23.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 2, 2024

Contact us: [email protected]

BRELA yawataka wamiliki wa viwanda, kampuni kusajili bidhaa zao

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wamiliki wa viwanda na kampuni kusajili bidhaa zao ili kupata masoko ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo, Oktoba 1, 2024, katika Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda yaliyofanyika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam, Ofisa Leseni wa BRELA, Ndeyanka Mbowe, alisema wako kwenye maonesho hayo ili kusajili viwanda, biashara, na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili bidhaa zao.

“Tulianza mabadiliko ya kidijitali na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Wamiliki wa viwanda na kampuni sasa wanasajili bidhaa zao mtandaoni,” alisema Mbowe.

Alifafanua kuwa tangu mwaka 2018, BRELA imekuwa ikiendesha shughuli za usajili wa viwanda kwa mfumo wa kisasa, huku ikilenga kuongeza ufanisi na kuwafikia wateja kwa njia rahisi zaidi.

“Usajili wa kampuni au kiwanda unakupa nafasi kubwa ya kushiriki katika maonesho ya ndani na nje, ambayo yanatoa fursa ya kutangaza bidhaa yako,” aliongeza.

Mbowe aliwahimiza wamiliki wa viwanda kusajili biashara zao kabla ya kuanza shughuli yoyote, ili kuhakikisha wanatumia maeneo yaliyokubalika kisheria kwa uzalishaji.

Hata hivyo, alisema mwitikio bado ni mdogo kwenye maonesho hayo, na akatoa wito kwa wenye viwanda na makampuni kuendelea kusajili bidhaa zao.

Baadhi ya wananchi walitembelea banda la BRELA na kupata elimu kuhusu usajili wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Godwin Claudi, mmoja wa wageni wa maonesho, alisema: “Leo nimeelewa kazi za BRELA, na nimehamasika kuanzisha kiwanda changu kidogo baada ya kupata elimu hii.”

Plakseda Luis, aliyesajili kiwanda chake, alikiri kuwa biashara yake sasa inaenda vizuri baada ya kusajili kupitia BRELA na kushiriki maonesho mbalimbali kwa ajili ya kutangaza bidhaa zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles