24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CAF yaishika pabaya Yanga

Jerry Muro
Jerry Muro

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KLABU ya soka ya Yanga imesema haiwezi kulipa kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) asilimia tano ya mapato yaliyotokana na mchezo wa juzi wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa madai kuwa hawakuingiza mapato yoyote.

Yanga iliondoa kiingilio katika mchezo huo wa pili wa Kundi A katika michuano hiyo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi wajitokeze kuishangilia timu hiyo.

Katika mchezo huo ambao Yanga ilipata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe, mashabiki walianza kuingia uwanjani mapema tangu saa 8:40 asubuhi ambapo mageti yalifungwa saa 11:50 baada ya uwanja kujaa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema klabu hiyo ipo tayari kulipa asilimia 15 ya gharama za uwanja lakini si kulipa asilimia tano ya CAF kwa sababu hawakupata mapato yoyote.

“Mashabiki walioingia uwanjani hawakulipa kiingilio hivyo hatutaweza kuilipa CAF kwa sababu hakuna fedha tulizopata kutokana na mchezo wa jana (juzi), katika makubaliano ya awali hatukukubaliana kuilipa CAF bali tulisema tutalipa gharama za mchezo ‘direct cost’ ikiwamo uwanja,” alisema Muro.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema kikao cha awali kilichofanyika jijini Cairo, Misri kabla ya mchezo huo, Yanga ilikubali kulipa gharama za mashabiki wake pamoja na gharama za uwanja asilimia 15, mchezo 10%, CAF 5%, TFF 5% na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 18%.

“Kama Yanga iliamua kuingiza mashabiki wake bure uwanjani kikao hakitambui suala hilo kwa kuwa halikujadiliwa bali walikubali kuwalipia mashabiki wao bila kuathiri gharama watakazodaiwa kwenye mchezo,” alisema.

CAF iliagiza kwamba mashabiki wanaotakiwa kuingia uwanjani wasizidi 40,000 ili kuepusha msongamano unaoweza kusababisha vurugu zisizo za msingi, hivyo inahesabika kuwa Yanga ililipia idadi ya mashabiki waliotajwa na shirikisho hilo linalosimamia michuano wanayoshiriki.

Aidha, Mwesigwa alisema klabu ya Yanga pia itahusika kulipa gharama za uharibifu uliofanyika  uwanjani ambazo zipo nje ya asilimia 15 wanayotakiwa kulipa kwa ajili ya uwanja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles