Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuwa imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wa watoa huduma ndogo za fedha nchini, yakiwemo kutokupewa mikataba ya mikopo, kutokupewa taarifa ya mikopo wanapotaka kulipa na kuchelewa kujibiwa maombi yao ya kulipa mapema.
Mbali na hayo, pia wateja hao hutozwa riba na gharama zingine kubwa wanapotaka kulipa mikopo mapema, jambo liloifanya BoT iwaagize watoa huduma hao waliolalamikiwa kuchukua hatua.
Taarifa iliyotolewa na mwishoni mwa wiki na Meneja, Idara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni wa BoT, Victor Tarimu ilieleza kwamba hatua ambazo zimetakiwa kuchukuliwa taasisi hizo ni pamoja na kuweka mfumo wa kutatua malalamiko ya wateja kwa mujibu wa Kanuni ya 54 ya Kanuni za Watoa Huduma Ndogo za Fedha (Wasio Pokea Amana) za Mwaka 2019, katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Mei 22, mwaka huu.
Tarimu alisema kuwa pia taasisi hizo zimetakiwa kukusanya na kuwasilisha Benki Kuu taarifa za malalamiko yote zikionyesha jina la mlalamikaji, namba ya simu ya mlalamikaji, makazi ya mlakamikaji mkoa, wilaya na tawi husika pamoja na kiasi cha mkopo husika, tarehe ya kukopa, riba, tozo mbalimbali, kiasi cha rejesho (installment), kiasi kilicholipwa mpaka muda huo, muda wa kuiva kwa mkopo; kiini cha malalamiko, tarehe ya kupokea lalamiko na hatua zinazochukuliwa na kampuni husika.
“Kutatua malalamiko tajwa katika kipindi cha wiki tatu tangu tarehe 22 Mei 2020 na malalamiko yaliyoshindikana yawasilishwe Benki Kuu pamoja na sababu za kushindwa kutatuliwa.
“Kuzingatia matakwa yote ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 iliyoanza kutumika tarehe 1 Novemba 2019 wakati wakiendelea na mchakato wa kuomba leseni Benki Kuu,” alisema Tarimu.
Aidha, alisema kuwa Benki Kuu itachukuwa hatua za kisheria, ikiwemo kuwafungia biashara watoa huduma ndogo za fedha watakaokaidi maelekezo yaliyoainishwa.
Pamoja na hali hiyo BoT imewataka wateja wote wa watoa huduma ndogo za fedha nchini wenye malalamiko kama yaliyoainishwa katika taarifa hii kuyawasilisha kwa maandishi kwa mtoa huduma husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kutatuliwa na nakala ya malalamiko hayo itumwe kwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Taasisi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania.