28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI: Kipunguni wabuni mbinu kuwashughulikia wanaokatili watoto

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Sauti nyingi zinapazwa kila uchao kuhusu ustawi wa watoto kutokana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini ambavyo vingi vinaumiza na kufifisha kizazi kinachotarajiwa kuwa cha kesho.

Ripoti ya takwimu za Uhalifu na Usalama Barabarani ya kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2023 iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania inaonyesha waathirika 15,301 waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa unyanyasaji wa kijinsia ikilinganishwa na waathirika 12,163 wa mwaka 2022 sawa na ongezeko la waathirika 3,138 (asilimia 25.8).

Kulingana na ripoti hiyo matukio mengi ya ukatili wanayofanyiwa watoto yanafanyika ndani ya familia na kwenye jamii ambayo ni ubakaji, ulawiti, kutupa watoto, kutelekeza familia na ukeketaji.

Ripoti hiyo imeainisha makosa yenye idadi kubwa ya waathirika kuwa ni ubakaji (8,185), ulawiti (2,382), mimba kwa wanafunzi (1,437), kuzorotesha wanafunzi kimasomo (922) na shambulio la aibu (396).

Mikoa iliyotajwa kuwa na changamoto kubwa ni Arusha (1,089), Morogoro (976), Tanga (884), Kinondoni (789) na Mjini Magharibi (788) wakati yenye idadi ndogo ni Kusini Pemba (100), Kusini Unguja (102), Kaskazini Pemba (103), Tarime, Rorya na Kaskazini Unguja (161 kila mmoja).

Kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa kabisa nchini.

Mojawapo ya jitihada hizo ni zile zinazofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Jamii Kipunguni lenye makao yake makuu Kipunguni, Dar es Salaam ambalo limekuwa likibuni mbinu mbalimbali za kutokomeza vitendo vya unyanyasaji kijinsia kwenye jamii.

Mbinu ya hivi karibuni iliyobuniwa na Sauti ya Jamii Kipunguni ni ya kuwaunganisha watoto pamoja, kuwapa mafunzo na kuwawezesha kuchaguana na kuunda uongozi wao.

Kiongozi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, anasema anaamini mbinu hiyo itafanikisha kwa kiasi kikubwa kupunguza au kutokomeza kabisa ukatili kwa watoto kwa kuwa watakuwa huru kusema yanayowasibu kwa viongozi wao kisha kupatiwa ufumbuzi.

“Tunaamini silaha ya kupinga ukatili siyo moja, tunajua ziko silaha nyingi lakini kila mmoja anatakiwa kushiriki kupinga ukatili kwahiyo tunabuni mbinu tofauti lengo turudi kwenye mstari kwa sababu takwimu za ukatili zinazidi kuongezeka na wanaofanya ukatili wengi ni watu wa karibu,” anasema Bishagazi.

Anasema mbinu hiyo ya uongozi wa watoto mitaani inalenga kutanua wigo wa kupinga ukatili dhidi ya watoto na kushirikisha watoto wawe na sehemu yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe.

“Tumekuwa tukiona watu wazima wana taratibu na uongozi wao kwenye jamii, kwenye vijiwe vya bodaboda kuna uongozi, vijiwe vya kahawa kuna uongozi, mtaani tuna ujirani mwema tuna uongozi lakini watoto hawana uongozi licha ya kwamba wanajumuika kwa pamoja, lakini watoto wadogo hawana uongozi, tuliwakusanya watoto tukawashirikisha kwamba tunataka wawe na uongozi wao wakafurahi sana, wamekaa wakachagua uongozi wao.

“Lengo ni wao kuweza kutanua wigo wa kuripoti vitendo vya ukatili, mtoto anaweza kufanyiwa ukatili akashindwa kumwambia baba au mama lakini anaweza kumueleza rafiki yake,” anasema.

Anasema katika harakati wanazozifanya wamebaini kuwa watoto wengi wanaofanyiwa ukatili wamekuwa wakishindwa kuwaeleza wazazi na walezi wao lakini wanaweza kuwaambia marafiki zao.

“Tulipolileta suala hili kwa wazazi wengi wametuunga mkono, tulikuwa tunawaza kupata watoto kati ya 20 hadi 25 lakini tumepata watoto 95 na wengine wanaendelea kuja kujiunga. Watoto walikaa wenyewe wakatengeneza uongozi wa muda na wakapendekeza utaratibu gani utumike kumchagua kiongozi wao,” anasema.

KUBAINI VIASHIRIA VYA HATARI

Bishagazi anasema watoto hao wamefundishwa pia kubaini viashiria vya ukatili mfano katika eneo la Kipunguni ambako huwa kuna masuala ya ukeketaji na mengine hivyo wakiona dalili watoe taarifa.

“Mfano mtoto anaweza akawa anaishi na mjomba lakini akaona si dalili za kawaida anamletea zawadi, anamuita chumbani au anamshika sehemu ambazo hazitakiwi, hizo ni dalili za ukatili anatakiwa kuripoti kwa kiongozi wake,” anasema Bishagazi.

Anasema pia watoto hao wamefundishwa kubaini viashiria vya ndoa za utotoni kwa kuwa mjini na vijijini zifanyika hivyo itasaidia kujua na kuwalinda wenzao.

“Tumewafundisha dalili za kugundua kama unataka kuozeshwa akiwa mdogo, mfano wakiona mama anaanza kuuliza maswali kwa kulinganisha elimu na kuolewa, anaongelea mambo ya ndoa, raha ya kuolewa, faida za kuolewa au baba anadhihaki elimu, anatoa mifano ya watu ambao hawajasoma au waliolewa na kufanikiwa na waliosoma wakafeli maisha.

“Ukiona wageni wanakuja na kama kwenye kabila lenu mahari ni ng’ombe na wao wanajadili ng’ombe wakati nyumbani hamfugi, ukaona baba anafoka kuhusu mambo ya shule toa taarifa na sisi tutajua kama ni kwa wema au ni ndoa za utotoni.

“Mfano kipindi cha shule mtoto anaambiwa asiende kuna wageni watakuja abaki, anapewa chai au vinywaji awapelekee, awasalimie halafu wengine wanapiga vigelegele kama ni binti mdogo ujue ndiyo dalili za kuelekea kuozeshwa…ukiona binti mwenzako haonekani mtaani fikisha taarifa kwa kiongozi wako na kwetu pia,” anasema.

Kwa mujibu wa Bishagazi watoto hao pia wamepanga vipaumbele vyao ambapo wameunda kamati za elimu, mazingira, ukatili ambazo zitakuwa na kazi ya kufanya tathmini ya hali ilivyo kisha kila mwezi watatoa taarifa.

“Wale walio kwenye kamati ya elimu tumewaelekeza kama mwenzao haendi shule waende wakamuone na kumuuliza, wakamuone na mzazi na wakileta mrejesho sisi tutajua jinsi ya kushughulikia tatizo hilo. Pia watakuwa na vipaumbele vyao ambavyo wanataka serikali ya mtaa iwafanyie na katika bajeti mbalimbali.

“Tunajua ndiyo tunatengeneza viongozi wa baadaye, watajua jinsi ya kuchagua viongozi kwa kufuata demokrasia…mtoto ambaye tuliona kwamba anafaa kuwa kiongozi wao hawakumtaka, wamechagua mtu wanayemtaka kwa vigezo vyao wenyewe,” anasema.

Kiongozi huyo wa Sauti ya Jamii Kipunguni anasema; “Tumewaambia watoto kuna kampeni inasema usinishike hapa kwangu, lakini sisi tumekwenda mbali zaidi tumewaambia huruhusiwi kushikwa popote pale na mtu yeyote yule, tumewafundisha watoto kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kushika hata nywele, kucha.

“Kama mama anakushika mwambie umeshafundishwa asikushike, kama ni mama mdogo anakuogesha mwambie usinishike hapa, hata kama unaumwa mwambie baba nimefundishwa anishike mama,” anasema Bishagazi.

KAZI ZA VIONGOZI

Bishagazi anasema kazi za viongozi ni kutatua migogoro midogo midogo na kuwa tayari kuwapokea wenzao na kuwasikiliza hasa kesi zinazohusu masuala ya ukatili.

“Watoto wanacheza wanaumizana halafu wakienda kwa wazazi wao wakati mwingine hawapati jibu sahihi kulingana na mzazi alivyoshinda, alivyolelewa au alivyokuzwa na wazazi wengine hawana uwezo wa kusikiliza kesi za ukatili.

“Kuna mzazi unakuta ana changamoto nyingi, ana mikopo ya kausha damu, mwingine ana kesi kadhulumiwa mirathi, mme wake anamfanyia ukatili au mke wake anamfanyia ukatili kwahiyo mtoto akienda kumpa taarifa jibu analopewa linaweza lisiwe rafiki,” anasema Bishagazi.

Anasema pia wamewapatia mafunzo viongozi wa watoto jinsi ya kutatua migogoro midogo kama vile kutukanana, kunyang’anyana vitu na mingine na kesi ambazo wanaona ngumu wanaziwasilisha katika taasisi hiyo.

Katibu wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Sada Ramadhani, anasema watoto wanapitia changamoto nyingi kama kubakwa, kulawitiwa au kupigwa lakini hawana sehemu ya kusemea na kwamba kupitia michezo mtoto anaweza kumweleza mwenzake changamoto anayopitia.

“Tunajua watoto wengi wako huru kuongea na wenzao hivyo, baada ya kuchaguana tunaamini tutapata taarifa za watoto waliofanyiwa ukatili na wanaohitaji msaada,” anasema Sada.

MWENYEKITI WA WATOTO

Mwenyekiti wa Watoto hao, Yasinta Mponze, anaishukuru Sauti ya Jamii Kipunguni kwa kuwakusanya na kuwapa elimu iliyowezesha kuunda uongozi wao kwa lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia.

“Mtoto mwenzetu akionewa au kufanyiwa kitendo ambacho hajakipenda anaweza kufikisha taarifa kwangu au viongozi wengine kama vile katibu na kupatiwa ufumbuzi,” anasema Mponze.

Sauti ya Jamii Kipunguni wanasema juhudi hizo zikifanyika na kwa nia njema waliyonayo zitafanikisha kuzuia ukatili kwa watoto na kwamba wanatamani wakiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwakani, watoto wa Kipunguni watoe mrejesho wa umoja huo na mambo yaliyofanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles