700,000 ambazo ni zao lililotokana na fedha haramu za mazalia ya kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuzitakatisha kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya Biashara ya Afrika kisha kuzitoa fedha.

Mshtakiwa alikana yote na Wakili Lukondo alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mwijage alisema kesi ya utakatishaji fedha haina dhamana hivyo mshtakiwa atakaa rumande hadi kesi yake itakapotajwa Agosti 25, mwaka huu.

Katika tukio jingine, mfanyabiashara Nagma Mohammed (53), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu likiwemo la kuendesha shughuli za kimawasiliano kutoka nje ya nchi na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hasara ya Sh milioni 203.9.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini, alidai mshtakiwa huyo aliendesha shughuli hizo katika nyakati tofauti.

Wakili Mkini alidai kosa la kwanza la kuendesha shughuli hizo za mawasiliano alilifanya Mei na Julai 20, mwaka huu maeneo ya Upanga, Dar es Salaam kwa kutumia Mkongo wa taifa bila kuwa na kibali cha TCRA.

Alidai shtaka la pili ni kukwepa kodi alilolitenda Mei 19 na Julai 20, mwaka huu katika maeneo hayo hayo wakati akifanya shughuli za mawasiliano kupitia Mkongo huo wa taifa.

Wakili Mkini alidai shtaka la tatu ni kuisababishia TCRA hasara ambalo alilitenda kati ya Mei 19 na Julai 20, mwaka huu akiwa hana kibali cha kufanya shughuli hizo kwa kutumia mtambo wa GSM VOIP Gateway.

Hakimu Mashauri alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Mkini alidai kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles