29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

CAG afichua halmashauri zilivyoshindwa kufikia lengo la makusanyo

 NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/19 halmashauri nchini zilikusanya Sh bilioni 300 kati ya Sh bilioni 736 zilizopangwa kukusanywa.

Kiasi hicho ni chini ya asilimia 50 ya mapato yaliyokusudiwa huku zaidi ya asilimia 70 ya halmashauri zikishindwa kufanikisha malengo yake ya kila mwaka ya ukusanyaji mapato ya ndani.

Aidha katika mwaka 2017/18 halmashauri zilipanga kukusanya Sh bilioni 687 na kufanikiwa kukusanya Sh bilioni 281 tu ambazo ni sawa na asilimia 41 ya lengo lililowekwa.

Kichere amebainisha hayo kupitia ripoti ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu ukusanyaji mapato toka vyanzo vya ndani katika mamlaka za Serikali za mitaa.

Ukaguzi huo ulijumuisha miaka minne ya fedha kuanzia 2015/16 hadi 2018/19 ambapo timu ya ukaguzi ilichagua mikoa sita ya Iringa, Kigoma, Mwanza, Dodoma, Mtwara na Dar es Salaam wakati halmashauri ni Kinondoni MC, Kigamboni DC, Dodoma CC, Chemba DC, Iringa MC, Iringa DC, Kasulu TC, Kigoma DC, Mwanza CC, Sengerema DC, Mtwara MC na Masasi DC.

“Ukaguzi ulichochewa na matatizo ya kiutendaji ya halmashauri katika ukusanyaji wa mapato,” alisema Kichere.

HALMASHAURI

Ukaguzi huo ulibaini kwa miaka minne ya fedha kuanzia 2015/16 hadi 2018/19, karibu asilimia 70 ya halmashauri hazikufanikisha malengo yao ya ukusanyaji mapato. 

“Mahitaji ya rasilimali za kifedha ya kukidhi huduma tofauti za kijamii katika mamlaka za Serikali za mitaa yamekuwa yakiongezeka, mchango wa mapato unaendelea kupungua kutoka asilimia 28 mwaka 2015/16 hadi asilimia asilimia 11 mwaka 2018/19. 

“Hali hii inamaanisha kuwa Serikali inaingiza sehemu kubwa ya fedha kwenye bajeti za halmashauri kinyume na malengo ya kupunguza utegemezi wa ufadhili wa Serikali Kuu,” alisema Kichere.

SABABU

Katika ukaguzi huo, Kichere alisema mamlaka za Serikali za mitaa hazifanikishi malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo vyake kwa sababu hazijiwekei malengo halisi ya ukusanyaji. 

“Kwa wastani zaidi ya asilimia 53 ya halmashauri zilirekodi tofauti zaidi ya asilimia 20 kutoka malengo yaliyowekwa licha ya msisitizo uliowekwa na Serikali kwamba tofauti katika malengo yaliyowekwa hayapaswi kuzidi asilimia 20 kwa kila chanzo cha mapato,” alisema Kichere.

Kulingana na ripoti hiyo, sababu zingine ni pamoja na usimamizi duni, ukosefu wa mikakati madhubuti ya kupanua wigo wa ushuru katika halmashauri na upungufu wa watumishi kati ya asilimia 23 na 70 katika idara za fedha na biashara.

“Maofisa wachache waliokuwepo walikosa ujuzi wa kutosha wa makadirio ya mapato na kukagua kodi kwa vyanzo vya mapato kama vile ushuru wa hoteli na ushuru wa huduma.

“Maofisa hawakuwa na maarifa ya kutosha na uwezo wa kutosha kuendesha mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki (LGRCIS) na mashine za kukusanya mapato (PoS),” alisema Kichere.

Alisema pia kukosekana kwa mafunzo ya mara kwa mara na kucheleweshwa kwa mawasiliano ya mabadiliko katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato kulisababisha pengo la maarifa kwa watumiaji wa mifumo.

Kichere alisema mifumo ya ukusanyaji wa mapato haikuunganishwa vizuri na akaunti kadhaa za benki na kusababisha utengamano kati ya ripoti za mapato zinazotokana na mifumo hiyo na zile zinazotokana na benki.

SHERIA ZILIZOPITWA NA WAKATI

Ukaguzi ulibaini kuwa halmashauri saba kati ya 12 zilizotembelewa zilikuwa zikitumia sheria ndogondogo ambazo hazikupitiwa upya kuzioanisha na viwango vya sasa vya soko, hususan ada na ushuru unaokusanywa kutoka kwenye masoko.

Kulingana na ripoti hiyo, katika halmashauri tatu zilizotembelewa takribani Sh milioni 104.2 hazikukusanywa kwa mwezi kwa sababu ya matumizi ya bei ambayo yalikuwa chini kuliko bei ya soko.

“Kutotekelezwa kwa sheria ndogo ndogo zinazopitishwa na mabaraza ya halmashauri ni kati ya sababu, maofisa waliohojiwa pia walionyesha kuwa kuna kuchelewa kupata idhini kutoka serikalini kwa sheria ndogo ambazo wakati mwingine huchukua hadi miezi sita.

“Kumesababisha kutoboreshwa kwa ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vilivyopo kwa sababu ya matumizi ya viwango vya zamani,” alisema Kichere.

 WAKUSANYA USHURU

Ukaguzi ulibaini pia mamlaka ya Serikali za mitaa hazikuwasimamia vyema wakusanya ushuru katika maeneo yao. 

“Wakusanya ushuru walikuwa wanakosa zana za ukusanyaji wa mapato na uwezo wa kutosha kuwawezesha kutumia mifumo ya ukusanyaji wa mapato na vifaa. Hii ilisababisha kuongezeka kwa makosa.

“Ukaguzi ulibaini kuwa halmashauri hazikufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba ya mawakala wa kukusanya mapato kama ilivyoainishwa katika mwongozo wa wakala wa kukusanya mapato ya nje ya mwaka wa 2016. 

“Halmashauri hazikuchukua hatua sahihi za marekebisho kwa wakusanya ushuru ambao hawakuzingatia masharti ya mikataba yao,” alisema Kichere.

Alisema hata ripoti za uchunguzi wa Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2015/16 hadi 2018/19 katika idara za fedha za halmashauri na sekretarieti za mkoa hazikuwa zikitoa taarifa kamili na za kina juu ya utendaji wa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri, badala yake zina muhtasari wa mafanikio ya malengo ya jumla ya ukusanyaji wa mapato.

MAPENDEKEZO

Kichere alishauri Serikali itathmini ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kushughulikia makosa yote ili kuhakikisha mifumo inafanya kazi vizuri.

“Mfumo lazima pia uweze kuonyesha kwa usahihi na kwa wakati mapato yaliyokusanywa na kuweza kutoa ripoti zinazohitajika kwa ajili ya kufanya maamuzi.

“Halmashauri ziwe na mipango madhubuti ya ukusanyaji wa mapato ambayo pia itahusisha mapitio ya mara kwa mara ya sheria ndogo, zikague mara kwa mara utendaji wa wakusanya ushuru katika maeneo yao na kuchukua hatua za haraka kurekebisha mapungufu,” alisema Kichere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles